Advertisements

Thursday, May 26, 2016

‘PROFESA MAGHEMBE NI MZIGO MWEPESI

Mbunge wa Bunda Mjini (Chadema), Ester Bulaya jana alichafua hali ya hewa bungeni baada ya kusema kwamba Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe ni mzigo na mwepesi kama ‘tishu’ kwa sababu hana uwezo wa kusimamia mambo mazito yaliyopo katika wizara hiyo, kama vile migogoro ya wananchi na hifadhi za Taifa.
“Huyu waziri ni mzigo kama alivyowahi kusema (Abdulrahman) Kinana. Mimi nasema yeye ni mwepesi kama tishu, hawezi kuisaidia wizara hii nyeti,” alisema mbunge huyo jana wakati akichangia hotuba ya Wizara ya Maliasili na Utalii.
Hata hivyo, Waziri wa Nchi, Sera, Uratibu na Bunge, Jenista Mhagama alisimama na kuomba mwongozo wa mwenyekiti juu ya mbunge huyo kutumia maneno ya kuudhi ambao uliungwa mkono na Mwenyekiti wa Bunge, Andrew Chenge aliyemtaka Bulaya kufuta neno mwepesi kisha aendelee na hotuba yake. Hata hivyo, Bulaya alikataa kufuta neno hilo na kusema wabunge hawaamuliwi maneno ya kutumia.
Chenge aliendelea kumsihi mbunge huyo kufuta neno hilo na katika mabishano hayo yaliyodumu kwa dakika tatu, baadaye, Bulaya alikubali kuondoa neno ‘tishu’ na kuliacha neno mwepesi na kuruhusiwa kuendelea kuchangia.
“Mwenyekiti sitafuta neno mwepesi, kama neno ‘tishu’ linawakera basi naliondoa libaki mwepesi,” alisema Bulaya.
Katika mchango wake, Bulaya alisema wananchi wanaoishi katika hifadhi zilizopo jimboni mwake wananyanyaswa na askari wanyamapori wakati Serikali imeshindwa kuwatengenezea mazingira mazuri ya kuishi.
Alimtaka waziri huyo kushughulikia kero zote zinazowakabili wananchi wa Bunda akisema Serikali haiendeshwi kwa maneno matupu, bali vitendo na dhamira ya dhati ya kuwahudumia wananchi.
“Tatua matatizo jimboni kwangu ili niweze kukupima kama wewe ni mzito au mwepesi,” alisema mbunge huyo akimwambia Profesa Maghembe.
Baada ya Bulaya kumaliza muda wake, mbunge aliyefuatia alikuwa Abdallah Ulega wa Mkuranga (CCM) ambaye alisema kuna haja ya wabunge kupimwa kama wamelewa getini ili kujua akili zao.
“Kijana aliyefunzwa vizuri hawezi kumtukana mzee kama yule (Maghembe). Kama suala ni uwaziri basi aangalie hata umri wake kabla ya kuzungumza... Naungana na aliyesema wabunge tupimwe vilevi kabla hatujaingia humu ndani. Unaweza kujenga hoja yako bila kutukana, huhitaji kutukana ili waziri atekeleze madai yako,” alisema mbunge huyo.

CHANZO: MWANANCHI

4 comments:

Anonymous said...

Hongera sana mama Bulaya,huyu waziri ni mzigo kabisa kabisa.inabidi apelekwe takukuru kabisa kabisa.mtu mbaya sana nimesikitika sana kwa kuwaingiza watanzania tena wazawa kwenye umasikini katika nchi yao bila kujali hawa watu wanaenda kupoteza mitaji yao,kitendo cha kusimamisha ghafla uuzaji viumbe hai bila kujali watu wamelipia leseni,vibali na wanalisha ni kitendo kibaya sana tena cha kulaaniwa.amewaingiza watu kwenye matatizo makubwa wanamikataba nje wengine walishapokea malipo ya awali (advances) , watalipa na nini? wana leseni halali na quota za mwaka mzima 2016 wamelipia.hii serikali siko inakotupeleka ila inatupeleka kwenye aibu na shida za kujifanyafanya wanatumbua bila kuzingatia au kufuata sheria na hii itawawaghalimu kwa maana watu wataenda mahakamani na serikali itashindwa watalipa nini??? amewafungulia kesi ya uhujumu uchumi wakati watu wana vibali halali kwa kweli inauma na inasikitisha sana lakini siku itafika mungu ataona haya mateso na uonevu huu unakwish.

Anonymous said...

Annony namba moja hapo juu kilio cha waloshikwa pabaya! Hebu tueleze hivo vibali ulikuwa mnavipata kwa uwazi gani na njia ipi? Hongera Mhe. Rais Magufuli. God bless Tanzania.

Anonymous said...

Waliopokea advance payment waseme walilipa kodi kiasi gani? Utapeli tu. Hapa kazi tu!

Anonymous said...

MNABWABWAJA TU HATA HAMJUI KUWA HII BIASHARA NI HALALI INAFANYWA NA WATANZANIA ,UNAPOLIPIA VIBALI NDIYO MAANA INAKUWA TAYARI UMEILIPA SERIKALI,SASA KAMA SERIKALI YA AWAMU YA TANO HAIHESHIMU SHERIA,INA MAANA INAWATAPELI WATANZAANIA AMBAO WAMELIPIA GHARAMA ZOTE ZA HIVI VIBALI,VINAPATIKANA KIHALALI KABISA NI BIASHARA YA KIMATAIFA INASIMAMIWA NA CITES-GENEVA KWA KUWA HAMJJUI HAKI ZENU NA HII BIASHARA TUTABAKI KUPIGA KELELE TU.WATANZANIA MTAENDELEA KUWA MASIKINI TU BILA KUJUA HAKI ZENU