Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa Balozi Tuvako Manongi akiwa ameshika medali ya Dag Hammarskjold waliyotunukiwa mashujaa watatu watanzania ambao wamepoteza maisha mwaka jana wakati wakihudumu katika Misheni za kulinda Amani za Umoja wa Mataifa. kushoto kwa Balozi ni Luteni Kanal George Ita'ngare, mshauri wa masuala ya kijeshi katika Uwakilishi wa Kudumu na kulia ni Bw,Herve Ladsous, Katibu Mkuu Msaidizi Mwandamizi na Mkuu wa Idara ya Operesheni za Ulinsi wa Amani za Umoja wa Mataifa.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon, akimvisha Bibi Yacine Mar Diop medal maalum ya Kapteni Mbaye Diagne ambaye alikuwa ni mume wa Bibi Yacine, Kapteni Diagne aliuawa mwaka 1994 wakati wa mauaji ya kimbali ya Rwanda. medali hiyo maalum imebuniwa na Baraza la Usalama kwa kutambua ushujaa na uthubutu wake na kujituma kwake kwa hali ya juu hadi kupelekea kupoteza maisha. Kapteni Diagne anakumbukwa kwa namna alivyookoa maisha ya mamia ya wanyarwanda kwa kuwaficha kwenye lori na kuwapeleka mahali salama kabla ya yenye mwenyewe kuuawa.
Na Mwandishi Maalum, New York
Umoja wa Mataifa, jana Mei 19 umefanya hafla maalumu ya siku ya Kimataifa ya Walinzi wa Amani wanaohudumu katika Misheni mbalimbali za Kulinda Amani chini ya kofia ya Umoja wa Mataifa.
Katika hafla hiyo jumla ya walinzi 129 wanajeshi na polisi waliopoteza maisha mwaka jana kwa kushambuliwa na makundi ya wapiganaji wenye silaha, matukio ya kigaidi, ajali na kuumwa walikumbukwa na kuenziwa kwa mchango wao.
Miongoni mwa Mashujaa hao 129 kutoka nchi 50, wapo mashujaa watatu kutoka Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mashujaa hao ni Sgt. Musa Abdrahamani Yusuf, Cpl. John Leornad Mkude na Pte. Juma Ally Khamis.
Hafla hiyo maalum ya kutambua mchango wa walinzi hao wa Amani na ambao wamejitolea maisha yao kwaajili ya kuwalinda na kuokoka maisha ya wananchi wasiokuwa na hatia katika nchi zinazokabiliwa na vita na migogoro ya wenyewenye kwa wenyewewe iliongozwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon.
Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, Balozi Tuvako Manongi, ndiye aliyepokea medali maalum za mashuja hao watatu kwa niaba ya familia zao. Medali waliyotunukiwa mashujaa hao na wengine inatambuliwa kama medali ya Dag Hammarskjold.
Hafla ya mwaka huu, pamoja na kutambua mchango wa mashujaa hao 129 , pia ilitambua kwa namna ya pekee na kwa mara ya kwanza, mchango na kujitolea wa hali ya juu ulikofanywa na Kapteni Mbaye Diagne raia ya Senegal, aliyepoteza maisha mwaka 1994 wakati akiokoa maisha ya wanyarwada wakati wa mauaji ya kimbali.
Kapteni Mbaye Diagne ameeziwa rasmi katika maadhimisho ya mwaka huu kwa kupewa medali maalum iliyopewa jina la Medali ya Mbaye Diagne, medali ambayo alikabidhiwa mjane wa Mbaye Bibi Yacine Mar Diop huku akishuhudiwa na watoto wake wawili.
Kapten Mbaye Diagne alikuwa mwangalizi wa Amani nchini Rwanda, kwa ushujaa mkubwa na bila ya kujali hatari iliyokuwa ikimkabili alitumia lori kuwaficha na kuwapeleka mahali salama mamia ya wanyarwada wakati wa mauaji ya kimbali ya Rwanda.
Kwa kutambua ushujaa na uthubutu wake huo, Baraza la Usalama lilibuni mwaka 2014 medali ya Kapten Mbaye Diagne ambayo watakuwa wanatunukiwa wanajeshi, polisi na raia ambao wameonyesha uthubutu na ushupavu wa hali ya juu kiasi cha kupoteza maisha yao wakati wakitekeleza majukumu yao.
Akizungumza wakati wa halfa hiyo ambayo ilibeba majonzi ya aina yake, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon, alieleza kwamba, hadi kufikia mwezi wa nne mwaka huu, jumla ya walinzi wa Amani 3,400 wakiwamo wanajeshi, polisi na raia walikuwa wamepoteza maisha tangu kuanzishwa wa shughuli za ulinzi wa Amani kwa kofia ya Umoja wa Mataifa miaka 70 iliyopita.
“Wakati leo tunawaenzi na kuwakumbuka mashujaa hawa 129 kutoka mataifa 50 waliopoteza maisha yao mwaka jana wakati wakitekeleza jukumu la kuwalinda wananchi wengine, jana ( Mei 18) walinzi wengine watano wanaohudumu huko Mali wamepoteza maisha baada ya kushambuliwa”. Akasema Ban Ki Moon kwa huzuni.
Balozi Tuvako Manongi akiandika katika kitabu cha kuwaeni walinzi wa amani wa Umoja wa Mataifa waliopotea maisha mwaka jana. miongoni mwa mashujaa 129 waliokumbukwa wapo watanzania watatu ambao ni Sgt. Musa Abdrahamani Yusuf, Cpl John Leornad Mkude na Pte. Juma Ally Khamis
Sehemu ya washiriki wa hafla ya siku ya Kimataifa ya Walinzi wa Amani wa Umoja wa Mataifa hafla hiyo ilifanyika jana Mei 19.
No comments:
Post a Comment