ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, May 28, 2016

UZEMBE WA MAOFISA WAMKERA DC

Tatizo la wananchi kuendelea kutumia maji ya madimbwi ambayo siyo salama na kujisaidia vichakani kwa kutokuwa na vyoo, kunatokana na uzembe wa maofisa wa afya na wahandisi wa maji.
Mkuu wa Wilaya ya Bukombe mkoani Geita, Amani Mwenegoha amesema wahandisi wa maji husubiri kufanya kazi za miradi badala ya kwenda vijijini kuwahamasisha wananchi kuchimba visima vya maji safi pamoja na matumizi bora ya vyoo.
“Bado suala la majisafi na salama ni tatizo, lakini hili linatokana na maofisa afya na wahandisi wa maji kukaa ofisini hawafanyi kazi mpaka kuwe na mradi au wasukumwe. Mkuu wa wilaya hawezi kufanya kila kitu peke yake, hawa walipaswa waende vijijini wawaelimishe wananchi wachimbe visima lakini hakuna anayefanya hivyo,” amesema Mwenegoha
Amesema kampeni ya kitaifa ya utunzaji mazingira imewasaidia wananchi wengi kutambua umuhimu wa kuwa na vyoo bora na vya kudumu na sasa wameepukana na tabia ya kujisaidia vichakani.
“Mabadiliko ni makubwa japo sio wote wenye vyoo, lakini huwezi kulinganisha na miaka ya nyuma, wapo walioelewa umuhimu wa kujisaidia chooni, lakini bado wengine wanajisaidia kwenye mifuko na kutupa barabara, tunaendelea kuwaelimisha,”amesema Mwenegoha.
Baadhi ya wananchi wa Kata ya Lyambamgongo wamesema licha ya elimu ya kujenga vyoo bora, bado mila ya kuchangia choo baba na mke wa mwana ni tatizo na pia inachangia watu kuendelea kujisaidia vichakani.
Mkazi wa Lyambamgongo, Margareth Lazaro amesema hujisaidia vichakani licha ya kuwa na choo nyumbani, kwa sababu hkinatumiwa na mkwewe.

No comments: