Friday, June 10, 2016

BARABARA YA DODOMA - MAYAMAYA KUKAMILIKA OKTOBA MWAKA HUU

Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi), Eng. Joseph Nyamhanga (Mwenye Suti), akisoma taarifa ya Ujenzi wa Barabara ya Mayamaya-Mela- Bonga (KM 188.15) wakati alipokagua ujenzi wa barabara hiyo Mkoani Dodoma. Kulia ni Meneja wa Wakala wa barabara Nchini (TANROADS) Mkoa wa Dodoma Eng. Leonard Chimagu.
Mhandisi Mkazi wa Ujenzi Barabara ya Mayamaya-Mela- Bonga (KM 188.15) Eng. Kini Kuyonza akitoa maelezo juu ya Ujenzi wa Moja la daraja lililopo katika barabara hiyo kwa Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi) Wa pili, Eng. Joseph Nyamhanga wakati wa ukaguzi wa barabara hiyo Mkoani Dodoma.

Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi), Eng.Joseph Nyamhanga (Wa Kwanza), akikagua moja ya daraja lililopo katika Barabara ya Mayamaya-Mela- Bonga (KM 188.15) ambapo Ujenzi wake umekamilika.
Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi), Eng.Joseph Nyamhanga (Wa pili kushoto) akipata maelezo juu ya Ujenzi wa Barabara ya Dodoma –Mayamaya (KM 43.65) Kutoka kwa Meneja wa Wakala wa Barabara Nchini (TANROADS) Mkoa wa Dodoma Eng. Leonard Chimagu( Wa tatu kushoto), wakati wa ukaguzi wa barabara hiyo Mkoani Dodoma.
Muonekano wa Sehemu ya barabara ya Mayamaya-Mela- Bonga yenye urefu wa (KM 188.15) ambapo ujenzi wake kwa kiwango cha lami unaendelea.


Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi) Eng. Joseph Nyamhanga amemuagiza Mkandarasi anayejenga Barabara ya Dodoma –Mayamaya yenye urefu wa KM 43.65 kumalizia kipande cha barabara ya kutoka Dodoma hadi Msalato yenye urefu wa KM 8 ifikapo Oktoba mwaka huu.

Eng. Nyamhanga ametoa agizo hilo Mkoani Dodoma alipokuwa akikagua ujenzi wa barabara ya Dodoma –Mayamaya (KM 43.65), Mayamaya –Mela –Mela –Bonga (KM 188.15) ambapo ujenzi wake kwa kiwango cha lami unaendelea.

“Hakikisheni mnakamilisha ujenzi wa kipande hiki cha KM 8 kutoka Dodoma hadi Msalato mapema kabla ya Oktoba mwaka huu”. amesema Eng. Nyamhanga.

Aidha, Eng. Nyamhanga amewataka Makandarasi wote wanaotekelea Miradi ya Ujenzi wa Barabara nchini kuongeza kasi ya ujenzi ili kuweza kukamilisha ujenzi wa barabara hizo kwa wakati ili zianze kutumika na kuleta maendeleo kwa wananchi.

Amesema kuwa barabara hizi ni Kiungo muhimu cha Miundombinu ya Barabara Tanzania kwani inaunganisha mikoa maarufu ya Kilimo ya Nyanda za juu kusini, Nyanda ya kati na Nyanda za kaskazini za mikoa ya Manyara na Arusha na pia ni kiungo kikuu kwenda nchi za SADC kupitia Dodoma.

Eng. Nyamhanga ameongeza kuwa Serikali kupitia Wakala wa Barabara Nchini (TANROADS) itaendelea kusimamia Ujenzi wa barabara hizo ili kuhakikisha zinajengwa kwa ubora unaotakiwaa kulingana na thamani ya fedha ili ziweze kudumu kwa muda mrefu.

“Sisi kwa upande wa Serikali kupitia wakala wetu TANROADS tutahakikisha barabara hizi zinajengwa kwa ubora unaotakiwa ili zidumu kwa muda mrefu”. amesisitiza Eng.Nyamhanga.

Aidha, Eng. Nyamhanga amewaomba wakazi walio karibu na Miradi hiyo ya ujenzi wa Barabara hizo kushirikina na Makandarasi kwa kulinda vifaa vinavyotumika kwa ajili ya ujenzi kwani barabara hizo zinajengwa kwa faida na matumizi ya wananchi wote.

“Serikali inajenga barabara hizi kwa ajili ya wananchi wote hivyo ni vema mkashirikiana na Makandarasi wetu kwa kutunza vifaa vya ujenzi”.amesisitiza Eng. Nyamhanga.

Naye Mkandarasi wa kampuni ya Sinohydro Coropration anayejenga sehemu ya barabara ya Dodoma-Mayamaya yenye urefu wa (KM 43.65) Eng. Zeng Yun amemuhakikishia Katibu mkuu huyo kuwa ujenzi wa Barabara hiyo utakamilika kwa wakati uliopangwa.

Barabara ya Dodoma –Mayamaya, Mayamaya –Mela-Bonga yenye urefu wa (KM 188.15) ni sehemu ya Barabara ya Kuu ya Kaskazini (The great North Road) kutoka Iringa kwenda Arusha kupitia Mikoa ya Dodoma na Manyara.

No comments: