Saturday, June 11, 2016

BUNGE LAAGIZA MBUMBE "SUGU" ACHUNGUZWE

Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi 'Sugu'
BUNGE limeielekeza Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge, kufanya uchunguzi kuhusu kitendo cha kukidhalilisha chombo hicho na Kiti cha Spika, kinachodaiwa kufanywa na Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi ‘Sugu’ kwa kuonesha kidole cha kati cha mkono wake, kuashiria matusi.

Mbilinyi alidaiwa kufanya hivyo Juni 6, mwaka huu, wakati alipokuwa akitoka kwenye ukumbi wa Bunge, baada ya kuwasilisha maoni ya Kambi ya Upinzani ndani ya chombo hicho kuhusu muswada wa kuzuia matumizi ya dawa za kuongeza nguvu kwa wanamichezo.

Akitoa maelekezo hayo bungeni mjini hapa jana, Naibu Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson alisema jambo lililoombewa mwongozo linahusu maadili ya Bunge. Alisema, mwongozo huo unatokana na kitendo cha Mbilinyi kuonesha kitendo ambacho kina tafsiri ya matusi.

“Endapo itathibitika kuwa kitendo hicho kimetendeka, itakuwa ni kinyume cha masharti ya kanuni ya 74 ya Kanuni za Kudumu za Bunge. Kwa mujibu wa nyongeza ya 8 kifungu cha 4 fasiri ya 1b ya kanuni za kudumu za Bunge, Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge, pamoja na majukumu mengine, imepewa jukumu la kushughulikia mambo yanayohusu maadili ya wabunge,” alisema.

Alisema kutokana na masharti ya kanuni aliyoitaja, anaelekeza kamati hiyo ifanye uchunguzi na kuchukua hatua stahiki. Maelekezo hayo ya Spika yalitokana na mwongozo ulioombwa Juni 6, mwaka huu na Mbunge wa Viti Maalumu, Jacqueline Msongozi (CCM) aliyeeleza kuwa Mbilinyi alikidhalilisha Kiti cha Spika na Bunge kwa kuonesha kidole kinachoashiria matusi.

Mbali na Msongozi, Mbunge wa Mbinga Mjini (CCM), Sixtus Mapunda, naye alisimama siku hiyo ili kuomba mwongozo na alipopewa nafasi alisema alichotaka kueleza kilishaelezwa na Msongozi. Awali wakati akijibu mwongozo wa Msongozi, Naibu Spika alisema, “Kwa kuwa sikumuona Mheshimiwa Mbilinyi akifanya kitendo hicho, nitafuatilia suala hilo na kulitolea mwongozo.”

HABARI LEO

No comments: