Wednesday, June 8, 2016

Mradi mkubwa wa umeme, Iringa – Shinyanga kukamilika Septemba 2016, Watumia zaidi ya Dola za Marekani milioni 224

Sehemu ya kituo cha kupoza umeme cha Dodoma 220/33kV kilichopo katika eneo la Zuzu mkoani Dodoma.
Meneja Mradi anayesimamia ujenzi wa vituo vya kupoza umeme wa mradi wa usafirishaji umeme kutoka Iringa hadi Shinyanga kV 400, Mhandisi James Mtei (kushoto) akiwaeleza waandishi wa habari juu ya maendeleo ya ukamilishwaji wa kituo cha kupoza umeme cha Dodoma kilichopo katika eneo la Zuzu mkoani Dodoma.

Na Greyson Mwase, Dodoma

Imeelezwa kuwa mradi wa usafirishaji umeme kutoka Iringa hadi Shinyanga katika msongo wa kilovolti 400 unaofadhiliwa na washirika mbalimbali wa maendeleo unatarajiwa kukamilika ifikapo Septemba mwaka huu.

Hayo yalielezwa na Meneja Mradi anayesimamia ujenzi wa vituo vya kupoza umeme wa mradi huo, Mhandisi James Mtei katika ziara ya waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali vya habari nchini inayoendelea mkoani Dodoma lengo likiwa ni kujionea utekelezaji wa miradi ya umeme inayofadhiliwa na Benki ya Dunia (WB).

Mhandisi Mtei alisema kuwa mradi huo uliogharimu zaidi ya Dola za Marekani milioni 224 sawa na takriban Shilingi bilioni 387.5 umejumuisha ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme umbali wa kilomita 670 na vituo vya kupoza umeme katika mikoa ya Iringa, Dodoma, Singida na Shinyanga.

Alisema kwa upande wa sehemu ya kutoka Iringa hadi Dodoma kilomita 225 imeshakamilika kwa asilimia 99 na kinachosubiriwa kwa sasa ni mkandarasi kulifahamisha rasmi Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kuwa kazi imemalizika ili kituo kianze kufanyiwa majaribio na kukabidhiwa kwa serikali mwishoni mwa mwezi Juni mwaka huu.

Alifafanua kuwa sehemu nyingine za kutoka Dodoma hadi Singida na Singida hadi Shinyanga utekelezaji wake umefikia asilimia 89 ambapo mradi wote kwa ujumla unatarajiwa kukabidhiwa kwa serikali mapema Septemba mwaka huu.

Alisisitiza kuwa mara baada ya mradi wote kukamilika kama ilivyopangwa hali ya umeme katika mikoa ya Iringa, Dodoma, Singida, Shinyanga na Kanda ya Ziwa kwa ujumla itaimarika sana.

Wakati huo huo Mhandisi Nishati Mkuu kutoka Wizara ya Nishati na Madini, Mhandisi Salum Inegeja aliongeza kuwa mradi huu ni sehemu ya mradi mkubwa wa kuunganisha gridi za Zambia, Tanzania na Kenya (ZTK).

Alisema kuwa katika mradi huo wa kikanda, Tanzania imeshatekeleza sehemu kubwa ya mradi huo kutoka Iringa hadi Singida na sehemu iliyobaki ya kutoka Singida hadi Namanga kupitia Arusha fedha zake kutoka Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) na Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Japan (JICA) zilishapatikana ambapo kwa sasa taratibu za tathmini ya fidia kwa watu watakaopisha mradi huo zinaendelea.

Aliendelea kusema katika sehemu ya kutoka Mbeya hadi Tunduma upembuzi yakinifu unaendelea ambapo unatarajiwa kukamilika ifikapo mwezi Novemba mwaka huu.

Mhandisi Inegeja alisema kukamilika kwa mradi mbali na kuimarisha upatikanaji wa umeme nchini, kutaiwezesha Tanzania kushiriki kikamilifu katika biashara ya umeme kupitia mifumo ya gridi za nchi jirani katika ukanda wa mashariki (Eastern African Power Pool -EAPP) na zilizopo katika ukanda wa kusini (Southern African Power Pool -SAPP).

Alitaja nchi zilizopo katika ukanda wa mashariki ni pamoja na Kenya, Uganda, Sudan, Ethiopia, Libya, Misri na Djibouti na zilizopo katika ukanda wa kusini ni pamoja na Afrika ya Kusini, Namibia, Botswana, Zimbabwe, Zambia, Angola na Swaziland.

Mhandisi Nishati Mkuu kutoka Wizara ya Nishati na Madini, Mhandisi Salum Inegeja (kushoto) akifafanua jambo kwa waandishi wa habari waliofanya ziara katika kituo cha kupoza umeme cha Dodoma, ambacho ni sehemu ya mradi wa usafirishaji umeme kutoka Iringa hadi Shinyanga katika msongo wa kilovolti 400 katika eneo la Zuzu mkoani Dodoma.
Meneja Mradi katika mradi wa usafirishaji umeme kutoka Iringa hadi Shinyanga katika msongo wa kilovolti 400 anayeshughulikia ujenzi wa njia ya usafirishaji umeme, Mhandisi Oscar Kanyama akielezea wigo wa mradi huo mbele ya waandishi wa habari waliofanya ziara katika kituo cha kupoza umeme cha Dodoma ambacho ni sehemu ya mradi huo katika eneo la Zuzu mkoani Dodoma.
Mmoja wa wanufaika wa fidia kwa ajili ya kupisha Mradi wa usafirishaji umeme kutoka Iringa hadi Shinyanga katika msongo wa kilovolti 400, Yona Rubano (kulia) akiwaeleza waandishi wa habari jinsi alivyotumia fedha hizo kujenga nyumba ya kisasa.

No comments: