Saturday, October 19, 2024

MIZENGO PINDA AWASILI BOTSWANA KUONGOZA MISHENI YA UANGALIZI YA SADC KATIKA KTIKA UCHAGUZI MKUU WA BOTSWANA

Waziri Mkuu Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Mizengo Kayanza Peter Pinda akiwa na Balozi wa Tanzania nchini Botswana mwenye makazi yake Afrika Kusini Mhe. James Bwana alipompokea katika Uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Sir Seretse Khama wa Gaborone, Botswana alipowasili kuongoza Misheni ya SADC ya uangalizi wa Uchaguzi Mkuu wa Botswana uliopangwa kufanyika tarehe 30 Oktoba 2024
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Afrika Mashariki Balozi Said Shaib Mussa akizungumza na Waziri Mkuu Mstaafu Mhe. Mizengo Pinda kwenye chumba cha mapumziko katika Uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Sir Seretse Khama wa Gaborone, Botswana alipowasili kuongoza Misheni ya SADC ya uangalizi wa Uchaguzi Mkuu wa Botswana uliopangwa kufanyika tarehe 30 Oktoba 2024

Waziri Mkuu Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Mizengo Kayanza Peter Pinda amewasili jijini Gaborone, Botswana tarehe 19 Oktoba, 2024.

Mhe. Mizengo Pinda ataongoza Misheni ya Uangalizi ya Uchaguzi ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC- SEOM) katika Uchaguzi Mkuu wa Jamhuri ya Botswana uliopangwa kufanyika tarehe 30 Oktoba, 2024.

Katika Uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Sir Seretse Khama jijini Gaborone Mhe. Pinda amelakiwa na Balozi wa Tanzania nchini Botswana mwenye makazi yake Afrika Kusini Mhe. James Bwana.

Mhe. Pinda ataongoza SEOM kufuatia kuteuliwa kuongoza Misheni hiyo na Mwenyekiti wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya SADC (Troika) na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Mhe. Pinda atazindua rasmi Misheni ya SEOM inayoundwa na wajumbe kutoka Nchi Wanachama wa SADC tarehe 22 Oktoba, 2024.

Mhe. Pinda kwa kushirikiana na Wajumbe wengine wa Troika (Zambia na Malawi) atakutana na wadau mbalimbali wa uchaguzi ikiwemo Tume ya Uchaguzi ya Botswana (IEC), Mabalozi wa Nchi za SADC waliopo Botswana, Vyama vya siasa, Asasi za Kiraia, Taasisi za dini na Vyombo vya Habari kwa ajili ya kuelezea kazi ambayo SEOM itafanya katika kipindi hiki kuelekea uchaguzi mkuu hadi kukamilika kwake.

No comments: