ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, June 29, 2016

TUNDU LISSU MAHAKAMANI

Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (katikati) na Mhariri wa Mawio, Simon Mkina (wa poli kutoka kushoto mwenye miwani) na mchapishaji wao Ismail Mahboob (wa tatu kutoka kushoto mbele).

MBUNGE wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (Chadema) amepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam akikabiliwa na mashtaka ya kuchapisha taarifa za uchochezi.

Lissu alisomewa mashtaka hayo jana na kuunganishwa na wenzake, Mwandishi wa gazeti la Mawio, Jabir Idrissa, Mhariri wa gazeti hilo, Simon Mkina na mchapishaji wa Kampuni ya Jamana, Ismail Mehboob ambao walisomewa mashtaka yao awali.

Baada ya Lissu kusomewa mashtaka hayo, Hakimu Mkazi Mkuu ,Thomas Simba, alifuta mashtaka mawili ya uchochezi kati ya matano yanayowakabili washtakiwa hao. Hakimu Simba alifuta mashtaka hayo baada ya upande wa Jamhuri kuyaondoa katika hati ya mashtaka kwa kuwa hayana kibali cha Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP).

Awali, Wakili wa Serikali, Paul Kadushi alimsomea Lissu mashtaka yake kwa kudai kuwa kati Januari 12 hadi 14, 2016 katika Jiji la Dar es Salaam, Lissu aliandika taarifa za uchochezi yenye kichwa cha habari kisemacho’ Machafuko yaja Zanzibar’.

Katika shtaka la pili linalowakabili washtakiwa wote, inadaiwa Januari 14, 2016 katika Jiji la Dar es Salaam, kwa nia ya kusababisha chuki kati ya wananchi wa Zanzibar na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, walichapisha gazeti la Mawio likiwa na habari hiyo ya uchochezi.

Aidha, inadaiwa Januari 14, 2016, Dar es Salaam, Lissu na wenzake bila ya kuwa na mamlaka yoyote, walisababisha hofu kwa wananchi wa Zanzibar kwa kuwaambia wasikubali kurudiwa kwa uchaguzi mkuu mwaka huu, kwa sababu utasababisha machafuko.

Baada ya kusomewa mashtaka, Lissu alikana kutenda kosa hilo na kuachiwa kwa dhamana. Kesi ilipotajwa kwa mara ya kwanza, Wakili wa utetezi, Peter Kibatala aliwasilisha pingamizi la awali akiiomba Mahakama iyafute mashtaka yote kwa kuwa yana mapungufu kisheria, lakini upande wa Jamhuri uliomba upewe muda kwa ajili ya kutolea ufafanuzi.

Jana Hakimu Simba alifuta mashtaka mawili baada ya wakili Kadushi, kudai kuwa wameondoa shtaka la kwanza (kula njama) na la tano (kuchapisha taarifa za uchochezi), kwa kuwa hayakuwa na kibali cha DPP.

Hata hivyo, Wakili Kibatala aliendelea kuiomba mahakama ifute mashtaka yote, yaliyobaki kwa sababu hati ya mashtaka imekosewa “hakuna sehemu iliyooneshwa kwamba makosa hayo yametendeka wapi”.

Aidha, katika Sheria ya Magazeti kuna baadhi ya vitu vimeruhusiwa na vingine havijaruhusiwa, lakini katika hati ya mashtaka hayajaorodheshwa hayo.

Alitoa mfano “katika sheria hiyo, hakuna sehemu inayokataza kuelimisha, kukosoa au kurebisha jambo endapo serikali ikikosea”.

Wakili Kibatala alidai kutokana na hati hiyo kutoeleza mambo hayo muhimu, Mahakama iyatupilie mbali mashtaka yaliyobakia kwa kuwa sheria ya magazeti haipo kwenye muungano wa Tanzania Bara na Visiwani.

Baada ya mabishano hayo, Hakimu Simba aliahirisha kesi hiyo hadi Julai 11, mwaka huu atakapotoa uamuzi.

(HABARI NA HABARI LEO)

No comments: