Wednesday, June 8, 2016

WAKALA WA VIPIMO KUTOA ELIMU KANDA YA ZIWA

Wazri wa viwanda na uwekezaji Mhe. Charles Mwiijage wakati wa mkutano wa ulioandaliwa na wakala wa vipimo hizi karibuni jijini Mwanza,
Mkulima akiangalia kwa makini jinsi mzani wa kupimia Pamba unavyofanya kazi.
Hapa ni Jinsi, Wakulima wasio waaminifu ambavy wanaweza kuchafua pamba kwakuweka mawe, hali inayo changia kushika kwa bei za zao hilo katika soko la Dunia.


ZAO LA PAMBA NA CHANGAMOTO YA MAJI KWENYE ZAO HILO

Wakala wa Vipimo nchini kuanza kutoa elimu mikoa ilimayo pamba


Na. Atley Kuni- RS Mwanza.

Kushuka kwa uzalishaji wa zao la pamba nchini kunatokana na baadhi ya wakulima wasiowaaminifu kuweka maji na mawe kwenye zao hilo na kuathiri mbegu ambazo badaye huzitumia mbegu hizo kwa ajili ya kupanda.

Kaimu meneja wa sehemu ya elimu na mawasiliano wakala wa vipimo makao makuu Iren John amesema hayo jijini Mwanza wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu namna ambavyo wamejipanga kuhakikisha pamba inayozalishwa inakuwa yenye ubora.

Iren John, amesema, kati ya watu 10 unaweza kupata watu 4 hadi 5 wanao weka maji kwenye pamba hali ambayo imechangia pamba ya Tanzania kuuzwa katika daraja la nne katika soko la Dunia.

Kufuatia hali hiyo, wakala wa Vipimo Nchini, imeamua, kutoa elimu kwa wakulima wa zao la Pamba kwa mikoa ya kanda ya ziwa juu ya matumizi bora ya mizani ya kupimia pamba kwa lengo la kuhakikisha mkulima/wakulima wanatambua namna bora yakutumia mizani hiyo lakini pia kuhakikisha mkulima hachafui pamba yake kwa kuweka maji kwa lengo lakujiongezea kipato.

Jumla ya vijiji vipatavyo 105 vya mkoa wa Mwanza na vijiji 44 vya Mkoa wa Geita vimeainishwa kwaajili yakupatiwa elimu ambapo katika mkoa wa Mwanza, wilaya zitakazo husishwa ni Magu, Kwimba, Sengerema na Misungwi.

Iren amesema, kutokana wakulima kutokuwa na elimu ya kutosha juu ya matumizi sahihi ya mizani hiyo, ilipelekea mkulima na mnunuzi kukomoana kwa kila upande na matokeo yake ni kushuka kwa bei ya Pamba katika soko la dunia lakini pia kupoteza uaminifu kwa wanunuzi wa pamba wa kimataifa kwa Pamba itokayo Tanzania.

“Hali ya kukomoana baina ya mnunuzi na mkulima ndiyo imekuwa chanzo cha Pamba yetu kupoteza thamani kwenye soko la Dunia” alisema Iren, na kuongeza, mkulima akiona muuzaji amechezea mizani, yeye anachofanya nikuweka maji au mawe kwenye pamba, mwisho wa siku, tunakuwa na pamba chafu lakini pia inasababisha mbegu za pamba zilizo nyunyuziwa maji kutoota”.

Iren amesema, endapo wakulima na wanunuzi wa pamba wakipatiwa elimu ya kutosha juu ya vipimo sahihi vya mizani, na kutambua namna ya kuujua mzani ulio chezewa, ni wazi kwamba, watakuwa waaminifu kwa kutoweka vitu visivyo stahiki kwenye pamba yao, lakini pia itasaidi pamba yetu kuaminika kwenye masoko ya kimataifa.

“Sasa hivi nchi inaongea juu ya Viwanda, lakini hatuwezi kuwa na viwanda bila kuwa na malighafi, na malighafi lazima tufahamu kwamba, nyingi zinatokana na mazao ya mashambani, hivyo basi nilazima kama wakala wa vipimo tuhakikishe wakulima wanapata elimu ya matumizi sahihi ya mzani ili anapo pima pamba yake ahakikishe mizani husika imehakikiwa na wakala wa vipimo Tanzania ” alisisitiza Iren.

Amesema kuanzia msimu wa mwaka huu, adhabu yakuchezea mizani iliyokuwa inatozwa imeongezwa kwani mtu atakaye jaribu kuchezea mzani, atakwenda jela miaka 3, pamoja na faini ambayo italipwa na mtuhumiwa mara baada yakumaliza kifungo chake jela.

Kwa upande wao wakulima wa wilayani Magu, wameupokea mpango huo wa elimu kwa moyo mkunjufu na kusema umekuja wakati muafaka, kwani, muda mrefu wamekuwa hawajui hatma ya zao hilo lililo jizolea umaarufu ndani na nje ya mipaka ya Tanzania katika miaka ya nyuma, kufuatia hatua hiyo wakulima wameahidi kuendelea kulima zao hilo.

“Huku kwetu Mwanza, tuliamini Pamba ni dhahabu nyeupe, kwa kuwa maendeleo yote unayo yaona yalichangiwa na zao la pamba, watoto wetu walisoma kwa zao la pamba”, anasema mkaazi wa kijiji cha Mahaha, Mabula Nhumba.

Wakala wa vipimo nchini ilianzishwa kwa mujibu wa sheria ya vipimo sura namba 340, ndiyo yenye jukumu la kusimamia usahihi wa vipimo vinavyotumika au vinavyotarajiwa kutumika kisheria kwenye maeneo ya kibiashara hapa nchini sambamba na kumlinda muuzaji wa pamba kwa kutoa usahihi wa vipimo.

MWISHO.


No comments: