Wednesday, June 15, 2016

WAZIRI MKUU MAJALIWA - BENKI PITIENI UPYA RIBA ZENU

 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akifungua Mkutano wa Wadau wa Benki za Wananchi kwenye Ukumbi wa Hazina mjini Dodoma Juni 15, 2016.
 Baadhi ya Washiriki wa Mkutano wa  Wadau wa Benki za Wananchi wakimsikiliza Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa  wakati alipofungua mkutano wao kwenye ukumbi wa Hazina mjini Dodoma Juni 15, 2016.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa  akiwa katika picha ya pamoja  na washiriki wa Mkatano wa Wadau wa Benki za Wananchi kwenye ukumbi wa Hazina mjini Dodoma juni 15, 2016. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amezitaka benki nchini zipitie upya riba zake ili Watanzania waweze kukopa na kurejesha kwa urahisi.

Amesema riba kubwa zinazotozwa na baadhi ya benki, huduma zisizokidhi mahitaji na uelewa mdogo wa masuala ya kifedha ni miongoni mwa changamoto wanazokabiliana nazo wananchi wanapotaka huduma za kifedha.

Waziri Mkuu ametoa agizo hilo leo (Jumatano, Juni 15, 2016) wakati wa ufunguzi wa mkutano wa wadau wa Jumuiya ya Benki za Wananchi (COBAT) mjini Dodoma.

Mkutano huo ulijumuisha wajumbe kutoka mikoa 10 ya Kigoma, Lindi, Simiyu, Manyara, Katavi, Mbeya, Mwanza, Morogoro, Singida na Dodoma kati ya mikoa 18 ya Tanzania Bara ambayo bado haina Benki za Wananchi ila ipo katika hatua za kuanzisha.

Amesema changamoto nyingine ni kutokuwepo kwa taarifa mbalimbali za sheria na taratibu ambazo zinakwamisha ufanisi wa kiutendaji kwa baadhi ya taasisi hasa zile zinazolenga kuwahudumia watu wa kipato cha chini.

“Tunahitaji kutafuta njia bora ya kutatua changamoto hizi, na Benki za Wananchi ni kiungo muhimu katika kushughulikia changamoto zinazokabili utoaji wa huduma za kifedha,” amesema.

Waziri Mkuu amesema ni muhimu kuanzisha Benki za Wananchi katika kila Mkoa ili kuweza kusambaza huduma hizo karibu zaidi na walengwa, hali ambayo itasaidia kupunguza umasikini kupitia ukuaji wa shughuli za kiuchumi.

Amesema Serikali itaangalia uwezekano wa kuiwezesha mikoa ambayo itaonyesha ari zaidi ya kuanzisha benki zao na akatoa wito waandae mikakati ya kuhamasisha wananchi ili wakusanye mitaji ya kutosha.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa COBAT, Bibi Elizabeth Makwabe amesema Jumuiya yao ilianzishwa mwaka 2006 ikiwa na wanachama saba na sasa hivi wamefikia 10 huku wananchi wanaowahudumiwa na benki hizo ni zaidi ya milioni mbili.

Amesema Jumuiya za Benki ya Wananchi inakabiliwa na changamoto mbalimbali zikiwemo mfumo hafifu wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) pamoja na ufinyu wa mitaji.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
S. L. P. 980,    
DODOMA.

JUMATANO, JUNI 15, 2016.

No comments: