Mbeya. Mkazi wa Jiji la Dar es Salaam, Gibson Mwasembo ameibuka kwenye kikao cha Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Amos Makalla akitaka kulipwa fidia kwa madai ya kugongwa na gari la mkuu wa mkoa huo mwaka 1980 na kupata ulemavu.
Jana, Makalla alihamishia ofisi yake katika Ukumbi wa Benjamini Mkapa kwa lengo la kusikiliza kero na matatizo ya wananchi.
Hata hivyo, Makalla aliwataka watendaji wa ofisi yake kuwasiliana na mzee huyo ili hatua zaidi za suala lake lifanyiwe kazi.
Akizungumza katika kikao hicho, Mwasembo alidai kuwa aligongwa na gari aina ya Landrover na dereva alimlipa fidia ya Sh3,000 kipindi hicho.
“Dereva alilipa fidia, mimi nimebaki mlemavu hadi sasa, nimekuja Mbeya mara nyingi nikitokea Dar es Salaam, nikifika hapa nalala stendi Kuu,’’alisema Mwasembo. Alisema wakati anagongwa na gari hilo alikuwa na umri wa miaka 22 na kuwa hali hiyo ilimsababishia ashindwe kufanya kazi yoyote na kuishi kwa utegemezi. Mwasembo ambaye alikuwa na nyaraka mbalimbali mkononi mwake alisema kwa sasa anachohitaji ni kupata fidia ya nyumba.
“Nimekuwa sina uwezo wa kufanya kazi yoyote tangu nigongwe na gari na kuwa mlemavu ningekuwa mzima ningeweza kumudu kufanya kazi na kujenga nyumba,” alisema. Mwanasheria wa Serikali, Wakili Basil Namkambe alisema suala la mzee huyo linafahamika na limefika kwenye ofisi yake.
“Kesi hiyo iliamriwa Aprili 20,1982 mshtakiwa alitiwa hatiani kwa kutakiwa kulipa faini ya Sh3,000 au kwenda jela miezi tisa,” alisema Wakili Namkambe.
No comments:
Post a Comment