Akizungumza na waandishi wa habari jana, Makamu mwenyekiti wa Bavicha, Patrick ole Sosopi alisema Bavicha imeamua kuzuia mkutano huo kutokana na tamko la Jeshi la Polisi kuzuia mikutano yote ya kisiasa.
“Tunaungana na tamko la Jeshi la Polisi, tunaungana na tamko la Rais John Magufuli pia hakuna mkutano wowote wa siasa unaotakiwa kufanyika, iweje CCM waandae mkutano huo, sisi vijana wa Chadema tutakuwepo pale Dodoma kuzuia mkutano huo,” alisema.
Ingawa Patrick hakufafanua ni njia zipi ambazo zitatumika kuzuia mkutano huo, lakini alisema watatumia njia halali kuhakikisha mkutano huo hautafanyika kama ambavyo mikutano ya vyama vingine imezuiliwa.
Jeshi la Polisi lilizuia kufanyika mikutano yote ya kisiasa, jambo ambalo lilipingwa na Chadema mahakamani kwa kufungua kesi Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza.
Katibu Mkuu wa Bavicha, Julias Mwita alisema vijana wa Chadema pia wanapinga tamko la Rais Magufuli la kuomba wataalamu wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) kutoka Rwanda, ili watoe mafunzo kwa watendaji wa Wakala wa Serikali Mtandao (eGA) kwa lengo la kuhakikisha kila fedha inayokusanywa inaonekana katika mtandao.
Alisema Tanzania ina vijana wengi wasomi ambao wana utaalamu katika mambo ya Tehama ambao hawana ajira, Rais anaweza kuwatumia kuliko kuchukua wataalamu kutoka Rwanda.
HABARI LEO
1 comment:
Kwa uwezo na mamlaka yapi ya kisheria waliyonayo Bavicha wazuie mkutano wa CCM? Je,nili CCM ilizuia mikutano ya Chadema? Huu ndio mwanzo wa kuleta uvunjifu wa amani nchini.Kwa strategies za namna hii Chadema bado wanasafari ndefu..
Post a Comment