Advertisements

Tuesday, July 5, 2016

Maoni ya Balozi wa Marekani nchini Tanzania Mark B. Childress Kuhusu maadhimisho ya siku ya Uhuru wa Marekani


Ubalozi wa Marekani
Dar es Salaam
TANZANIA
KWA UCHAPISHAJI TAREHE 4 JULAI, 2016
Wakati Marekani ikiadhimisha miaka 240 ya Uhuru wetu, ninakumbushwa kwamba nchi yetu, kama ilivyo kwa Tanzania, imedhamiria kuimarisha amani, utulivu, na ukuaji wa uchumi kwa  raia wake wote.  Tarehe 4 Julai, tunasherehekea Katiba yetu tunayoienzi, ambayo ni nyaraka inayotupa na kutuhakikishia haki binafsi kama vile uhuru wa kujieleza, uhuru wa kukusanyika na uhuru wa vyombo vya habari.  Tuna fahari kwa demokrasia yetu ya uwakilishi ambayo kwa karne kadhaa imewezesha kuwekwa kwa mifumo ya kuhakikisha uwiano wa mamlaka baina ya mihimili ya utawala (checks and balances) katika kulinda amani na ustawi wa raia wetu wote.
Hivi sasa kampeni kali za uchaguzi wa Rais ajaye wa Marekani zinaendelea.  Rais ajaye wa Marekani atakuwa na nguvu kubwa katika kuweka sera, lakini atakuwa akifanya kazi katika mfumo wenye nyenzo za kuwianisha mamlaka kama ilivyoelezwa hapo juu.  Nyenzo hizo ni pamoja na mahakama imara, mhimili wa bunge lenye sehemu mbili na vyombo huru vya habari vinavyowapa Wamarekani, taarifa, maoni na mawazo mbalimbali.  Kwa hali hiyo, ninaguswa pale sauti za Kitanzania
zinapopazwa na kutoa malalamiko kuhusu kuminywa kwa demokrasia, iwe ni kwa kupiga marufuku mikutano ya kisiasa au kuzuia matangazo ya televisheni ya vikao vya Bunge.  Ninaamini kwamba mapambano dhidi ya rushwa – ambayo kwa hakika ni muhimu sana kwa nchi zetu mbili – ni lazima yafanyike bila kukwaza majadiliano, hali ya kutofautiana maoni au kuwepo kwa uhuru wa kujieleza.  Ukweli ni kwamba mkinzano wa kibunifu kati ya mawazo tofauti yanayoshindana ndiyo huifanya demokrasia kuimarika, kustawi na kuwa hasa ya uwakilishi wa watu.
Kama ilivyokuwa kwa watangulizi wangu, ninaunga mkono azma ya Tanzania ya kudumisha na kuimarisha amani na ustawi.  Kwa hakika watu wa Marekani tunajivunia urafiki wetu wa muda mrefu na watu wa Tanzania.  Aidha, tuna fahari kuwa mbia mkubwa zaidi wa maendeleo nchini Tanzania na kuendelea na uwekezaji wetu katika maeneo mengi, ikiwa ni pamoja na afya, elimu, kilimo na ukuaji wa uchumi.  Malengo yetu ya pamoja na urafiki wetu unadhihirishwa na kufanana kwa mijadala ya umma katika nchi zetu kuhusu mifumo ya kuwianisha mamlaka miongoni mwa mihimili ya serikali na umuhimu wa kuwa na vyombo huru vya habari vinavyoweza kuripoti kwa usahihi utendaji wa serikali kwa raia.  Majadiliano ya wazi kuhusu uwezo wa serikali kuwasilisha kwa uaminifu matakwa ya raia wake na kulinda amani na ustawi ndiyo yaliyoiwezesha nchi yangu kujitangazia uhuru wake miaka 240 iliyopita.  Wamarekani walijitahidi sana wakati huo, na tunaendelea kujitahidi hivi leo kupitia majadiliano haya makali katika jamii na siasa.  Ninaamini kwamba Marekani, na nchi zote zenye demokrasia yenye afya zinaimarika zaidi na zaidi kutokana na majadiliano haya.

No comments: