Advertisements

Saturday, July 9, 2016

TAASISI 680 KUFUTWA, ZIPO ZA KIDINI NA ZA KISIASA

WAKALA wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA), inakusudia kuzifutia usajili bodi za udhamini 680 za taasisi mbalimbali; ambazo zimekiuka masharti, ikiwa ni pamoja na kutokuwa hai.

Aidha, Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Harrison Mwakyembe ameuruhusu wakala huo kuanza kusajili bodi za udhamini; huku akiutaka kuhakikisha bodi zitakazosajiliwa zinaendeshwa kwa mujibu wa sheria na taratibu.

Akizungumza jana Dar es Salaam katika mkutano wa Bodi ya Wadhamini ya Rita, Dk Mwakyembe alisema, wakala huo unatakiwa kuzifuta haraka bodi hizo ili kuwepo na bodi chache ambazo ziko hai.

“Mmefanya kazi nzuri ya kuhakiki baadhi ya hizi bodi, endeleeni kuhakikisha tuna vyombo vichache ambavyo viko hai…kuna bodi kama 500 ambazo haziko hai na mnakusudia kuzifuta, zifuteni haraka,” alisema Dk Mwakyembe.

Alisema serikali imedhamiria kudhibiti mapato na ndio sababu katika mkutano wake na Bodi ya Rita alitoa agizo kwa wakala huo kusitisha usajili mpya wa wadhamini wa asasi, vyama, misikiti, makanisa na taasisi mbalimbali huku akitoa siku 90 wakala huo ukamilishe uhakiki wa bodi hizo.

Alisema baadhi ya vikundi hivyo ambavyo vingine vimekuwa vikiibuka wakati wa kampeni na uchaguzi vimekuwa vikitumika vibaya kupata misamaha ya kodi na vingine kuomba ruzuku.

Dk Mwakyembe alifafanua kuwa katika kikao chake na mamlaka zote zinazohusika na usajili wa vikundi vya kijamii, mashirika, kampuni na asasi mbalimbali ulikuwa na lengo la kuimarisha taratibu za usajili ili kudhibiti utitiri wa vikundi hivyo.

Aidha, alisema mkutano huo pia ulikuwa na lengo la kufanya maboresho kwa mamlaka hizo ili mifumo yao iweze kuwasiliana ili kulinda maslahi mapana ya Taifa.

Awali Kaimu Ofisa Mtendaji Mkuu wa Rita, Emmy Hudson alisema, tayari tangazo la kusudio la kuzifutia usajili bodi za wadhamini limeshaandaliwa na litatolewa muda wowote kuanzia sasa.

Alisema jumla ya bodi za wadhamini zilizosajiliwa ni 5,262 ambazo kati ya hizo zilizohakikiwa ni 1,544 na kwamba katika uhakiki huo walikumbana na changamoto ya malalamiko kutoka kwa bodi hizo kuwa nyingine ziko mbali.

Hudson alisema kati ya hao 5,262 ambao wako kwenye kanzi data ya wakala huo walichambua na kubaini walioko hai ni 4,287 pekee.

“Bodi za Udhamini 500 zimebainika kuwa haziko hai…zoezi la kuingiza taarifa kwenye databae (kanzidata) linaendelea lakini pia tunaomba tuongezewe muda au ikiwezekana liwe endelevu,” alisema.

Alisema kabla ya kuanza kwa uhakiki wa bodi hizo tayari walikuwa na idadi ya bodi 200 ambazo zilitakia kufutiwa usajili na zilipelekewa notisi za kufutiwa usajili wao ambapo kati ya hizo 20 tu ndizo zilizojibu na kuomba kutofutiwa usajili wao.

Hata hivyo, alisema wakala huo umekuwa ukikabiliana na changamoto mbalimbali ikiwemo za taasisi kumiliki mali bila kuwa na idhini ya bodi ya wadhamini kinyume cha sheria, muda wa kutembelea taasisi hizo kuwa mdogo, baadhi ya taasisi kubadili majina na anuani zao bila kutoa taarifa.

“Lakini pia tumebaini kuwepo kwa baadhi ya bodi ambazo hazitambui wajibu wao na pia mkanganyiko wa tafsiri ya sheria kutoka katika taasisi mbalimbali zinazoshughulika na usajili,” alisema Hudson.

Kazi kubwa zinazofanywa na bodi za udhamini ni kusimamia rasilimali fedha pamoja na uendeshwaji wa kampuni au taasisi husika.

No comments: