Advertisements

Tuesday, July 19, 2016

Wakurugenzi 6 wa NSSF Wasimamishwa Kazi Kupisha Uchunguzi

BODI ya Wadhamini ya Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) imeagiza kusimamishwa kwa wakurugenzi sita, mameneja watano na mhandisi mmoja wa shirika hilo kupisha uchunguzi, kubaini wahusika katika tuhuma za ubadhirifu, matumizi mabaya ya ofisi na kutofuata kanuni, sheria na taratibu katika uwekezaji, usimamizi wa miradi, manunuzi ya ardhi na ajira.

Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya NSSF, Profesa Samwel Wangwe, alikiri  jana usiku kusimamishwa kwa vigogo hao 11, kupisha uchunguzi wa tuhuma zilizoelekezwa kwao.

“Ni taarifa sahihi hizo. Kulikuwa na tuhuma katika ripoti ya ukaguzi, kwa hiyo tumeamua wakae pembeni ili kupisha uchunguzi, hawajafukuzwa kazi. Taarifa hiyo ya kusimamishwa ni sawa sawa,” alisema Profesa Wangwe jana usiku.

Kwa mujibu wa taarifa kwa wafanyakazi, iliyotolewa na Ofisi ya Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, iliwataja wakurugenzi sita waliosimamishwa kuwa ni Yacob Kidula (Mkurugenzi wa Mipango, Uwekezaji na Miradi), Ludovick Mrosso (Mkurugenzi wa Fedha) na Chiku Matessa (Mkurugenzi wa Rasilimali Watu na Utawala).
Wengine ni Sadi Shemilwa (Mkurugenzi wa Udhibiti Hadhara na Majanga), Pauline Mtunda (Mkurugenzi wa Ukaguzi wa Mahesabu ya Ndani) na Crescentius Magori (Mkurugenzi wa Uendeshaji).

Aidha, taarifa hiyo iliwataja mameneja waliosimamishwa kuwa ni Amina Abdallah (Meneja Utawala), Abdallah Mseli (Meneja wa Uwekezaji), Mhandisi John Msemo (Meneja wa Miradi), Davis Kalanje (Mhasibu Mkuu), Wakili Chedrik Komba (Meneja Kiongozi – Mkoa wa Temeke) na Mhandisi John Ndazi (Meneja Mradi).

Taarifa hiyo kutoka Ofisi ya Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, ilisema kwamba uamuzi huo umefanywa na Bodi chini ya Profesa Wangwe iliyokutana Julai 15, mwaka huu kutokana na taarifa mbalimbali za wakaguzi wa hesabu na shughuli za uendeshaji wa shirika hilo la umma.

“Bodi ya Wadhamini ya Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii chini ya Uenyekiti wa Profesa Samwel Wangwe katika kikao chake cha 106 kilichofanyika tarehe 15 Julai, 2016 kimeagiza kusimamishwa kazi kwa wakurugenzi sita (6), mameneja watano (5) na mhandisi mmoja ili kupisha uchunguzi kubaini wahusika katika tuhuma za ubadhirifu, matumizi mabaya ya ofisi na kutofuata kanuni, sheria na taratibu katika uwekezaji, usimamizi wa miradi na manunuzi ya umma na ajira,” ilieleza taarifa hiyo.

Hivi karibuni, NSSF ilitajwa katika vyombo vya habari kuhusu tuhuma zikiwamo za ununuzi wa ardhi usiofuata taratibu za manunuzi ya umma, kuwapo kwa ubadhirifu na ajira za upendeleo katika shirika hilo, ukiwataja wahusika kuwa ni baadhi ya wakurugenzi wa shirika hilo.

1 comment:

Anonymous said...

"AJIRA ZA UPENDELEO"; Are you kidding me? Huo ni mchezo wa kawaida Tanzania, toka tuupate Uhuru mpaka sasa. Mfano, tazama FOREIGN Affairs ministry!