WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amesitisha
utoaji wa vibali vya uvunaji wa mbao kutoka katika mashamba nane ya miti ya
kupandwa yanayosimamiwa na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS).
Serikali kupitia Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania
(TFS) chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii inamiliki mashamba ya miti ya
kupandwa 18, na kati ya hayo uvunaji umekuwa ukifanyika katika mashamba nane
ambayo ni Sao Hill (Mufindi), Buhindi (Sengerema), Meru/Usa (Arumeru), West
Kilimanjaro (Hai), Shume (Lushoto), North Kilimanjaro (Rombo), Kiwira (Rungwe)
na Kawetire (Mbeya Vijijini).
Waziri
Mkuu ametoa agizo hilo leo (Ijumaa, Julai 8, 2016) na kufafanua kwamba usitishaji huo
unalenga kutathmini taratibu, kanuni na vigezo sahihi vinavyotakiwa kutumika
katika kugawa malighafi kutoka kwenye mashamba hayo.
Amesema wadau wote wa viwanda
vinavyojikita katika malighafi ya misitu na hususan wamiliki wa viwanda vya
kupasua mbao wanashauriwa kuwa watulivu wakati utaratibu huu ukifanyiwa mapitio
na umma utatangaziwa rasmi pindi uboreshaji huo utakapokamilika.
IMETOLEWA
NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU
2 MTAA WA MAGOGONI,
S. L. P. 3021,
11410 DAR ES SALAAM
IJUMAA, JULAI 8, 2016.
No comments:
Post a Comment