Advertisements

Sunday, August 14, 2016

KILA MTU KUPATA UMEME 2020

Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo akisalimiana na wanakijiji wa kata ya Kwamgwe iliyopo wilayani Handeni mkoani Tanga wakati alipofanya ziara kuangalia utekelezaji wa usambazaji wa umeme katika Jimbo la Handeni Vijijini kunakofanywa na Kampuni ya Future Century Limited. (Picha na Wizara ya Nishati na Madini).
WAZIRI wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo amesema serikali imeweka mikakati ya kuhakikisha kuwa ifikapo mwaka 2020 kila mwananchi anapata umeme wa uhakika na kuwezesha uchumi wa nchi kukua kwa kasi.

Aliyasema hayo baada ya kupokea taarifa ya utekelezaji wa miradi ya usambazaji wa umeme vijijini inayosimamiwa na Wakala wa Nishati Vijijini (REA) Awamu ya Pili (REA II) kutoka kwa watendaji wa Shirika la Umeme Nchini (Tanesco) mkoani Tanga.

Profesa Muhongo yupo mkoani Tanga kwa ajili ya kukagua miradi ya umeme vijijini inayotekelezwa na Rea pamoja na kuzungumza na wananchi.

Alisema kwa kutambua mchango wa nishati ya umeme katika ukuaji wa viwanda nchini, serikali imeweka mkakati wa kuhakikisha kuwa kasi ya usambazaji wa umeme vijijini inaongezeka ili ifikapo mwaka 2020 mgawo wa umeme uwe ni historia.

Alieleza kuwa serikali imeamua kuweka nguvu katika usambazaji wa umeme hususan katika maeneo ya vijijini ili kufuta umasikini, kwani kupitia nishati ya umeme wananchi waishio vijijini wana uwezo wa kuanzisha viwanda vidogovidogo na kuongeza ajira na kupunguza wimbi la vijana wengi kukimbilia mijini kwa ajili ya kutafuta maisha.

“Serikali iko makini katika kuhakikisha kuwa makandarasi wenye sifa wanapewa kazi ya kusambaza umeme vijijini, hatuhitaji makandarasi wasiotekeleza miradi kwa wakati,” alisema Profesa Muhongo. Ili kuendana na mahitaji ya umeme nchini, Profesa Muhongo aliitaka Tanesco kuhakikisha inaongeza megawati 200 za ziada ndani ya miezi 18.

Alisema wakati serikali kupitia Rea ikiendelea na kazi yake ya kusambaza umeme nchi nzima, shirika hilo linatakiwa kuhakikisha nishati ya uhakika inapatikana ikiwamo kubuni vyanzo vipya vya umeme.

Akielezea mpango wa utekelezaji wa miradi ya umeme vijijini itakayosimamiwa na REA Awamu ya Tatu, Profesa Muhongo alisema serikali imetenga zaidi ya Sh trilioni moja kwa ajili ya kusambaza umeme katika maeneo yote kipaumbele kikiwa ni katika vijiji vilivyokosa umeme REA Awamu ya Pili (REA II).

Hata hivyo, alieleza kuwa makandarasi waliokwamisha miradi ya REA Awamu ya Pili hawatapewa kazi ya kusambaza umeme vijijini katika REA Awamu ya Tatu.

Awali akielezea utekelezaji wa miradi ya umeme vijijini mkoani Tanga, Meneja wa Tanesco mkoani humo, Abdulrahman Nyenye alisema miradi ya umeme vijijini chini ya ufadhili wa Rea imekuwa ikitekelezwa katika wilaya zote nane za Tanga Mjini, Muheza, Korogwe, Handeni, Kilindi, Lushoto, Pangani na Mkinga ambazo zinapata umeme wake kutoka Gridi ya Taifa kupitia vituo vya Hale, Kange na Tanga (Majani Mapana).

Alisema kundi la kwanza lilihusisha wilaya za Korogwe, Lushoto, Handeni na Kilindi ambapo mradi wa wilaya hizo ulitekelezwa na mkandarasi STEG International Services Ltd ya Tunisia na kusimamiwa na Tanesco.

Alifafanua kuwa gharama za mradi huo ilikuwa ni Dola za Marekani 9,463,502 (Sh bilioni 14.6) na kwamba kundi la pili lilihusisha wilaya za Muheza, Mkinga, Tanga Vijijini na Pangani na kutekelezwa na mkandarasi Sengerema Engineering Group Ltd ya Tanzania na kusimamiwa na Tanesco.

Wakati huohuo, Waziri Muhongo amesema hakuna fidia yoyote itakayotolewa kwa wananchi watakaopisha ujenzi wa miundombinu ya kusambaza umeme wa Rea.

Aliyasema hayo alipozungumza kwa nyakati tofauti na wakazi kutoka katika vijiji vya Kweditibile na Kamgwe wilayani Handeni akiwa katika kukagua utekelezaji wa miradi ya usambazaji wa umeme vijijini.

Alisema serikali imetenga kiasi kikubwa cha fedha kwa ajili ya usambazaji wa umeme vijijini ambapo iwapo fedha hizo zitatumika kwa ajili ya kulipa fidia, inaweza kuathiri utekelezaji wa miradi ya Rea.

“Mkumbuke kuwa iwapo fedha hizi zitatumika kulipa fidia kwa wananchi wanaopisha miradi ya umeme vijijini, fedha nyingi zitatumika na kukwamisha utekelezaji wa miradi ya Rea,” alisema Profesa Muhongo na kuongeza kuwa miundombinu ya umeme haihitaji eneo kubwa hivyo haiwezi kuathiri mazao kwenye mashamba kama inavyoaminika na watu wengi.

HABARI LEO

No comments: