Advertisements

Saturday, August 6, 2016

Makala: Kiswahili na changamoto za kujitakia


Awali ya yote nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia pumzi na Afya, na kuweza kuandika mawazo yangu haya machache. Nikukumbushe kidogo japo kwa ufupi Kuhusu lugha ya Kiswahili ilipoanzia, Kiswahili kilikuwepo toka karne za mwanzo kabisa kikiwa katika mfumo wa vilugha vidogovidogo vilivyoitwa lahaja. “Lahaja ni vilugha vidogovidogo vya lugha moja ambavyo hubainika kijamii au kijiografia.”
Mnamo mwaka 1930 kulizuka mjadala wa kutafuta lugha itakayotumika katika ukanda wa Afrika Mashariki kwa ajili ya mawasiliano, biashara, na siasa. Kulianzishwa kamati ya lugha ya Afrika Mashariki iliyokua na kazi ya kutafuta lugha itakayotumika, ndipo kiunguja kikachaguliwa kati ya lahaja nyingi za lugha ya Kiswahili na kusanifishwa kutokana na kuenea kwake kuanzia unguja, bara mpaka kufika mashariki ya Kongo a idadi kubwa ya wasemaji.

Harakati ziliendelea baina ya wataalamu (wanaisimu) wa lugha katika kuongeza istilahi na misamiati ili kuifanya lugha iweze kukidhi mahitaji ya kila sehemu, wasanii mashuhuri kama Shaaban Robert walitumia sanaa kuieneza, kuitunza na kuikuza lugha ya kiswahili katika kila kona ya afrika mashariki, wanaharakati wa kupigaia uhuru nao walichangia kukisambaza/kuitangaza lugha.

Baada ya uhuru serikali nayo haikua nyuma katika kuhakikisha lugha ya Kiswahili inatumika, inakua na kuenea kila sehemu kwa kuunda chombo kitakacho simamia kiswahili (BAKITA), nao wataalamu kutoka taasisi ya uchunguzi wa kiswahili (TUKI) kutoka chuo kikuu cha Dar es salaam hawakua nyuma, walianzisha na kuchapisha kamusi mbalimbali za Kiswahili.

Tangu usanifishaji wake lugha ya Kiswahili kipindi cha ukoloni, harakati na changamoto zake katika kuikuza, kuieneza na kuisambaza kabla na baada ya uhuru mpaka kufikia leo 2016, Kiswahili kimekua kijografia na idadi ya wazungumzaji, sasa Kiswahili kina wazungumzaji zaidi ya milioni 100 dunia nzima, Kiswahili huzugumzwa katika nchi zaidi ya 15.

Kiswahili sasa kimekua miongoni mwa lugha zinazozungumzwa sana duniani, ni moja kati ya lugha 7 zinazozugumzwa zaidi duniani, Afrika kinashika nafasi ya pili, lugha ya kiswahili imekuwa na mafanikio makubwa duniani, ni lugha rasmi ya umoja wa Afrika, mashirika mbalimbali makubwa ya utagazaji duniani yameanzisha redio za kurusha matagazo yao kwa lugha ya Kiswahili ili kufikia jamii zinazozungumza kiswahili, Mfano BBC Swahili, Dira ya Dunia, Sauti ya
Amerika nk.

Kiswahili kimekua kikiwavutia wengi, imefikia hatua sasa inafundishwa katika vyuo vikubwa duniani, vyuo kama chuo kikuu cha mawasiliano ya habari china, chuo kikuu cha lugha za kigeni cha Beijing, chuo cha Glasgow, chuo cha Cambridge, Harvard, Stanford na vingine vingi.

Kwa Juhudi zote hizo zinazofanywa na wanaofanya kukikuza na kufanya kiswahili kiwafikie watu wengi zaidi duniani bado zinaonekana kutoendani na kasi ya ukuaji wa lugha yenyewe, wahusika wakuu wa lugha ambao ni nchi za afrika mashariki bado jitihada zetu kukifanya kiwe kikubwa zaidi ni ndogo, bado raia wake hatukizugumzi ipasavyo, bado hatujaamka kutumia fursa zilizopo mbele yetu Kupitia lugha yetu ambayo ndio inaonekana kubeba tamaduni za watu wa Afrika Mashariki, Kiswahili ni moja ya tanzu za mila, tamaduni na desturi zetu watu wa Afrika Mashariki hasa Tanzania.

Dhana ambayo ipo katika vichwa vyetu ni kuwa lugha yetu adhimu ya Kiswahili haijitoshelezi kimsamiati, inakosa istilahi kukidhi matakwa ya taaluma mbalimbali, lakini ukweli ni kwamba Kiswahili kimejitosheleza kimsamiati, Kiswahili ni kipana, Kiswahili ni kikubwa. Tatizo ni kukosa wazungumzaji ambao wako tayari kujua na kujifunza zaidi kufahamu vizuri maneno yake.

“Kweli penye miti hapana wajenzi,” kuna wengine wanakutana na maneno tofauti ya Kiswahili ambayo hawakuwahi kuyaona, ila kwakuwa tu wameshazoea kuyapatia mbadala wake kwa Kingereza basi utasikia “bora Kiingereza”. Watu wa zamani wanakwambia “fimbo ya jirani haiui nyoka”. Wakiwa na maana kwamba, matatizo yako usitegemee jirani yako akutatulie, onesha kwanza mweyewe unataka kujisaidia ili wa pembeni waweze kukusaidia.

Wa kuikuza lugha ni sisi wenyewe kwa mikakati thabiti na uhamasishaji wa hali ya juu katika kuifanya lugha ya kiswahili kua tishio zaidi duniani. Tunaposema tunataka kuipeleka mbele. Tanzania kiuchumi ili hali tamaduni zetu ziko nyuma, itakua jambo la kustaajabisha sana, kiswahili ni tamaduni yetu watanzania.

Najua hatupendi itolewe mifano ya nchi kama China, ila sidhani kama China walisema kwakuwa sisi bado hatujaendelea ndio kwanza tunajenga nchi basi tutumie Kingereza kwanza mpaka hapo tutakapo kua imara, la hasha, walipokuwa wanajenga nchi na tamaduni zao pia walikuwa
wakizidumisha. Ndio maana mpaka leo hii hawajui historia za nchi zigine zaidi ya zao wenyewe.

Haya turudi kwenye dhumuni kuu la hii makala fupi, changamoto kadhaa ambazo zikiangaziwa kwa stakiri hakika tutajivunia zaidi na lugha yetu adhimu hadi wanaokikosoa watuunge mkono, Fid Q aliwahi kusema “wafurahishe waliokaribu wa mbali watasogea.”

Tanzania kuna vyuo vikuu na vishirika vyake vitoavyo stashahada, shahada, shahada za uzamili na uzamivu za kiswahili (chuo kikuu huria cha Tanzania, chuo kikuu cha Dar es Salaam, chuo kikuu kishiriki cha Dar es salaam, chuo kikuu cha Dodoma, chuo kishiriki cha Mkwawa, hii inamaanisha kuna wawakufunzi/wahadhiri wa lugha ya Kiswahili katika hivi vyuo wanaojituma na kuhakikisha wanadahili na kutoa wahitimu watakao kidhi uhitaji wao katika maeneo mbalimbali yanatakiwa kua na wanaisimu.

Maswali ni mengi nayojiuliza katika ngazi hii ya vyuo, sawa vyuo vina toa wahitimu wengi wa Kiswahili lakini wanaishia wapi? Na ni kipi hasa wanafundishwa? Wanafundishwa ili waje kuwa wa kina nani baadaye? Wanaandaliwa vizuri kweli kuja kukabiliana na soko la ajira mtaani? Soko lenyewe ni lipi, wanaoneshwa au wanatakiwa wajioneshe? Mtanijibu.

Tumeanzisha hizi taaluma za Kiswahili Tanzania, Afrika na dunia kwa ujumla ili tukuze lugha na kuisambaza na kuwa na watu wengi wanaojua Kiswahili sanifu, wenye ufahamu yakinifu wa sarufi ya lugha yetu adhimu, Lakini wanaisambaza? Au Je, Wanatumika ipasavyo?

Kwanini vyuo Kupitia wakufunzi wao, kwa sababu (ni wanafunzi wengi wanamaliza) Kwanini wasikae wakabuni njia mbadala ya kuwatafutia ajira hawa watu? Mfano, kuna taaluma kadhaa ambazo huwa zinachangia moja kwa moja kuisambaza elimu katika jamii, taaluma za uandishi wa
habari na utangazaji, ukweli ni kwamba waandishi wa habari na watangazaji wanachangia kwa kiasi kikubwa kuharibu lugha, Kwanini vyuo na wizara husika wasikae na kufikiria kudahili hawa

Wataalamu wa lugha kuja kua watangazaji, wahariri au waandishi wa habari, au kupitishwe sheria vyuo vikuu kwamba lugha ya Kiswahili iwe ni lazima kwa kila ngazi ya uandishi wa habari. Hawa wataweza kueneza istilahi na maneno mengi sahihi ya lugha yetu na kufanya itumike zaidi kwani watu watakuWa wanasikia na kusoma mara kwa mara.

Mzizi wa wanafunzi wa shule za msingi kujua Kiswahili fasaha ni walimu, na ukweli ni kwamba walimu wetu wanaofudisha kiswahili sio wanaisimu/wataalamu wa Kiswahili, ni wanafunzi waliofaulu vizuri kiswahili na kuamua kurudi kufundisha kiswahili. Sasa tumepata kuanzisha taaluma ya Kiswahili, kwanini hawa wanaomaliza kusomea kiswahili ndio wasiwe walimu wa Kiswahili kuanzia ngazi ya msingi mpaka elimu ya juu? Au wapelekwe wakasomee ualimu na kurudi kufundisha wadogo na watoto wetu.

Je, Kuna ushirikiano kati ya wahadhiri wa hapa nchini na wa huko nje wanaofundisha taaluma hii ya kiswahili? Je wanaofundisha kiswahili huko nje ni kweli wanataaluma ya ualimu au walisomea kiswahili? Isijekua kuna walimu huko nje lakini hawajui vizuri sarufi ya lugha na kupotosha watu. Niishie hapo nisijetoka nje ya mada.

Turudi serikalini na taasisi zinazo linda na kutunza Kiswahili Tanzania, Wizara ya Habari, Utamaduni, Wasanii na Michezo, wizara ya elimu, sayansi, na teknolojia na Baraza la Kiswahili Tanzania.
Wizara zenye majukumu ya moja kwa moja katika kuhakikisha kiswahili kinakua na mizizi halisi yenye kuenea katika kila idara ni wizara ya elimu, sayansi, na teknolojia pamoja na wizara ya habari, utamaduni, sanaa na michezo, Je zinafanya nini? Kasi waliyonayo katika kushughulikia masuala ya lugha ina akisi kasi ya ukuaji na uhitaji wa kiswahili chenyewe duniani?

Je, kuna ushirikiano thabiti baina ya hizi wizara katika usimamizi wa hii lugha? Maana usijitape na minazi kama huwezi kuikwea. Umoja ni nguvu, utengano ni udhaifu, Tuseme wakaamua kushirikiana kwa pamoja kupitisha sera mpya na sheria mpya za matumizi ya lugha (sera na sheria za lugha katika elimu pamoja na shughuli mbalimbali za kibiashara na uchumi, hata kijamii) haya mabadiliko ukitoa tu kwa jamii husika kubadilika.

Chachu ya mabadiliko lazima ianzishwe na serikali Kupitia sera zake pamoja na sheria ili kuongeza uhamasishaji wa matumizi ya kiswahili nchini. Serikali Kupitia wizara hizi mbili wapitishe sheria kwa vyuo na kwenye mashirika ya utangazaji pamoja na taasisi zake kuhusu kutumia kiswahili.

Mfano. Kupitishwe sheria kwa waandishi wa habari na watangazaji wawe wamesomea lugha ya Kiswahili (wawe na vyeti). Ufundishwaji wa somo la lugha katika kila taalamu vyuoni, walimu wa Kiswahili wawe wamesoma lugha kwa ngazi kutokana na ngazi wanayofundisha.

Serikali iwauganishe wahadhiri wa Kiswahili Tanzania na wale wa nje ya nchi ili kuleta usawa wa ufundishaji duniani kote, mafunzo ya lugha yetu yalandane na kila upande wa dunia, kubuniwe mashindano na Harakati mbalimbali za lugha duniani kote.

Sidhani kama ninayosema hayawezekani kama tukiamua kweli kuyafanya kwa minadhiri ya kutunza utamaduni, mila na desturi. Kiswahili ni moja ya tanzu na njia za kutunza mila, desturi na tamaduni zetu, kiswahili ni fahari ya mtanzania. Sijawasahau BAKITA, yawapasa serikali kuliunda upya Baraza hili la Kiswahili Tanzania liendane na wakati, vijana kutoka vyuoni wanaosomea kiswahili wawekwe pale, Baraza liundwe upya lisimamie lugha ipasavyo, lichapishe kamusi na vitabu vya sarufi ya lugha, vitabu vya hadithi, methali, misemo, misamiati na semi zingine (wa kutunza kiswahili ni sisi wenyewe sio wageni).

Wataalamu wapo, Kwanini wasituthibitie ubora na utajiri wa lugha hii rahisi na tamu kinywani mpaka kichwani? Kiswahili chenyewe kinatusikitikia “kweli penye miti hapana wajenzi.” Hatuna sababu ya kushindwa kuinyanyua na kuithamini hii lugha ikiwa tuna wanaisimu wasio na kazi mtaani na wengine wapo mavyuoni. Eti jamani, wanamaliza vipi shahada bila kufanya uchunguzi Kuhusu jamii zetu
na lugha yetu tukazisoma?

Wa mwisho kabisa ni wanaisimu wenye, kweli mnamaliza na mnakosa cha kuifanyia hii lugha? Mbona fursa zipo nyingi Kupitia hii lugha au ndio msemo wa mtaani “ukiwa nje ya mchezo unaona kweli”? ila sidhani kama ni hivyo kweli, Kiswahili bado kina mambo mengi ya kukifanyia,
ikiwa waliamua kusomea hii lugha maana yake wanaipenda, basi na wafanye yanayotakikana kufanyika. Wakijiunga vikundi kwa vikundi wakagawana kazi.

Mgaagaa na upwa hali wali mkavu” wajuzi wa lugha wanasema, huwezi ukajituma na ukakosa hata chochote kitu, wajuzi wa hii lugha wanaosema hawana kazi na waamke wafanye kitu kwa ajili ya hii lugha.

Ukitoa tu wasomi, serikali, vyuo na vyuo hata sisi wananchi hatuoneshi nia kweli ya kutaka kujua Kiswahili fasaha, tumejawa na kasumba nyingi za kutokuthamini lugha yetu, tumejawa na shauku za kujua lugha za wenzetu pasi na kujali ya kwetu, tunaongea tu kiswahili kwa sababu tumewakuta watu wanaotuzunguka wanakizungumza.

Tumekuwa tukishangaa sana pale tunapokutana na maneno ambayo hatukuwahi kuyasikia kabla na kuona bora kuyapatia mbadala wake kwa lugha nyingine. Ila tukumbuke kisichotumika hupotea.

Ni rai yangu kwa wadau wote wa kiswahili kuungana kwa pamoja kuithamini na kutukuza lugha hii adhimu ya kiswahili, ili kuifanya iwe ya kwanza duniani na kuweza kutunza utajiri wetu wa lugha na jamii. Matumizi fasaha ya kiswahili huleta utulivu wa moyo na fikra. Matumizi fasaha ya kiswahili huongeza hali ya unzalendo katika nyoyo na akili zetu.

Ningependa kuishia hapa maana wenyewe wanasema mwenye busara huweka akiba ya maneno na siku zote akiba haiozi. Basi mi sina budi kuweka kalamu chini, poleni sana na samahani kama kuna niliowakwaza.

Kama nimekosea basi nikosoe nijirekebishe siku nyingine.

IMEANDIKA KWA NA:

BARAKA HEMEDI JEREKO

Twitter @jerekojr

Jereko98@gmail.com 0788121085
Credit:BONGO5

No comments: