Advertisements

Thursday, August 4, 2016

UWANJA MPYA WA NDEGE DAR KUKAMILIKA MWAKANI

MAMLAKA ya Viwanja vya Ndege nchini (TAA) imeainisha mikakati yake ya kufanya maboresho katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) kwa kuboresha jengo la abiria (terminal II), ambayo yataenda sambamba na ujenzi wa terminal III.

Aidha, imesema iko kwenye mchakato wa kufanya upembuzi yakinifu kwa ajili ya ujenzi wa njia ya kurukia ndege. Pia, imepanga kuoanisha mifumo ya mawasiliano na usalama katika majengo matatu ya abiria ya uwanja huo (terminal I, II, III).

Hayo yameelezwa na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TAA, Ramadhan Maleta wakati akizungumza na viongozi wa dini na wajumbe wa Kamati ya Amani ya Mkoa wa Dar es Salaam, waliotembelea ujenzi wa mradi huo wa jengo hilo. Maleta alisema maboresho ya jengo la terminal II, yataanza mwakani na kwamba kwa sasa Serikali iko katika mchakato wa kutafuta pesa kwa ajili ya kufanya maboresho hayo.

“Tunataka kujenga njia nyingine ya kurukia ndege, kwa sababu wataalamu walifanya utafiti wakasema kwamba kufikia mwaka 2025, barabara hii moja ya sasa haitatosha kwa matumizi,” alisema Maleta.

Awali, akizungumza kwenye ziara hiyo, Mwenyekiti wa Kamati hiyo na Shehe wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhad Mussa Salum alisema mradi huo kama utakamilika kwa wakati, utawasaidia Watanzania na pia utaongeza idadi ya ndege kubwa kutua nchini.

Alisema ujenzi wa jengo hilo ni ishara tosha kuwa Serikali inafanya kazi kubwa ya kuwaletea wananchi wake maendeleo na kwamba kamati hiyo itashirikiana na Serikali si tu katika kuhamasisha masuala ya amani bali hata maendeleo.

“Mradi huu si tu utawasaidia Watanzania, lakini pia utaleta heshima kwa nchi kwa kuwa na viwanja vinavyoendana na hadhi ya Watanzania. Sisi tunaunga mkono juhudi za Serikali kuwaletea maendeleo wananchi,” alisema Shehe Alhad.

Katibu wa Kamati hiyo, Padri John Solomon alisema kikubwa kilichowafanya kutembelea mradi huo ni kutaka kuona juhudi za Serikali, kuhakikisha Tanzania inakuwa na uwanja mkubwa wa kisasa.

Mbali na ziara hiyo, kamati hiyo pia ilitumia nafasi hiyo kufanya maombi na dua kwa ajili ya mradi huo ili uweze kukamilika salama, bila kutokea kwa tatizo la aina yoyote ambalo linaweza kukwamisha.

Akitoa ufafanuzi wa mradi huo, Mkurugenzi wa Mradi huo, Mohammed Millanga alisema, ujenzi wa jengo hilo litakalohudumia abiria milioni sita kwa mwaka, unatarajiwa kukamilika Desemba mwakani.

Alisema hadi sasa mradi huo ambao ulikuwa utekelezwe kwa awamu mbili kwa sasa, awamu hizo zinatekelezwa kwa pamoja na umekamilika kwa asilimia 45.

Hata hivyo, Millanga alitaja baadhi ya changamoto, kuwa ni maandalizi ya ufunguzi wa jengo hilo, ambapo alisema wameshaanza kulifanyia kazi jambo hilo. Changamoto nyingine ni jinsi ya kuoanisha mifumo ya mawasiliano na usalama katika majengo matatu ya abiria.

“Kitu kingine ni kwamba wadau walikuwa wanataka mambo mbalimbali, lakini sisi inabidi tufanye kazi ndani ya bajeti iliyopangwa ili mambo yaweze kwenda vizuri,” alisema Millanga.

HABARI LEO

No comments: