Advertisements

Friday, September 9, 2016

MCHEZAJI WAZAMANI WATIMU YA TANZANIA ‘TAIFA STARS’, MOHAMMED MSOMALI AFARIKI JAMAL MALINZI ATUMA SALAM ZA RAMBIRAMBI

Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Jamal Malinzi amemtumia salamu za rambirambi Mwenyekiti wa Chama Cha Soka Mkoa wa Morogoro (MRFA), Paschal Kihanga kutokana na kifo cha Kocha na mchezaji mahiri wa zamani wa Timu ya Tanzania ‘Taifa Stars’, Mohammed Msomali.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka MRFA, Kocha Mohammed Msomali ambaye anaweza kuelezwa kuwa ‘gwiji’ la kandanda la Tanzania, alifikwa na umauti Septemba 08, 2016 saa saba mchana akiwa nyumbani kwake akisubiri kupata mlo wa mchana. Amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 74.
Taarifa za awali zinaeleza siku mbili zilizopita, Kocha Msomali alilalamika kuugua kifua na kwamba baada ya kupata tiba mchana, alijipumzisha akisubiri kupata mlo wa mchana, lakini walipokwenda kumwamsha, alikutwa amefariki dunia. 
Anatarajiwa kuzikwa kesho Septemba 09, 2016 saa 7 mchana mara baada ya swala Ijumaa.
Mbali ya salamu hizo kwenda MRFA, Rais Malinzi pia ametuma salamu za rambirambi kwa familia ya Marehemu Msomali, ndugu, jamaa na marafiki huku akiwataka kuwa na moyo wa subira wakati huu mgumu wa msiba wa mpendwa wao.

Katika nafasi za uchezaji, historia inaonesha kuwa Msomali nyota yake ilianza kuonekana kwenye timu mahiri ya Cosmopolitan ya Dar es Salaam kabla ya kuchezea klabu nyingine za Young Africans pia ya Dar es Salaam, Mseto ya Morogoro, Timu ya Mkoa wa Morogoro ‘Moro Stars’ na Timu ya Tanzania ‘Taifa Stars’ kadhalika timu ya Bara ambayo ni maarufu kwa jina la Kilimanjaro Stars.
Wakati wa uhai wake, Msomali amepata kuzifundisha Mseto na Tumbaku za Morogoro ambayo aliipa ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara (Klabu Bingwa Tanzania) mwaka 1975. Pia alizinoa Young Africans, Timu ya Mkoa wa Morogoro ‘Moro Stars’ na kwa muda mrefu timu ya Tanzania ‘Taifa Stars’ sambamba na ile ya Bara ambayo ni maarufu kwa jina la Kilimanjaro Stars.
Mwenyezi Mungu ailaze roho ya marehemu Mzee Mohammed Msomali mahala pema peponi.
Innalillah Wainnailaihi Raajiuun – Hakika sisi ni wa Mungu, na kwake tutarejea.

No comments: