Advertisements

Tuesday, September 20, 2016

RAIS MAGUFULI AWALILIA WALIOKUFA AJALI YA BASI NJOMBE

RAIS Dk John Magufuli ametuma salamu za rambirambi kwa familia za watu walliokufa katika ajali ya basi la Kampuni ya New Force iliyotokea Septemba 19, 2016 saa 2:00 usiku katika Kijiji cha Lilombwi, Kata ya Kifanya, Tarafa ya Igominyi Mkoani Njombe ambapo watu 12 wamepoteza maisha na wengine 28 kujeruhiwa.
Basi hilo limepinduka katika kona ya barabara wakati likisafiri kutoka Dar es Salaam kwenda Songea Mkoani Ruvuma.
Katika salamu hizo kupitia kwa Mkuu wa Mkoa wa Njombe Dk Rehema Nchimbi, Rais Magufuli amesema amepokea taarifa za ajali hiyo kwa masikitiko makubwa na kwamba anaungana na familia, ndugu, jamaa na marafiki wote waliopatwa na msiba katika kipindi kigumu cha majonzi.
"Ndugu Mkuu wa Mkoa wa Njombe Dkt. Rehema Nchimbi naomba unifikishie pole nyingi kwa wote walipatwa na msiba, wamewapoteza wapendwa wao, wamewapoteza watu waliowategemea na hakika familia zimetikisika.
"Sote tuwaombee wote waliofikwa na msiba wawe na moyo wa subira, uvumilivu na ustahimilivu na pia tuwaombee Marehemu wote wapumzishwe mahali pema peponi, Amina" Amesema Rais Magufuli.
Rais Magufuli pia amewapa pole majeruhi wote na amewaombea wapone haraka ili waweze kuungana na familia zao na kuendelea na shughuli zao za kila siku.

No comments: