Advertisements

Thursday, September 1, 2016

SERIKALI NZEGA YAKUTANA NA VIONGOZI WA VYAMA VYA SIASA

Image result for NZEGA TOWN
Na Mussa Mbeho, Tabora

SERIKALI wilayani Nzega Mkoani Tabora imechukua hatua za makusudi za kukutana na kujadiliana na viongozi mbalimbali wa dini na vyama vyote vya siasa vilivyoko wilayani humo kwa lengo la kuhakikisha amani na usalama vinaendelea kudumishwa.

Mkutano huo wa amani uliofanyika juzi wilayani humo uliandaliwa na Mkuu wa wilaya hiyo Godfrey Ngupula akishirikiana na Kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya kujadili na kukubaliana na wanasiasa umuhimu wa kudumisha amani na usalama wilayani humo.

Aliwakumbusha viongozi wa dini na Makatibu wa vyama vya siasa vya
NCCR-MAGEUZI, CUF, ACT-WAZALENDO, CHADEMA, TADEA, UDP, UPDP na JAHAZI
ASILIA kuwa vyama vyote ni sawa na kila kimoja kinapaswa kudumisha amani ya nchi katika utekelezaji shughuli zake huku kikijiepusha na
vurugu zisizo na tija.

Alisema wilaya yake imekuwa na utaratibu wa kukutana mara kwa mara na kujadili kwa uwazi jambo lolote bila shida na wanasikilizwa na kuongeza kuwa changamoto inayowakabili wana Nzega sio kubinya demokrasia kama inavyoelezwa bali ni kujiletea maendeleo.

‘Ndugu zangu tunapaswa kuwa kitu kimoja, fikirieni kwa makini kama ipo haja ya kuchukuliwa na upepo kwa dhamira ya kutaka demokrasia huku mkihatarisha amani ya nchi’, aliasa.

Alisema mikakati inayofanywa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo ya kulazimisha kufanya mikutano na maandamano nchi nzima hapo Septemba 1 mwaka huu haikubaliki kwani itasababisha uvunjifu wa amani, kama kuna tatizo linatatuliwa kwa njia ya mazungumzo zaidi kuliko hii ya
msuguano.

Alitanabaisha kuwa Nzega ina changamoto nyingi zinazopaswa kushughulikiwa ikiwemo ya elimu kwani wilaya hiyo imekuwa ya mwisho kwa miaka mitatu mfululizo katika matokeo ya darasa la saba.

Aidha alisema wilaya hiyo pia inaongoza kwa matukio ya mauaji kutokana na imani za kishirikina na pia kumekuwa na ongezeko kubwa la utoro wa wanafunzi mashuleni na mimba za utotoni.

Alisema UKAWA walizunguka nchi nzima kumnadi Lowassa kwa mbwembwe zote, lakini Mungu si Athumani, ametupatia Dr Magufuli asiye na mzaha na maendeleo ya nchi, hivyo haoni mantiki ya watu kuwa tayari kufa eti kisa wanakataliwa wasifanye mikutano.

Ili kuhakikisha Nzega inabaki katika utulivu na amani na hata baada ya Septemba Mosi, Ngupula aliahidi kuendelea kukutana na viongozi hao kwa lengo la kujadiliana na kutafuta mwafaka wa ki wilaya kwa jambo lolote kwa manufaa ya wananchi.

Wajumbe walikubaliana kuwa haina haja kuingia katika maandamano hayo kwani sio kipaumbele cha wana Nzega, japokuwa mjumbe kutoka CHADEMA licha ya kuelewa maelezo ya DC bado alionekana kukubali kwa shingo upande.

No comments: