Advertisements

Thursday, September 15, 2016

WAATHIRIIKA WA TETEMEKO WATOA YA MOYONI

WANANCHI wa Manispaa ya Bukoba, walioathiriwa na tetemeko kubwa la ardhi lililotokea Jumamosi iliyopita, wametoa ya moyoni baada ya kutaka watendaji na wenyeviti wa mitaa mkoani Kagera, wafanye tathimini ya haki kwa waathirika hao ili wapate takwimu sahihi zitakazowezesha kupatiwa msaada kama ilivyolengwa.

Aidha, wamewataka watendaji na wenyeviti hao, kuhakikisha wanatoa haki sawa kwa kila mtu aliyeguswa na janga hilo; na si kubagua kama wanavyofanya sasa. Wananchi hao wametoa kilio chao jana mbele ya Mwenyekiti wa Taifa wa Jumuiya ya Wazazi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abdallah Bulembo ambaye alikuwa na ziara ya kukagua maeneo yaliyoathiriwa na tetemeko hilo na kuwapa pole waathirika hao.

Mkazi wa Kata ya Hamgembe Omukishenye ambaye ameathiriwa na tetemeko hilo, Joyce Joseph ambaye nyumba yake ilianguka na kwa sasa analala nje na familia yake ya watu saba, alimueleza Bulembo kuwa watendaji walifika na kuangalia nyumba kwa nje, wakaandika na kuondoka.

Wananchi hao walisema wanapowaomba watendaji hao, waingie ndani waone madhara yaliyotokea, wanajibiwa vibaya, hali inayowafanya waone kama serikali yao imewatelekeza.

“Tunashukuru wewe kuja kutusalimia na kutuletea misaada, leo ni siku ya tano tunalala nje, hatuna chakula, hatuna chochote tuko kama unavyotuona. Pia tunaomba uwaagize watendaji na wenyeviti wa mitaa na vijijini wafanye tathimini ya kina; mfano zipo baadhi ya nyumba ukipita nje unaona nyufa, lakini ukiingia ndani kuta zote zimeanguka, tukiwaeleza, waingie ndani wanatwambia nyamaza msitusumbue,” alidai Joyce.

Mkazi wa Kata ya Kashai, Amoni Mwijage alisema wapo baadhi ya wenyeviti wa mitaa, wanapopita wanabagua wakati wa kuandika majina kwa ajili ya tathimini na wanaiendesha kisiasa.

“Kama mwenyekiti ni wa chama fulani anasema hakuna kumuandika huyu kwa sababu si wa chama chetu, lakini wajue kuwa sisi tunaumia na wote tunahitaji misaada na hili janga sio kwamba tuliliomba kuwa hivi. Sisi hatuwezi kuhama maeneo yetu kwenda kwenye kambi na kuacha vifaa vyetu watuletee mahema ya muda hapa tulipo wakati utaratibu ukiendelea wa kutuletea msaada zaidi,” alisema Mwijage.

Baada ya Bulembo ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM kusikia malalamiko hayo kutoka kwa wananchi hao aliowatembelea na kujionea hali iliyopo, alimwagiza Mkuu wa Mkoa wa Kagera na Kamati yake ya Ulinzi na Usalama kufanya tathimini kwa kina na kwenda ndani zaidi na kulenga mkoa mzima, kwani waathirika hawapo Manispaa ya Bukoba tu; na endapo hawatafanya hivyo, lawama zitakuwa kubwa na lengo lililokusudiwa halitafikiwa.

“Watu wanaoenda kufanya tathimini na kuandika majina ya watu waingie ndani ya nyumba, wajiridhishe ni kipi kinachoendelea sio kupita nje wakaandika takwimu zisizo sahihi, wakati madhara ni makubwa. Pia hili janga lisiingizwe katika mambo ya kisiasa wala itikadi fulani…hili ni janga la Watanzania wote na ni msiba wetu sote, maana wananchi wamesema wanabaguliwa kwa mambo ya kisiasa, hawaandikwi kwa sababu ya mtu ni chama fulani, alisema Bulembo.

Aidha, Bulembo alitoa msaada wa vitu mbalimbali vikiwemo vyandarua, kilo 500 za mchele, maji ya kunywa, chumvi, shuka, maharage kilo 250 na mablanketi vyenye thamani ya Sh milioni 6.8, na Sh milioni mbili taslimu kukarabati Shule ya Sekondari ya Omumwani, inayomilikiwa na Jumuiya ya Wazazi Bukoba Mjini. Fedha zote ni Sh milioni 8.8.

Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Salum Kijuu alisema taarifa za sasa kuhusu hali ilivyo ikiwamo nyumba zilizoathirika, zikiwemo zilizoanguka 840 na zenye nyufa kubwa 1,264 ilikuwa ya awali, lakini tathimini inaendelea na mpaka sasa inakadiriwa nyumba 5,000 zimeathiriwa na tukio hilo, ambalo halijawahi kutokea Tanzania.

Kijuu alisema majeruhi wamepungua na kubaki 51 kati ya 170 waliokuwa amelazwa, ambao 23 kati ya hao wanahitaji kufanyiwa upasuaji.

“Lakini bado wananchi wanalala nje hatujapata mahema, kwa sasa wataalamu wa jiolojia watapita mitaa yote ili kutoa elimu kwa wananchi ili waweze kujikinga vipi pale wanapohisi hali kama hiyo, pia Ubalozi wa China umeagiza dawa, ziko njiani zinaletwa kwa ajili ya waathirika hao,” alisema Kijuu na kuongeza:

“Kwa hatua za mwanzo tunapanga kuwapatia wananchi kila familia bati 20 na mifuko mitano ya saruji huku wapangaji walioathirika watapewa shilingi 120,000 kwa ajili ya kulipia kodi kwa muda wa miezi sita. Pia mpaka sasa wapo madaktari 13 wa kawaida kutoka Hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando, madaktari bingwa watano wakiambatana na mkurugenzi wa hospitali hiyo ya rufaa, wataalamu wa usingizi wawili, madaktari wa upasuaji wanne, muuguzi wa kawaida mmoja na madaktari sita kutoka China.”

Misaada mbalimbali imeanza kutolewa, kwa wabunge kutoa posho yao ya siku moja huku Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akichangisha zaidi ya Sh bilioni 1.4 kutoka kwa Jumuiya ya Mabalozi na wafanyabiashara nchini kwa ajili ya kuwasaidia waathirika wa tetemeko hilo.

Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Jiolojia nchini, Profesa Abdukarim Mruma alisema tangu Tanzania ipate Uhuru, hili ni tetemeko la tisa kutokea lakini mengine yalikuwa madogo, tofauti na la Jumamosi, kwani wamefanya utafiti na kugundua kitovu cha tetemeko hilo ni wilayani Missenyi katika Msitu wa Minziro.

“Hatuna chombo cha kutabiri matetemeko kabla ya kutokea dunia nzima hakuna kipimo hicho, hatumung'unyi maneno matetemeko yatazidi kutokea, lakini madogo ila tulichogundua ni kwamba Kagera iko karibu na Bonde la Ufa na pia miamba iliyoko chini ni laini ukilinganisha na Mkoa wa Mwanza kwa hiyo inasababisha tetemeko likitokea hata dogo lazima lilete madhara fulani,” alieleza Profesa Mruma.

Aliwashauri wananchi kuacha kukimbia nyumba zao pindi wanapoona au kusikia dalili ya tetemeko hilo, bali waingie uvunguni mwa meza, vitanda au katika kingo za nyumba ambako wanakuwa salama zaidi kwani tetemeko linachukua sekunde zisizozidi nane kupita wakati watu wakikimbia wanakutana na kuta au milango inayowadhuru.

HABARI LEO

No comments: