Advertisements

Thursday, September 15, 2016

WAPINGA KULAZIMISHWA KUSOMA ILANI YA CCM

By Juma Ng’oko, Mwananchi jng’oko@mwananchi.co.tz

Mwanza. Baadhi ya wakuu wa idara na vitengo wa Manispaa ya Ilemela mkoani hapa wamepinga agizo la kutakiwa kusoma na kuielewa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015 hadi 2020.

Wakuu hao wanadai kuwa agizo hilo linakiuka Katiba ya nchi kuhusu haki ya mtu kuchagua chama anachokitaka.

Agizo hilo lilitolewa na Mkuu wa Wilaya ya Ilemela, Dk Leonard Masale kwenye mkutano na watumishi hao.

“Atakayeona hawezi kufanya hivyo, afadhali aache kazi kwa hiari yake badala ya kusubiri kutumbuliwa,” amesema Dk Masale.

Amesema hawezi kufanya kazi na watumishi wa umma ndani ya ofisi yake au manispaa ambao hawatekelezi yaliyomo kwenye Ilani ya CCM kwa kuwa ndicho chama kilichoshika Serikali inayotawala.

Pia, amewataka kuhakikisha vinafanyika vikao mara kwa mara vya watumishi wa kila idara, kuanzisha dawati la mafunzo kwa wenyeviti wa Serikali za mitaa na kubaini watumishi hewa.

Mtumishi aliyezungumza kwa sharti la kutotajwa jina lake gazetini, amesema baada ya kikao hicho kuwa agizo la kusoma Ilani ya CCM ni sawa na kuingilia uhuru wa watumishi.

“Kauli hii ni ya kibabe, ambayo kwa namna moja au nyingine inaingilia uhuru wa mtu kuamini chama akipendacho,” amesema mtumishi huyo.

No comments: