ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, October 1, 2016

BALOZI SEIF AWATOA HOFU WANANCHI, ASEMA SMZ IPO MAKINI KATIKA MIKATABA YA MASUALA YA MAFUTA NA GESI ASILIA

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif akiahirisha Mkutano wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar uliokuwa ukifanyika katika Ukumbi wa Baraza hilo uliopo Mbweni nje kidogo ya Kusini mwa Mji wa Zanzibar.
Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar wakisikiliza Hotuba ya kufungwa kwa Baraza la Wawakilishi iliyotolewa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi hayupo pichani.


Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar wakisikiliza Hotuba ya kufungwa kwa Baraza la Wawakilishi iliyotolewa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi hayupo pichani.Picha na – OMPR – ZNZ.


Serikali ya mapiduzi ya Zanzibar imejipanga vyema kuingia katika mikataba bora na Makampuni au Taasisi zitakazohusiana na uendeshaji wa miradi katika sekta ya mafuta na gesi asilia mikataba ambayo itafanywa kwa uwazi na makini ili iweze kuleta tija kwa Taifa pamoja na Wananchi wote. 

Akitoa Hoja ya kuahirisha Mkutano wa Tatu wa Baraza la Tisa la Wawakilishi Mbweni nje kidogo ya Mji wa Zanzibar Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema Serikali inatambua hofu waliyonayo baadhi ya wananchi juu ya mikataba ya masuala ya mafuta na gesi asilia. 

Balozi Seif Ali Iddi alisema Serikali kwa kuitambua hofu hiyo imeamua mikataba yote inayohusiana na Sekta hiyo itashuhudiwa na watu wote kupitia vyombo vya Habari lengo ni kuwa na uwazi ambao utalipatia heshima Taifa na kupunguza malalamiko na minong’ono isiyokuwa ya lazima. 

Hata hivyo alitanabahisha Umma kwamba kilichopo kwa hivi sasa ni sheria na sio mafuta na wataalamu bado wanaendelea kufanya utafiti wa uwepo wa mafuta na gesi Zanzibar na utakapokamilika kiwango cha nishati hiyo kitajuilikana Nchini hapo baadae.

Balozi Seif alisema ni ukweli usiopingika kwamba kupatikana kwa nishati ya mafuta na Gesi asilia hapa Nchini kutaiwezesha Zanzibar kukua kwa haraka uchumi wake kwa kuongeza mapato ya Serikali, Wananchi sambamba na kuongezeka kwa ajira hasa kwa Vijana.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alieleza kwamba kupitishwa kwa Mswada wa Mafuta na Gesi asilia ni jambo la Kihistoria kwa Taifa kwa vile Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi amekubali kuiweka saini sheria hiyo mbele ya vyombo vya Habari, Kamati ya Katiba na Sheria ya Baraza la Wawakilishi pamoja na Kamati ya Uongozi ya Baraza la Wawakilishi.

Akizungumzia suala la Tetemeko la Ardhi lililoikumba Mikoa ya Kagera Mwanza na ile ya Jirani huko Tanzania Bara, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif aliwashukuru Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kwa uamuzi wao wa kuchangia posho ya siku Moja kwa kila Mjumbe wa Baraza hilo ili iwasilishwe katika Mikoa iliyopatwa na Tetemeko hilo.

Balozi Seif alisema moyo uliyoonyeshwa na Waheshimiwa wajumbe wa Baraza hilo wa kulijadili suala hilo na hatimae kutoa maamuzi ya kuchangia wahanga wa Tetemeko hilo umeonyesha mshikamano mkubwa uliopo wa Watanzania katika kusaidiana na kufarijiana kila maafa yanapotokea katika sehemu moja ya Muungano.

Alitoa wito kwa Wananchi wote wa ndani na nje ya Tanzania kuendelea kuchangia kwa hali na mali ili kurejesha hali ya Mikoa iliyoathirika kwa tetemeko la ardhi lililotokea Tarehe 10 Septemba mwaka huu na kuleta vifo, majeruhi na kuathirika kwa miundo mbinu na makazi ya Wananchi.

Kuhusu zoezi la kuwahamisha Wafanyabiashara wa Makontena Darajani na wale wa Jengo la Treni na kuwahamishia Saateni lililoanza Tarehe 15 Febuari mwaka huu, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisema uamuzi huo wa Serikali umetokana na haja ya kubadilisha mandhari na haiba ya Mji wa Zanzibar.

Alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ina ya dhati ya kuuletea Mji wa Zanzibar haiba inayostahiki na kamwe sio kuwakomoa wafanyabiashara hao kama inavyodaiwa na baadhi ya Watu wasioitakia mema Zanzibar.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliendelea kutoa Taarifa kwamba zoezi hilo ni la kudumu la litaendelea kutekelezwa na Serikali katika maeneo mengine ambayo Wafanyabiashara wameamua na kuvamia kufanya biashara zao bila ya mpango maalum.

“ Itakumbukwa kwamba mnamo tarehe 15 Febuari 2016 Serikali iliamua kuhamishwa wafanyabiashara wa makontena darajani na wale wa Jengo la Treni na zoezi likaanza rasmi tarehe 15 lengo ni kuweka haiba nzuri ya mji na sio kuwakomoa wafanyabiashara hao ”. Alisema Mtendaji Mkuu huyo wa Serikali.

Balozi Seif Ali Iddi aliwaomba Wananchi wote hasa wafanyabiashara kuendelea kuunga mkono zoezi hilo linalofanywa na Serikali kwa lengo la kujengewa miundombinu imara na ya kisasa itakayotowa fursa kwao kufanya biashara ya uhakika itayokwenda sambamba na mazingira yanayokubalika Kimataifa.

Miswada Mitano imejadiliwa na kupitishwa kuwa sheria kwenye Baraza hilo la Wawakilishi Zanzibar ambayo ni pamoja na Mswada wa sheria ya kuanzisha Taasisi ya elimu ya Zanzibar na Mambo mengine yanayohusiana na hayo pamoja na mswada wa sheria ya marekebisho ya sheria mbali mbali na kuweka masharti yaliyo bora kuhusiana na mambo hayo.

Mengine ni mswada wa sheria ya kurekebisha sheria ya Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar nambari 8 ya mwaka 1999 kama ilivyorekebishwa na sheria nambari 11 ya mwaka 2009 na kuwekwa masharti bora pamoja na mambo mengine yanayohusiana na hayo, mswada wa sheria ya mafuta { utafiti na uchimbaji } na gesi asilia pamoja na mswada wa sheria wa kufanya marekebisho ya 11 ya Katiba ya Zanzibar inayohusu kifungu cha 66.

Kwa kupitishwa mswada huo Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kwa sasa ataweza kuzitumia nafasi zake 10 bila ya kuwepo masharti magumu ya Kikatiba na hasa kuhusiana na nafasi mbili kwa ajili ya upande wa upinzani.

Baraza la Wawakilishi Zanzibar limeahirishwa hadi Jumatano ya Tarehe 23 Novemba mwaka huu wa 2016 mnamo saa 3.00 asubuhi.

Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

No comments: