ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, October 5, 2016

HALMASHAURI YA JIJI LA ARUSHA YAKANUSHA KUTUMIA MAFUTA LITA ZA MAFUTA 1900.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Arusha ndugu Athuman J. Kihamia anapenda kukanusha na kutoa ufafanuzi juu ya taarifa iliyosambazwa kwenye mitandao ya kijamii kuhusu matumizi ya mafuta lita 1900. Halmashauri ya Jiji la Arusha ina jumla ya Idara 13 na Vitengo 5. Idara ni Utawala, ujenzi, Fedha, Elimu Msingi, Elimu Sekondari, Maendeleo ya Jamii, Afya, Usafishaji na Mazingira, Mipangomiji, Mipango   Takwimu na Ufuatiliaji na Maji. 

Vitengo ni Ugavi, Ukaguzi wa Ndani, Sheria na Uchaguzi. Katika Idara zote kuna jumla ya magari 48 mitambo 5 na wastani wa matumizi ya mafuta kwa Idara zote ni lita 18,900 kwa mwezi na Idara zenye matumizi makubwa ni ujenzi na usafishaji na mazingira hii inatokana na Idara hizi kutumia idadi kubwa ya malori na mitambo katika kutekeleza shughuli zake.  Mafuta yanaweza kununuliwa kwenye vituo binafsi endapo itatokea dharura na GPSA inakosa mafuta na manunuzi yatafanywa kwa kuzingatia bei isiyozidi viwango vya GPSA.

Baadhi ya watu wasiokuwa na nia njema wanasambaza  taarifa hizo katika mitandao ya kijamii kutokana na juhudi mbalimbali ambazo Mkurugenzi amekuwa akizifanya za kutatua kero mbalimbali kwa kubana matumizi yasiyokuwa ya lazima zikiwemo posho mbalimbali za watumishi na Waheshimiwa Madiwani. Fedha nyingi huelekezwa katika huduma mbalimbali za jamii kama vile afya na elimu.


Hata  hivyo kumekuwepo baadhi ya watu wasiokuwa waaminifu ambao wamejipanga kuchafua kila jambo jema linalofanywa na Mkurugenzi wa Jiji nia yao kuu ikiwa ni kumtoa kwenye lengo kuu la kuwahudumia wananchi bila ubaguzi wa aina yoyote, kusimamia miradi ya maendeleo na matumizi ya fedha zinazotokana na kodi za wananchi na ruzuku toka Serikali Kuu zilizokuwa zikitumika kinyume na utaratibu. 

Aidha Mkurugenzi  Kihamia amekuwa akipokea jumbe za vitisho na matusi kutoka kwa baadhi ya Madiwani lengo likiwa ni kudhoofisha juhudi anazozifanya za kuliweka  Jiji katika mstari.

Tangu Mkurugenzi Kihamia alipoteuliwa  amekuwa akisisitiza kufuatwa kwa kanuni, sheria, taratibu na miongozo na kuwachukulia hatua wale wote waliokwenda kinyume na utaratibu ikiwepo kurejeshwa posho zinazolipwa kinyume na taratibu kwa Madiwani wa Halmashauri ya Jiji la Arusha na kufuta posho zisizokuwa za lazima zilizokuwa zikilipwa kwa Maafisa mbalimbali wa Jiji.

 Pia anatoa rai kwa watumishi wa Jiji wenye tabia yakutoa nyaraka za Serikali kinyume na sheria na kusambazwa katika mitandao ya jamii waache tabia hiyo kwani kosa la jinai na atakayegundulika  atawajibika kwa mujibu wa sheria zilizopo. Ndugu Kihamia ameahidi kuwa kumchafua katika mitandao ya kijamii hakutapunguza dhamira yake ya kuwahudumia wananchi kwa weledi na uadilifu  kwa kutenda  haki bila kumwonea mtu yeyote.

Tangu alipofika Jiji la Arusha mwezi Julai 2016 Mkurugenzi hajawahi kuidhinisha mafuta, wala posho kwa ofisi ya Mkuu wa Wilaya, wala kwa Mkuu wa Mkoa ambazo hazikuhusiani na shughuli za Halmashauri ya Jiji la Arusha. 
Hivyo wananchi  wanaombwa kupuuza taarifa hizo kwani hazina ukweli wowote na zina lengo la kumchafua  Mkurugenzi huyu.

Frank R. Sanga
Afisa Tawala, Halmashauri ya  Jiji 
Arusha.
05 Oktoba 2016.

No comments: