Advertisements

Monday, October 17, 2016

Wanafunzi wasoma chini ya miembe

SHULE ya Msingi Kashifa, kata ya Ikola, iliyo mwambao mwa Ziwa Tanganyika katika Wilaya ya Tanganyika, mkoani Katavi, inakabiliwa na uhaba wa vyumba vya madarasa na kusababisha wanafunzi kusoma chini ya miti kwa zaidi ya miaka mitano.

Shule hiyo yenye zaidi ya wanafunzi 600 wanaosoma kuanzia darasa la kwanza hadi la saba ina vyumba viwili vya madarasa.

Akizungumza na gazeti hili, diwani wa Ikola, Philiomon Moro alikiri kuwa shule hiyo inakabiliwa na uhaba wa vyumba vya madarasa. Alisema vyumba vipo viwili hivyo walimu wanalazimika kufundisha wanafunzi wakiwa wameketi chini ya miembe.

“Shule hiyo haina uhaba wa madawati kwani tayari wazazi na walezi wakiwemo wadau wa maendeleo wamechangia madawati mapya lakini kutokana na uhaba wa vyumba vya madarasa madawati hayo yamehifadhiwa nje, shuleni hapo," amesema.

Baadhi ya wanafunzi wanaosoma shuleni hapo wamedai kuwa wanalazimika kusoma nje shule huku wakipigwa jua mchana kutwa hali inayosababisha wengi wao wasifike shuleni kusoma.

Mbunge wa Mpanda Vijijini, Moshi Kakoso, amekiri kuwepo kwa uhaba huo wa vyumba vya madarasa shuleni hapo na amewaasa madiwani kuwaelimisha wananchi ili waone umuhimu wa kujitolea kujenga miundombinu ya shule ikiwemo vyumba vya madarasa.

HABARI LEO

No comments: