Lema alikamatwa usiku wa kuamkia jana akiwa mkoani Dodoma, kuhudhuria vikao vya Bunge na kusafirishwa hadi Arusha.
Akizungumza jana na waandishi wa habari ofisini kwake Kamanda wa Polisi Mkoani Arusha, Charles Mkumbo, alisema Lema yuko mahabusu kwa mahojiano mpaka watakapomaliza na kumfikisha mahakamani, kujibu makosa anayokabiliwa nayo.
Mkumbo alisema Lema amekuwa akitoa maneno na lugha za uchochezi na kuzirudia kila mara, hivyo wameona vyema wamweke ndani kwa mahojiano.
“Juzi tulimkamata akitokea Dodoma na tulifanya naye mahojiano na kumwachia kwa dhamana, lakini kuna baadhi ya makosa hatukuwahi kumhoji, sasa ndio tumeamua kumhoji,” alisema.
Pamoja na Polisi kutosema ni lugha gani ya uchochezi imetumiwa na Mbunge huyo kiasi cha kuka matwa, Novemba Mosi mwaka huu Kamanda Mkumbo akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake, alitaja maneno ya uchochezi anayodaiwa kuyasema Lema.
Alisema kwamba Lema alitamka maneno haya: “Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akiendelea kukandamiza demokrasia na siasa za ukandamizaji, taifa litaingia katika umwagaji wa damu, nchi hii inaandaliwa kwenda katika utawala wa kidikteta”.
Wakati mbunge huyo anahojiwa na Polisi mjini Arusha, Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe akizungumza na waandishi wa habari mjini Dodoma, amelaani kukamatwa kwa mbunge huyo, akidai ni utekaji nyara.
Katika kesi inayomhusu Tundu Lissu, Hakimu Mkazi Mwandamizi, Thomas Simba wa Mahakama ya Kisutu alitoa hati ya kukamatwa kwa mbunge huyo wa Chadema kwa sababu amekiuka masharti ya dhamana katika kesi ya uchochezi, inayomkabili na wenzake watatu.
Baada ya Wakili wa Serikali, Patrick Mwita kudai kuwa kesi hiyo imekuja kwa ajili ya kutajwa, lakini mshtakiwa Lissu hajafika mahakamani na Mdhamini wa Lissu, Robert Katula kuieleza mahakama hiyo kuwa alipewa taarifa na Lissu kupewa ruhusa ya moja kwa moja na kwenda kwenye kesi nyingine Mwanza, Hakimu Simba alisema mshtakiwa ameondoka bila ya ruhusa ya Mahakama, hivyo anatoa hati ya kukamatwa na hakutakuwa na msamaha.
Aliwataka wadhamini wake wafike mahakamani hapo, kueleza mdhamana wao amekwenda kinyume na masharti ya dhamana. Hata hivyo, Wakili wa Utetezi, Faraja Mangula, alidai Lissu hajafika mahakamani kwa sababu amekwenda jijini Mwanza kwa ajili ya kusimamia kesi za Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana.
Hata hivyo, wakili Mwita aliiomba Mahakama imfutie dhamana mshtakiwa huyo kwa sababu amekwenda kinyume na masharti ya dhamana aliyopewa, pia amekuwa akirudia kosa hilo mara kwa mara. Kesi itatajwa tena Novemba 21, mwaka huu.
Mbali ya Lissu katika kesi hiyo, washtakiwa wengine katika kesi hiyo ambao dhamana yao bado inaendelea ni Mhariri wa gazeti la Mawio, Simon Mkina, Jabir Idrisa na Mchapishaji wa Kampuni ya Jamana, Ismail Mehboob.
Hivi karibuni Mahakama iliwaonya wadhamini wa Lissu, kutokana na kutotoa taarifa kama mshtakiwa huyo amekwenda nchini Ujerumani kwa ajili ya matibabu.
Katika kesi hiyo, inadaiwa Januari 12 hadi 14, mwaka huu, Dar es Salaam, Jabir, Mkina na Lissu, kwa pamoja waliandika na kuchapisha taarifa za uchochezi zenye kichwa cha habari kisemacho, ‘Machafuko yaja Zanzibar’ kwa lengo la kuleta chuki kwa wananchi wa Zanzibar na serikali yao.
Katika mashtaka mengine, Mehboob anadaiwa Januari 13, mwaka huu katika jengo la Jamana lililopo Ilala, Dar es Salaam, alichapisha gazeti la Mawio lililokuwa na taarifa za uchochezi, pia alichapisha gazeti hilo bila kuwasilisha hati ya kiapo kwa Msajili wa Magazeti.
Aidha, washtakiwa hao kwa pamoja wanadaiwa Januari 14, mwaka huu, Dar es Salaam, bila ya kuwa na mamlaka yoyote, waliwatisha na kuwatia hofu wananchi wa Zanzibar, wasiweze kushiriki kwenye kurudia Uchaguzi Mkuu.
HABARI LEO
No comments:
Post a Comment