Advertisements

Thursday, November 17, 2016

LEMA SASA AWAWEKA POLISI MATATANI

ASKARI wa Jeshi la Polisi na wenzao wa Jeshi la Magereza mkoani Arusha wameingia matatani baada ya Hakimu Mfawidhi, Agustino
Rwezile, kuwataka waache kuwasumbua waandishi wa habari na wananchi wengine wanaokwenda kusikiliza kesi mbalimbali mahakamani.
Zikiwamo zinazoendelea sasa za Mbunge wa Arusha mjini, Godbless Lema.
Aidha, Hakimu Mfawidhi huyo alisema atamuandikia barua Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani Arusha kumtaarifu juu ya suala hilo na pia Mkuu wa Jeshi la Magereza, lengo likiwa ni kuhakikisha kuwa waandishi wa habari na wananchi wengine wanaozingatia taratibu katika kufuatilia mwenendo wa kesi kwenye mahakama hiyo ya Hakimu Mkazi Arusha hawabughudhiwi kwa namna yoyote.
Hakimu mfawidhi Rwezile alitoa ufafanuzi huo wakati akielezea tukio lililojiri jana kwenye mahakama hiyo, wakati askari takribani sita wa Jeshi la Magereza walipozua kitimtim kwa kuwakimbiza waandishi Janeth Mushi wa gazeti la Mtanzania na Lilian Joel wa gazeti la Uhuru waliokuwa wakimpiga picha Lema, aliyekuwa akifikishwa mahakamani hapo kukabiliana na mashtaka yakiwamo ya uchochezi.
Katika tukio hilo lililowaacha watu kadhaa midomo wazi, askari hao wa Magereza, bila kujali kuwa baadhi yao walikuwa na silaha za moto, walionekana wakiwakimbiza kwa kasi waandishi wa habari ( Janeth na Lillian), ambao kwa bahati walinusurika baada ya kumfikia hakimu Hakimu Nestory Baro wa mahakama hiyo ambaye aliwaokoa baada ya kuwashika na kisha kuwataka askari waache kuidhalilisha; mahakama kwa vitendo vya aina hiyo.
Hali hiyo ilimlazimu Wakili anayemtetea Mbunge Lema, John Mallya, kumwomba Hakimu Mfawidhi Rwezile kutolea tamko suala hilo la unyanyasaji dhidi ya wanahabari unaofanywa na askari katika viunga vya mahakama hiyo.
Akizungumza mahakamani hapo, Hakimu Mfawidhi Rwezile alisema Mahakama haifanyi kazi kwa siri na kwamba, bila kujali mtu mwenye kesi mahakamani hapo ni kiongozi au la, waandishi wa habari na watu wengine wote wanaruhusiwa kuingia mahakamani hapo bila bughudha, alimradi wanafuata taratibu na hakuna sheria wanayoikiuka.
Alisema mara zote, mahakama kama mhimili mmojawapo, inalazimika kuhakikisha kuwa kila anayefika mahakamani hapo anaingia salama na pia kutoka akiwa salama. Kama mnaona kuna tatizo la kiusalama, utaratibu unajulikana na utawekwa kwa sababu hapa siyo Magereza wala Polisi, alisema na kuongeza: Watu wanakuja (mahakamani) kutafuta haki zao.
Hivyo hatutarajii kuona wala kusikia kama nilichoona leo wakiwafanyia waandishi wa habari. Nimeonya na sitarajii jambo hili lijirudie.;
Hakimu mfawidhi huyo alisisitiza kuwa hakuna mwananchi anayepaswa kubughudhiwa ikiwa atazingatia taratibu za kuwapo mahakamani ikiwamo kujiepusha na masuala ya siasa kwenye eneo hilo na kwamba, ikitokea jambo hilo la unyanyasaji dhidi ya waandishi wa habari na wananchi wengine likajirudia, wapeleke malalamiko kwa viongozi wa mahakama na suala hilo litashughulikiwa.
Aidha, Hakimu mfawidhi huyo aliwaomba radhi waandishi wa habari kwa tukio la kukimbizwa na askari wakiwa mahakamani hapo.
Alisema suala hilo halitaishia hapo kwa sababu ataandika barua kwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha na pia Mkuu wa Magereza kwa nia ya kuona kuwa suala hilo halijirudii tena.
Awali, Hakimu Baro wa mahakama hiyo alisema inasikitisha kuona kuwa baadhi ya askari wa Jeshi la Magereza na Polisi wakiwasumbua waandishi wa habari pindi wanapofika kwenye mahakama hiyo kufanya kazi zao, hasa wakati wa kesi zinazowahusu viongozi.
ILIVYOKUWA
Lema alifikishwa mahakamani majira ya saa 2:00 asubuhi. Wakati akiteremka kutoka kwenye gari la Magereza lililomfikisha hakamani hapo, waandishi waliokuwapo walijaribu kumpiga picha picha na ndipo askari walipowazuia na kuwaendea kwa kasi.
Kuona hivyo, waandishi hao wakaanza kukimbia huku wakipiga kelele za kuomba msaada. Askari hao sita wakaongeza kasi kuwafukuza, lakini hawakufanikiwa kuwatia mikononi baada ya waandishi kufanikiwa kumfikia Hakimu Baro, ambaye aliwashika na kuwakinga kabla ya kuanza kuwahoji askari hao sababu ya kuwakimbiza waandishi hao.
Hakimu huyo alisikika akisema kuwa kitendo cha askari hao kuwakimbiza waandishi wa habari kwenye eneo hilo la mahakama wakiwa na silaha siyo sahihi kwa sababu ni jambo linalodhalilisha mhimili huo mmojawapo wa dola.
Baada ya kuwaokoa waandishi hao kutoka kwenye hatari ya kuangukia mikononi mwa askari Magereza, Hakimu Baro aliwaongoza hadi kwa hakimu Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Rwezile ili wafikishe kilio chao kwake.
Wakizungumza na Nipashe, waandishi hao walisema wamesikitishwa na tukio hilo kufukuzwa na askari kama wezi kwa sababu tu ya kutekeleza wajibu wao kazini.
Walisema ni vizuri uongozi wa mahakama na pia wa jeshi la polisi na Magereza kuchukua hatua ya kuzuia unyanyasaji wowote dhidi ya waandishi wa habari pindi wanapokuwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha kutekeleza wajibu wao kwa sababu tatizo hilo limekuwa likijitokeza mara kwa mara.
Walisema kinachosikitisha zaidi, ni kwa baadhi ya askari wa Magereza na pia polisi kutotaka kutambua kibali maalumu cha mahakama kinachowaruhusu kufanya kazi zao mahakamani hapo.

CHANZO: NIPASHE

No comments: