Advertisements

Friday, November 11, 2016

MAHAKAMA YAMPA SIKU 7 PROFESA LIPUMBA NA MSAJILI WA VYAMA KUJIBU HOJA ZA CUF

Mahakama Kuu imewapa siku saba Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Jaji Francis Mutungi na Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba na wenzake kujibu madai ya chama hicho.

Msajili, Lipumba na wenzake walipewa muda huo jana na Jaji Sekieti Kihiyo kutokana na kesi ya madai iliyofunguliwa na Bodi ya Wadhamini wa CUF mahakamani hapo.

Katika kesi hiyo namba 23 ya mwaka 2016, bodi ya wadhamini CUF inaiomba mahakama itoe amri ya kubatilisha barua ya Msajili inayomtambua Profesa Lipumba kuwa ndiye mwenyekiti wa chama hicho.

Pia, wanaiomba mahakama itoe amri ya kumzuia Msajili kufanya kazi nje ya mipaka yake ya kisheria katika utekelezaji wa majukumu yake na pia itoe amri ya kumzuia Msajili kuingilia masuala ya kiutawala ndani ya chama hicho.

Mbali na Msajili na Profesa Lipumba, wadaiwa wengine katika kesi hiyo ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) na wanachama wengine tisa waliosimamishwa uanachama wa chama hicho, akiwamo Naibu Katibu Mkuu Bara ambaye pia ni Mbunge wa Kaliua (Tabora), Magdalena Sakaya.

Kesi hiyo ilitajwa jana mahakamani hapo kwa mara ya kwanza tangu ilipofunguliwa Oktoba 19, mwaka huu na mahakama ikataka wadaiwa kuwasilisha majibu ya madai hayo ya CUF, Novemba 17, mwaka huu.

Pia, Mahakama ilielekeza upande wa Maalim Seif kuwasilisha majibu ya hoja za wadaiwa Novemba 23 na ikapanga kesi hiyo itajwe tena Novemba 24, kwa ajili ya kuendelea na hatua nyingine.

Wadai katika kesi hiyo wanawakilishwa na mawakili Juma Nassoro na Halfani Daim wakati Msajili na Mwanasheria Mkuu wa Serikali wanawakilishwa na Wakili wa Serikali Mkuu (PSA), Obadia Kameya na Lipumba na wenzake wakiwakilishwa na Mashaka Ngole.

Katika hati ya Kiapo kinachounga mkono maombi hayo, Maalim Seif anadai kuwa Msajili wa Vyama vya Siasa hana mamlaka ya kuingilia utendaji wa ndani wa Vyama vya Siasa.

Anadai kuwa Sheria ya Vyama vya Siasa na Katiba ya nchi haimpi mamlaka Msajili wa Vyama vya Siasa kuwa chombo cha rufaa wala kurejea mambo ya utawala ndani ya chama cha siasa.

Badala yake anadai mamlaka hayo yako kwa vyombo vya juu vya chama na Mahakama na kwamba jukumu la Msajili ni kusajili vyama na kuweka kumbukumbu za vyama hivyo.

CUF kimekuwa na mgogoro wa kiuongozi baada ya Profesa Lipumba kuandika barua ya kutengua uamuzi wake wa awali wa kujiuzulu ambao Msajili alikubaliana naye na alikiandikia barua chama kuendelea kumtambua mwenyekiti huyo. Hata hivyo, CUF ilimfukuza uanachama Lipumba.

No comments: