Advertisements

Tuesday, November 22, 2016

MAJAMBAZI DAR WAENDELEA KUANGUKIA MIKONONI MWA POLISI HUKU POMBE FEKI NA MITAMBO YAKE PIA VIKIKAMATWA.

Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam imeendesha operesheni katika maeneo mbalimbali ya jiji hilo na kuwakamata watuhumiwa 67 wakiwemo watano waliokutwa wakiuza na kusambaza pombe bandia aina ya konyagi na vifaa vya kutengeneza kinywaji hicho.

Akizunguma jana jijini Dar es Salaam, Kamanda wa Polisi wa kanda hiyo, Kamishna wa Polisi, Simon Sirro alisema watuhumiwa hao pia walikamatwa wakiwa na chupa tupu za konyagi 175, chupa zenye kinywaji cha konyagi 17 na vifungashio vya viroba vya konyagi 111.

Aidha, alisema watuhumiwa hao walikamatwa wakiwa na vifuniko vya chupa za konyagi 200, lebo na stika za konyagi, katoni 111 za viroba vya konyagi, vimiminika vya pombe aina ya spiriti lita 20, ndoo kubwa aina ya jaba moja na koki 10, viroba original pakiti 14,916 na Victorious pakiti 1,080.

Aliwataja watuhumiwa waliokamatwa na bidhaa hizo bandia kuwa ni Ladness Kagaruki (26), mkazi wa Sinza madukani, Aloyce Emmanuel (53), mkazi wa Salasala, Leonard Arobogasti (49), mkazi wa Makongo, Godfrey Gabriel (29) na Eveline Sandole (58) wakazi wa Mwenge.


Kamanda Sirro alisema watuhumiwa wote wanaendelea kuhojiwa na upelelezi utakapokamilika watafikishwa mahakamani kujibu mashtaka yanayowakabili, huku akieleza kuwa kwa suala la shisha, tayari watuhumiwa watatu wanashikiliwa na upelelezi wao utakapokamilika watafikishwa mahakamani.

Katika tukio lingine, wanamshikilia Kulwa Rajabu anayetuhumiwa kwa ujambazi akiwa na silaha aina ya Browning yenye namba A731441 yenye risasi 12 ndani ya magazine.

Alisema mtuhumiwa huyo alikamatwa Novemba 16, mwaka huu saa 10.00 jioni Mbande Mbagala baada ya kuwekewa mtego. Alisema silaha hiyo iliibiwa Novemba 13, saa 9.30 usiku maeneo ya Tuangoma katika tukio la uvunjaji na kuibwa kwa vifaa mbalimbali ambavyo vyote vilipatikana.

Aidha, alisema baada ya mahojiano ya kina mtuhumiwa huyo alitaja silaha nyingine ambayo ni bastola aina ya Revolver iliyofutwa namba ikiwa na risasi mbili ikiwa imefichwa maeneo ya msitu wa Dona huko Yombo.

Pia wamemkamata mtuhumiwa anayetambulika kwa jina moja la Shomari aliyekuwa akituhumiwa kwa mauaji yaliyofanyika kwenye daladala Oktoba 28, mwaka huu Tandika Tambuka.

Kwa mujibu wa Sirro, baada ya Polisi kupata taarifa na kumfuatilia, mtuhumiwa huyo alianza kukimbia na ndipo askari walifyatua risasi juu ili asimame, lakini hakutii amri na askari walimpiga risasi mbili mguuni na kudondoka chini kisha kumkamata pamoja na bastola yake aina ya Revolver ikiwa na risasi mbili ndani ya magazine.

No comments: