Advertisements

Sunday, November 6, 2016

Mkataba kusaka walioficha mabilioni Uswisi wasainiwa

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk Augustine Mahiga
HUKU kukiwepo na dhana ya kuwa kuna Watanzania wanaotorosha fedha na kuzificha katika mataifa mbalimbali ikiwemo Uswisi, hatua moja muhimu imefanyika katika kukabili suala hilo, baada ya serikali ya nchi hizo mbili, kusaini mkataba muhimu.

HabariLeo Jumapili imebaini kufikiwa kwa makubaliano ya ushirikiano muhimu wa kisheria kwenye masuala ya jinai, unaolenga kuwajengea uwezo makachero wa Tanzania, kuchunguza masuala mbalimbali ya kiuhalifu nchini Uswisi.

Mkataba huo umeenda mbali zaidi, kwa kuweka wazi kuwa kuanzia sasa makachero hao, wanaweza kuchunguza fedha za Watanzania zilizohifadhiwa nchini Uswisi, tofauti na awali ambapo sheria za nchi hiyo zilikuwa zinazuia.

Mkataba huo umesainiwa hivi karibuni wakati wa Maadhimisho ya miaka 50 ya ushirikiano kati ya Tanzania na Uswisi. Uswisi ni nchi inayosifiwa kuwa na huduma bora za kibenki huku ikiwa na sheria kali zinazowalinda wateja wake.

Mkataba wa makubaliano hayo, ambao umeleta mwanga katika kukabiliana na usiri wa fedha hizo, ulisainiwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk Augustine Mahiga na Balozi wa Uswisi nchini, Florence Mattli.

Akizungumza na gazeti katika mahojiano maalumu kuhusu mkataba huo, Balozi Mahiga alisema kuwa katika kuendeleza ushirikiano mzuri baina ya nchi hizo, Tanzania itanufaika na ruhusa hiyo ya kufuatilia akaunti za fedha Uswisi.

Alisema kuwa kipengele hicho, kimekubaliwa kwenye makubaliano na kwa sasa hakuna tena kikwazo kitakachoizuia Tanzania kuchunguza akaunti hizo.

Alisema kuwa hatua hiyo inatokana na Serikali ya Uswisi pia kuridhishwa na namna ambavyo Tanzania imekuwa ikipambana na vitendo vya rushwa na ufisadi, kwa lengo la kuwaletea maendeleo wananchi wake chini ya uongozi wa Rais John Magufuli.

Alisema, Uswisi imekuwa ni rafiki mkubwa wa Tanzania tangu enzi na enzi huku ikiisaidia katika uboreshaji wa sekta mbalimbali.

“Kweli hiyo ni hatua nzuri kwa Tanzania hasa kwa kipindi hiki ambapo Serikali ya Awamu ya Tano imekuwa ikikabiliana na rushwa na kila aina ya ufisadi na kwa hiyo ruhusa hii itasaidia kulinda fedha zetu kutoroshwa,” alisema Balozi Mahiga.

Akijibu swali ni lini serikali itakuwa tayari kupeleka makachero nchini humo, kuchunguza madai ya kuwepo kwa Watanzania walioficha fedha kwenye benki za nchini humo, Balozi Mahiga alisema; “Siwezi kusema ni lini hatua hiyo inaweza kuanza kuchukuliwa kwa kuwa zipo mamlaka zinazohusika na utekelezaji wake, ila ninachoweza kusema ni kuwa hatua iliyofikiwa ni ya msingi kwetu kama nchi.”

Zitto apongeza Mkataba Akitoa maoni yake kuhusu makubaliano hayo, Mbunge wa Kigoma Mjini, Kabwe Zitto (ACT – Wazalendo ), mmoja wa wabunge ambaye amekuwa akilizungumzia suala la ufichwaji wa mabilioni ya fedha nje ya nchi, aliliambia gazeti hili kuwa kipengele hicho kwenye mkataba huo ni kizuri na kitasaidia kupatikana kwa fedha zilizofichwa katika benki za Uswisi.

Alitumia nafasi hiyo kuipongeza serikali kwa uamuzi huo uliofikiwa na kusema ni hatua ya kimafanikio, hasa ikizingatiwa kuwa fedha hizo zinatokana na nguvu za wanyonge, ambapo pia zilipatikana kinyume na sheria. Balozi Mattli, alisema kuwa ushirikiano kati ya Tanzania na Uswisi, umekuwa ukiimarika zaidi kila siku, na kuwa nchi hiyo itaendelea kuisaidia Tanzania kwa hali na mali.

HABARI LEO

No comments: