NGUZO 101 za umeme zimeteketezwa na kusababisha hasara ya Sh. milioni 121, kutokana na kuwapo kwa vitendo vya uchomaji moto ovyo, vinavyofanywa na baadhi ya wananchi, katika maeneo mbalimbali mkoani Kagera.
Ofisa Mazingira wa Mkoa wa kagera, Haji Kiselu, alisema jana kuwa nguzo zote hizo zimechomwa moto mwaka huu.
Alisema uchomaji huo wa moto unatokana na kutosimamiwa vyema kwa sheria ya mazingira namba 20 ya mwaka 2004, ambayo inaelekeza uundwaji wa kamati kuanzia ngazi za vijiji, kata hadi wilaya na pia kuhakikisha sheria ndogo za halmashauri zinatungwa na kusimamiwa.
Kiselu alizitaja changamoto mbalimbali wanazokabiliana nazo katika udhibiti wa uchomaji moto ovyo kuwa ni pamoja na kutosimamiwa vyema kwa sheria ya mazingira, kutosimamiwa utekelezaji wa mpango bora wa matumizi ya ardhi na kushindwa kudhibiti vitendo vya ukataji kuni.
Zingine ni upasuaji mbao, uanzishwaji wa mashamba katika hifadhi na uchomaji wa mkaa na kuwa vitendo vya uchomaji moto hufanyika nyakati za usiku, hivyo ni vigumu kuwatambua wahusika.
No comments:
Post a Comment