Advertisements

Friday, November 4, 2016

Serikali yasikiliza sauti ya wadau wa habari

Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Nape Nnauye
SERIKALI imewasilisha bungeni kwa mara ya pili Muswada wa Huduma za Habari wa mwaka 2016 ukiwa na mabadiliko katika maeneo saba, ikiwemo kuviondolea vyombo vya habari adhabu kwa baadhi ya makosa ya mwandishi na ukamataji wa mitambo na vifaa vya wanahabari.

Aidha, Serikali imewatoa hofu waandishi kuhusu muswada huo na kusema ikiwa waandishi wa habari watasimamia maadili yao na kutii sheria, hawana haja ya kuhofu kwani Serikali itakuwa mlinzi wao namba moja.

Muswada huo ukiwa na maboresho, uliwasilishwa jana na Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Nape Nnauye.

Wakati Serikali ikieleza hayo, taaarifa rasmi ya Kambi Rasmi ya Upinzani bungeni ikitolewa na Msemaji wa kambi hiyo, Joseph Mbilinyi, alishauri Waziri mwenye dhamana ya habari asiachiwe mamlaka ya kuweka viwango vya elimu katika kanuni bali Bodi ya Ithibati na Baraza Huru la Habari likaweka viwango hivyo. Ilipendekeza kiwango kiwe diploma.

Kambi hiyo ilitaka Bodi ya Ithibati isiishie kwa waandishi wa habari, bali pia iwe na mamlaka ya ithibati kwa elimu inayotolewa na vyuo mbalimbali vya uandishi wa habari nchini. Mbilinyi alipendekeza kuwepo kifungu mahususi cha kuwalinda wanahabari dhidi ya vitendo viovu vinavyoweza kufanywa dhidi yao .

Hata hivyo, kambi hiyo ya upinzani iliunga mkono kuanzishwa kwa Bodi ya Ithibati pamoja na Baraza Huru la Habari ili kuwe na viwango na uangalizi pamoja na uratibu wa kitaaluma katika tasnia ya habari pamoja na kuwakatia bima waandishi wa habari.

Aidha, Kamati ya Huduma na Maendeleo ya Jamii kuhusu muswada huo, imependekeza pamoja na uvaaji wa vitambulisho kwa waandishi wa habari, kanuni zieleze kuhusu mavazi kama ilivyo kwa wanasheria, madaktari na wauguzi. Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Peter Serukamba, ndiye aliyetoa maoni ya kamati hiyo bungeni jana.

Maboresho saba

Nape alisema walifanya maboresho kwa kuzingatia mawazo ya wadau, ikiwemo Kamati ya Bunge, taasisi za habari kama Jukwaa la Wahariri (TEF), Baraza la Habari (MCT), Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake (Tamwa), Taasisi ya Wanahabari Kusini mwa Afrika, Tanzania (MISA-TAN) na Umoja wa Wamiliki wa Vyombo vya Habari (MOAT).

Maboresho hayo ni katika eneo la kuainisha haki na wajibu wa wanahabari; kuainisha haki ya chombo cha habari kukata rufaa; uwakilishi wa wanahabari katika Bodi ya Ithibati; Jaji Mkuu kuweka utaratibu kusikiliza haraka kesi za kashfa.

Maeneo mengine ni kuviondolea vyombo vya habari adhabu kwa baadhi ya makosa ya mwandishi; vyombo vya dola kukamata mitambo na vifaa vya wanahabari na mitambo kutohusika moja kwa moja kwa kosa la gazeti.

Nape alisema katika uwakilishi wa Bodi ya Ithibati, kati ya wajumbe saba, wakiwemo wanne waandishi, sasa kutakuwa na uwiano katika sekta binafsi na ya umma. Awali hakukuwa na uwiano huo.

“Moja ya mageuzi makubwa ya muswada ni kuviondolea vyombo vya habari au umiliki wake adhabu ya makosa yanayomhusu mwandishi binafsi. Sasa mwandishi kama mwanataaluma kamili anaweza kuwajibishwa na Bodi ya Ithibati kwa makosa ya kimaadili badala ya mtindo wa sasa wa kila kosa la mwandishi kubebwa na chombo chake,” alisema Nape.

Kuhusu kukamata mitambo, Nape alisema maoni ya wadau yamezingatiwa na sasa maboresho yamemuondoa Mkurugenzi wa Idara ya Habari kuwa na mamlaka ya kukamata mitambo badala yake kazi hiyo itafanywa na Polisi kwa mujibu wa Sheria ya Makosa ya Jinai (CPA).

Aidha, Nape alisema kuhusu mitambo ya uchapishaji kuwa sehemu ya makosa chombo cha habari kinapoandika uchochezi au makosa mengine ya kashfa, wachapaji wameondolewa katika makosa yanayotokana na maudhui ya watu wengine.

HABARI LEO

No comments: