ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, November 26, 2016

Wakurugenzi Na Mameneja ATCL Wapanguliwa

Bodi  ya Wakurugenzi ya Shirika la Ndege nchini (ATCL) imewaondoa katika nyadhifa zao wakurugenzi wote waliopo katika menejimenti na baadhi ya mameneja, baada ya kubainika kuwa na kasoro za kiutendaji na kielimu.

Uamuzi huo, ambao hautamhusisha  Mkurugenzi Mkuu wa Shirika hilo, Ladislaus Matindi, ulitolewa katika kikao kilichofanyika Novemba 18, lengo likiwa ni kuboresha muundo wa ATCL, ili kukidhi matakwa ya muda mfupi wakati muundo wa kudumu ukiandaliwa.

Akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi za Makao Makuu ya shirika hilo, Mwenyekiti wa Bodi ya ATCL, Mhandisi Emmanuel Korosso, alisema katika kikao hicho bodi iliamua kuwaengua wakurugenzi watano waliokuwa katika idara mbalimbali, ikiwamo ya biashara, ambayo ilikuwa na kaimu.

Mhandisi Korroso alitaja idara nyingine ambazo wakurugenzi wameondolewa  kuwa ni fedha, usalama, ufundi na uendeshaji, ambayo mkurugenzi wake alikuwa anaelekea kustaafu.

“Kwakuwa wakurugenzi wengi walikuwa wanakaimu  nafasi hizo, tumeamua wakurugenzi wanaokaimu warudishwe katika nafasi zao  za chini, ambazo si menejimenti au wahamishiwe katika vituo vya mikoani,” alisema Mhadishi Korosso.

Alisema bodi pia imeagiza  kuondolewa kabisa katika shirika hilo wakurugenzi na mameneja waliothibitishwa ili waweze kupangiwa majukumu mengine yatakayoendana na sifa walizonazo.

Alisema kikao hicho pia kimemuagiza Mtendaji Mkuu kutangaza mara moja nafasi za wakurugenzi na mameneja zilizo wazi kwa kufuata muundo uliopitishwa.

Mbali na hilo, Mhandisi Korosso alisema kwa sasa shirika hilo limeweza kuongeza nidhamu katika mapato na matumizi, jambo ambalo limechangia kuanza kulipa baadhi ya madeni wakati Serikali ikisubiri uhakiki umalizike ili iweze kuyachukua.

“Tumeweza kudhibiti mapato na matumizi vizuri, kumekuwa na ongezeko la mapato ya uzito wa ziada wa mizigo kutokana na usimamizi mzuri, ukusanyaji wa mapato kutoka vituoni na mawakala umeboreshwa sana kutokana na ufuatiliaji wa karibu wa mauzo,” alisema Mhandisi Korosso.

Aliongeza kuwa, bodi pia imetoa ruhusa kwa wafanyakazi na familia zao kupewa tiketi bure mara moja kwa mwaka kama stahiki ya likizo na tiketi yenye punguzo mara moja kwa mwaka.

Kampuni ya ATCL, ambayo awali ilikuwa haina ndege hata moja, ilianza kufanya  kazi za safari za ndege Oktoba 14, mwaka huu, baada ya Serikali kununua ndege mbili mpya aina ya Bombardier Q400.

No comments: