Advertisements

Thursday, November 3, 2016

Walichosema ACT kuhusu ahadi za Rais Magufuli katika uchaguzi wa mwaka jana

Na Regina Mkonde
Chama cha ACT-Wazalendo kimemkumbusha Rais John Magufuli kutekeleza ahadi yake aliyoitoa katika kipindi cha kampeni za uchaguzi mkuu wa mwaka jana, kuwa serikali yake haitaruhusu mwanafunzi atakayefaulu kwenda chuo kikuu ambaye atashindwa kujiunga na elimu hiyo kwa kukosa ada ama mkopo.

Katibu wa Itikadi, Mawasiliano na Uenezi wa ACT, Ado Shaibu leo amesema chama hicho kimetoa tamko hilo, baada ya takwimu zilizotolewa hivi karibuni na Bodi ya Mikopo kwa Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HELSB) kuthibitisha kuwa takribani wanafunzi 65,000 wenye sifa za kujiunga na elimu ya juu, wanafunzi 20,000 ndiyo waliopata mikopo.

“Kwenye mikutano yake ya kampeni Rais Magufuli alitamba kuwa serikali yake hakuna mwanafunzi ambaye atafaulu kwenda chuo kikuu ambaye atashindwa kujiunga na elimu hiyo kwa kukosa mkopo. tunamtaka kutekeleza ahadi yake kwa vitendo.”

Ameongeza kuwa “Kwenye mikoa mingi iliyotembelewa viongozi wa chama wamepinga vikali utaratibu wa sasa wa utoaji mikopo wa elimu ya juu ambao kama ukiachwa bila kupingwa utafanya watoto wengi kutoka familia masikini washindwe kujiunga na elimu ya juu kwa kukosa mikopo,”

Shaibu amedai kuwa, kisingizio kinachotolewa na serikali cha kutilia mkazo kwenye kozi za kipaumbele hakistahili kutumiwa kwa kuwa ni kigezo cha kuwanyima watoto wa masikini haki ya kujiunga na elimu ya juu.

“Katika ilani ya ACT ya mwaka 2015 suluhisho la mikopo ya elimu ya juu limepambanuliwa vyema. kifungu 5.4.2 (v)(d) ya ilani yetu inapendekeza kuanzishwa kwa utaratibu wa scholarship kwa kozi za kipaumbele ili mkopo utumike kusomesha wanafunzi wengi zaidi wa kozi zinazosalia,” amesema.



No comments: