Dar es Salaam. Wakati Serikali ikifanya jitihada kulifanya Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) kushindana na kampuni binafsi, biashara ya usafiri wa anga nchini inazidi kuporomoka, ikiathiri kampuni, ajira na kipato cha huduma zinazoambatana na usafiri huo.
Wakati Air Tanzania ikiandaa wafanyakazi wapya kwa ajili ya kuhudumia ndani ya ndege mbili aina ya Bombadier zilizonunuliwa hivi karibuni, kampuni pinzani za Precision Air na Fast Jet zinapunguza wafanyakazi na safari ili kukabiliana na kuporomoka huko kwa biashara ya usafiri wa anga.
Hayo yanatokea wakati kukiwa na malalamiko ya hali ya uchumi kuwa ngumu, ikihusishwa na hatua mbalimbali ambazo Serikali ya Awamu ya Tano imekuwa ikichukua kurekebisha uchumi.
Hatua hizo za Serikali zimesababisha kudorora kwa mzunguko wa fedha na kuathiri kipato cha wananchi wengi.
Wakati biashara ya anga ya ndani ilikuwa ikitegemea safari za wafanyakazi wa umma, Serikali imedhibiti safari hizo, huku wafanyabiashara wakijifunga mikanda kutokana na hatua hizo za Serikali kugusa huduma zao.
Fastjet na Precision Air, kampuni zilizoshika soko wakati Air Tanzania ilipoporomoka kibiashara, sasa zinapunguza safari zake, huku uahirishaji wa safari ukizidi kusumbua abiria.
“Sina uhakika huenda vipato vya watu wanaotumia usafiri huu vimepungua,” alisema mjumbe mmoja wa Bodi ya Wakurugenzi ya ATCL.
“Biashara ya ndege ina ushindani na huduma zikiwa nzuri ndipo unapata wateja wengi. Kusafiri ni sehemu ya utalii, kwa hiyo ni utashi wa mtu kuamua apande ndege ipi ili afike salama na kufurahia safari.”
Alisema ndege nyingi zimetengenezwa kwa ajili ya abiria na sehemu kubwa ya gharama zake katika uendeshaji ni mafuta, hivyo abiria wakiwa wachache hawawezi kuruka.
Alisema ingawa ndege zinatofautiana, kuna zinazobeba abiria 30 huku nyingine zikiwa zaidi, hivyo inapotokea abiria hawajatimia inakuwa vigumu kuruka.
“Labda abiria wa ndege wameamua kutumia usafiri wa barabara na majini kwa sababu hali ya kipato inachangia hivyo ni uamuzi wa mtu,” alisema mjumbe huyo.
Fastjet, ambayo ilikamata soko hilo kutokana na mpango wake wa kutoza nauli nafuu kulingana na muda wa kulipa tiketi, ilianza mwaka 2012 kwa malengo ya kusafirisha wateja 350,000 na kuuza tiketi 1,000,000, ikiwa na ndege tatu.
Kwa mujibu wa ripoti ya mwisho wa mwaka 2015, Fastjet ilisafirisha abiria 775,000, ikiwa ni ongezeko la asilimia 30 lakini hali ilibadilika nusu ya pili ya mwaka idadi ya abiria ilipungua kutokana na sababu mbalimbali ikiwamo hali ya kiuchumi na sababu kubwa ikitajwa kuwa ni kushuka kwa thamani ya shilingi dhidi ya dola ya Marekani.
Hata hivyo, ripoti hiyo inabainisha mazingira magumu ya kiabishara kwa kupata hasara ya dola 21.9 za Marekani (Sh47.7 bilioni) ikiwa ni nafuu kutoka hasara ya Dola 72.1 (Sh157 bilioni) mwaka 2014.
Mabadiliko hayo yaliendelea kuiathiri kampuni hiyo na hadi kufikia mwaka huu yalizidi kujitokeza baada ya kutangaza kupunguza wafanyakazi wake ili kujiimarisha kiuchumi.
Mchakato huo ulifanyika Septemba 8 na ulianza kwa marubani 14 ambao walikuwa wanafanya kazi katika ndege za Airbus zilizoondolewa na kampuni hiyo.
Hatua hiyo ilifikiwa baada ya kutoa ndege za Airbus na kuiacha moja kisha kuingiza nyingine aina Embrear E 190 inayoweza kubeba abiria 96 ambayo ilikodishwa kutoka Shirika la Ndege la Bulgaria.
Hata hivyo, hali ilizidi kuwa tete katika uendeshaji wake baada ya abiria wengi kulalamikia safari kukwama, huku wengine wakilazimika kusafiri tofauti na muda uliopangwa. Hali imesababisha shirika hilo kusitisha safari zake za Nairobi, Kenya na Entebbe, Uganda ambazo zilianza miaka ya karibuni.
Precision Air ilishika usafiri wa anga kwa kuanza kushindana na Air Tanzania na baadaye kukamata soko, lakini imekuwa ikiporomoka katika miaka ya karibuni na sasa inaonekana kuzidiwa, ikiwa imesaliwa na ndege moja.
Ripoti iliyotolewa hivi karibuni katika mkutano mkuu wa mwaka wa wanahisa uliofanyika 29 Agosti, inasema matokeo ya mwaka huu yamechagizwa na shirika kuwa na idadi ndogo ya ndege kwa ajili ya shughuli zake.
Inasema hali hiyo ilisababishwa na injini 13 kuwa katika matengenezo makubwa, kushuka kwa thamani ya shilingi, bei za mafuta zisizotabirika pamoja hali tete ya usalama katika ukanda wa Afrika Mashariki.
Hayo yalisababisha kampuni hiyo kupata hasara kabla ya kodi ya Sh91.6 bilioni, ikiwa ni ongezeko la asilimia 12 ikilinganishwa na hasara ya mwaka jana ya Sh83 bilioni ikiwa ni ongezeko la asilimia 14 ikilinganishwa na mwaka wa fedha 2013-14.
Hata hivyo, hivi karibuni Meneja Uratibu na Uhusiano wa Precision Air, Hillary Mremi alikaririwa akisema kuwa hali ya kudorora kwa biashara hiyo haitokani na sera za Serikali ya Awamu ya Tano.
Mremi alisema biashara hiyo si rahisi kutokana na gharama za uendeshaji kuwa kubwa duniani kote.
“Faida ya biashara ya usafirishaji wa ndege ni ndogo. Hivyo ukicheza nayo, inaathiri mpaka mtaji wako. Unaweza kuona namna gani ilivyo hatari, ukikosea kidogo itakugharimu zaidi, hivyo ni ngumu na hapa nchini biashara hii ni ngumu,” alisema Mremi.
Alisema kutokana na hoja hiyo, kwa kiasi kikubwa wanaathiriwa na kodi nyingi pamoja na tabia ya watu kujijengea tabia kuwa usafiri huu wa anga ni kifahari.
Alisema hatua ya Rais Magufuli kubana matumizi na kupunguza safari za viongozi wa Serikali haijawaathiri kibiashara kwani wameongeza idadi ya wasafiri.
Alifafanua kwamba hawezi kusema moja kwa moja kwamba biashara imeshuka kipindi hiki au cha Serikali ya Awamu ya Nne kwa sababu kitakwimu idadi ya abiria wao bado ipo vilevile.
Hivi karibuni, Precision Air ilianza safari zake kutoka Dar es Salaam na Zanzibar kwenda Hifadhi ya Serengeti, wakati Septemba ilirejesha safari za kwenda Hahaya nchini Comoro.
Yaja na ndege za bei nafuu
Wakati hayo yakitokea, Air Tanzania imejiimarisha ili kupambana kibiashara na mashirika hayo binafsi baada ya kununua ndege mbili aina ya Bombardier Q400.
Tayari imeshatangaza safari za Dar-Mwanza, Dar-Kigoma, Dar-Kilimanjaro na inatarajiwa kurejesha safari zake za Mbeya na maeneo mengine.
Air Tanzania itakuwa na uwezo wa kupambana na kampuni hizo binafsi katika suala la mizigo. Shirika hilo la Serikali halitozi mzigo wa kilo 21 kushuka chini, wakati Fastjet inaruhusu mzigo wa mkononi tu.
Abiria kukwama
Miongoni mwa watu waliokwama uwanja wa ndege baada ya Fastjet kuahirisha safari zake ni Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Harrison Mwakyembe.
Tukio hilo lilitokea Novemba 26 katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) wakati Dk Mwakyembe na abiria wengine wakitaka kuelekea Songwe.
“Nilikuwa na shughuli nyingi mkoani Songwe lakini imenibidi niahirishe baada ya ndege kushindwa kuondoka,” alisema Dk Mwakyembe ambaye ni Mbunge wa Kyela.
Hata hivyo, Dk Mwakyembe alisema sheria za mawasiliano nchini zinaitaka kampuni hiyo kutoa huduma za chakula na malazi endapo itachelewa zaidi ya saa nane.
Hii siyo mara ya kwanza kwa abiria wa kampuni hiyo kukwama uwanjani na wakati mwingine kujikuta wakilazimika kurudi nyumbani baada ya safari za ndege hiyo kuahirishwa.
Wasomi wanena
Wasomi walikuwa na maoni tofauti kuhusu kuyumba kwa biashara hiyo. Mhadhiri wa Shule ya Biashara ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Mutahyoba Baisi alisema hali hiyo inatokana na hali ya uchumi kwa sababu uendeshaji wa mashirika ya ndege ni gharama kubwa.
“Kuna wakati usafiri wa ndege ulikuwa wa kawaida. Lakini sasa hivi si kawaida kutokana na hali halisi ya maisha,” alisema.
“Ninahisi hata mfumo wa Serikali kudhibiti safari huenda unachangia baadhi ya ndege kupunguza safari mbalimbali zikiwamo za ndani.”
Alisema sasa ni nadra watumishi kusafiri mara kwa mara tofauti na hapo awali walivyokuwa wakisafiri kwa kutumia ndege.
Alisisitiza kuwa uendeshaji wa ndege ni gharama kubwa hivyo kila kampuni inayofanya shughuli hizo inalenga pia kupata faida na si hasara.
Mawakala wa safari za ndege
Mmoja wa mawakala wa usafiri wa ndege alilalamikia kupungua kwa abiria, akihusisha na uamuzi wa Serikali kufuta safari za watumishi wa umma.
Wakala huyo, Adrian Mwakalinga alisema biashara yao ilitegemea watu kutoka serikalini, ambao walikuwa wakisafiri kwa makundi, lakini wamekwama kutokana na Rais Magufuli kuzuia safari za nje na sasa wanasafiri kwa vibali.
“Kwa sasa hali ni mbaya. Kwa siku tulikuwa tunaweza kupata abiria hadi 10, lakini sasa unashinda siku nzima na kumbulia watu wawili lakini wakati mwingine si ajabu ukakosa kabisa,” alisema.
Hata hivyo, wakala huyo alisema changamoto nyingine wanayokutana nayo sasa ni teknolojia ya kununulia tiketi.
“Sasa teknolojia imerahisisha sana. Mtu anaweza kukaa nyumbani kwake na kubook mpaka akalipia kwa simu yake ya mkononi hivyo haimlazimu tena kufika ofisi za mawakala,” alisema.
Dereva teksi wabaki na vilio
Mmoja wa madereva teksi, Khalfan Mohamed alisema kutokana na hali ya uchumi, idadi ya abiria wanaokwenda uwanja wa ndege kwa ajili ya safari imepungua.
“Tangu mwaka huu uanze hali imekuwa mbaya, hasa kwa madereva wa teksi. Zamani kipindi kama hiki cha kuelekea sikukuu za mwisho wa mwaka, nilikuwa nafululiza kupeleka abiria uwanja wa ndege. Lakini sasa kwa wiki napata abiria mmoja hadi wawili, tena kwa manati.”Alisema zamani si viongozi wa Serikali pekee waliokuwa wateja wao, bali hata watu wa kawaida ambao walikuwa wanasafiri kwa shughuli mbalimbali, ikiwamo kusalimia ndugu jamaa na marafiki.
“Nadhani kipato kimeshuka na baadhi waliokuwa wakitumia usafiri wa ndege sasa wamerudi Ubungo (kituo cha mabasi ya mikoani). Maana huku ndiko kuna unafuu kuliko kupanda ndege wakati hali yako ya uchumi hairuhusu,” alisema.
Kampuni bora za ndege
Kampuni bora 10 katika usafiri wa anga mwaka 2016 ambazo zilipigiwa kura kulingana na takwimu na huduma za mwaka 2015 kutoka kwa wateja mbalimbali, kampuni hizo ni
1.Emirates: Ndege ya Dubai imefanikiwa kuajiri wafanyakazi zaidi ya 56,725 na kufanya safari 3,600 kwa wiki katika mabara sita duniani.
2. Qatar Airways: Kampuni bora ya ‘business class’ na ilishinda kama ndege bora Mashariki ya Kati katika kutoa huduma.
3. Singapore Airlines: Ni ndege bora kwa Bara la Asia na ilitajwa kuwa na siti zenye ubora katika bussiness class
4. Cathay Pacific: Kampuni iliyojikita China. Ina huduma bora iliyofanya kuwa ya kwanza kwa daraja la kwanza.
5. Ana All Nippon Airways: Pamoja na huduma zake, ni ndege bora kwa Bara la Asia.
6. Etihad Airways: Ilifanikiwa kupata tuzo muhimu ya kuwa ndege inayotoa sehemu nzuri kwa ajili ya chakula.
7. Turkish Airlines: Ni ndege bora katika Bara la Ulaya iliyojikita Istanbul.
8. Eva Air: Imeshangaza wengi kutokana na upya wake katika biashara ya ndege na kushika nafasi ya nane ikitokea Taiwan. Inafanya vizuri katika bussiness class.
9. Qantas Airways: Ni shirika linaloongoza Austria katika ushindani wa ndege na limekuwa katika 10 bora kwa miaka minne mfululizo.
10. Lufthansa: Hili ni shirika bora katika Magharibi ya Ulaya na limeshika mara tano nafasi ya ndege bora kwa safari za Atlantic.
No comments:
Post a Comment