Dar/Arusha. Viongozi wa Ukawa, Edward Lowassa wa Chadema na Maalim Seif Sharif Hamad wa CUF wamekwenda kumjulia hali Mwenyekiti wa NCCR–Mageuzi, James Mbatia baada ya kutoka kwenye matibabu nchini India, ambako alifanyiwa upasuaji wa mguu.
Mbatia, ambaye pia ni Mbunge wa Vunjo, alifanyiwa upasuaji huo Novemba 14 katika Hospitali ya Zydus Ahmedabad Gujarat baada ya mguu huo kumsumbua kwa takribani miaka 37.
Akiwa nyumbani kwa Mbatia Mbezi Beach, Lowassa amesema, “Nimekuja kumuona mheshimiwa (Mbatia). Nimefurahi zaidi baada ya kunieleza anaendelea vizuri. Watanzania waendelee kumuombea na siku zijazo atazidi kupata nafuu zaidi.”
Maalim Seif alimpa pole na kusema, “Binadamu ndivyo tulivyoumbwa, kuna kuumwa na usipoumwa tushukuru Mungu.”
Akizungumzia matibabu yake, Mbatia alisema ilitumika teknolojia ya kisasa kwenye upasuaji huo uliochukua saa nne kutokana na tatizo la mguu lililoanza akiwa na umri wa miaka 15.
No comments:
Post a Comment