ANGALIA LIVE NEWS

Monday, December 12, 2016

SHEIKH PONDA AMTEMBELEA LEMA GEREZANI

KATIBU wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania, Sheikh Issa Ponda, amemtembelea Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema (Chadema) katika Gereza la Mahabusu Kisongo,  nje ya mji wa Arusha.

Sheikh Ponda alimtembelea Lema jana   kumjulia hali yake.

Lema anaendelea kushikiliwa katika mahabusu hiyo baada ya kukosa dhamana ya mashitaka ya uchochezi  yanayomkabili.

Taarifa ya Sheikh Ponda kufika gerezani hapo ilitolewa jana na aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa Baraza la Vijana la Chadema (Bavicha) Wilaya ya Arusha Mjini, Noel ole Varoya, alipozungumza na MTANZANIA.

“Leo (jana) Sheikh Ponda alikuwa gerezani Kisongo kumtembelea Lemba ambako alimtia moyo huku akimtaka aendelee na mapambano ya kuwapigania Watanzania.


“Alisema alikwenda kumsalimia na siyo kumpa pole kwani ni watu wachache kama Lema ambao wana moyo wa kupigania wanyonge.

“Alimwambia  wanapomuweka ndani hawampunguzii umaarufu wala hawamrudishi nyuma, asifikiri atakuwa dhaifu kwa kukaa gerezani bali wanazidi kumuimarisha kwa sababu watu wa nje na ndani ya Tanzania wanatambua anapigania haki za wanyonge.

“Alimshauri atakakapotoka gerezani, asiache kupigania haki za wanyonge,” alisema Ole Varoya akimnukuu Sheikh Ponda.

Lema alikamatwa Novemba 2, mwaka huu nje ya viwanja vya Bunge mjini Dodoma na kufikishwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha, Novemba 8 mwaka huu akikabiliwa na kesi mbili za uchochezi.

Katika mashauri hayo alishindwa kupata dhamana kutokana na maombi ya mawakili wa Serikali waliodai   Lema anakabiliwa na kesi nyingine mbili za uchochezi katika mahakama hiyo na hivyo asipewe dhamana.

Desemba 2 mwaka huu, mahakama hiyo ilifuta rufaa ya Lema baada ya rufaa hiyo kukatwa nje ya muda.

Mawakili wake walitakiwa kuwasilisha kusudio la kukata rufaa ndani ya siku 10 tangu uamuzi wa maombi ya marejeo ya mwenendo na uamuzi wa mahakama ya chini kutupwa na Mahakama Kuu, Kanda ya Arusha.

No comments: