ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, December 14, 2016

TRA: Makanisa yasichanganye sadaka na mapato mengine

By Raymond Kaminyoge na Hadija Jumanne, Mwananchi mwananchipapers@mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imewataka maparoko na viongozi wengine wa makanisa kutochanganya sadaka na mapato mengine wakati wakiandaa hesabu zao kwani hiyo inaweza kusababisha watozwe kodi kubwa ya mapato isivyostahili.

Hayo yalisemwa jana na Meneja wa Elimu kwa Mlipakodi wa mamlaka hiyo, Diana Masala alipokuwa akizungumza kwenye semina za viongozi wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Dar es Salaam.

Alisema, “Kwa kuwa sadaka na zaka huwa hazitozwi kodi, wakati wa kuandaa hesabu zenu za mapato ya kanisa ni lazima myatenganishe ili ijulikane sadaka ni ipi na mapato mengine ni yapi. Kuyajumuisha mapato hayo pamoja bila ya kuchanganua, mtatozwa kodi kubwa kinyume na kanuni za TRA.”

Alisema hesabu hizo zinatakiwa kuwa na akaunti tofauti hata kwenye benki.

Akitoa mada, Masala alisema hata taasisi za dini zinazofanya biashara ambazo asilimia 75 ya mapato yake yanatumika kwa ajili ya huduma kwa jamii, nazo zimesamehewa kodi.

“Kama taasisi ya dini inafanya biashara, lakini sehemu kubwa ya mapato yake inasaidia huduma mbalimbali ikiwamo afya na elimu hazitozwi kodi,” alisema.

Alisema lengo la semina hiyo kwa viongozi hao wa dini ni kuwapa elimu kwa kuwa wao pia ni miongoni mwa walipakodi.

“Taasisi za dini kama makanisa yanamiliki shule, kumbi za starehe, hivyo ni lazima tuwape elimu ya namna ya ulipaji sahihi wa kodi,” alisema.

Akizungumza kuhusu semina hiyo, Mjumbe wa Kamati ya Fedha na Uchumi wa Kanisa jimbo hilo, Padri Novatus Mbaula alisema itawapa uwezo wa kufahamu masuala mbalimbali yanayohusu kodi.

Alisema mafunzo hayo yatawasaidia kujua kodi wanazotakiwa kulipa na zile ambazo wamesamehewa.

Wakati mafunzo hayo yakiendelea, TRA ilitoa nafasi kwa viongozi hao kuhakiki Namba ya Utambulisho ya Mlipakodi (TIN).

Wawili kortini

Wakati huohuo, maofisa wawili wa TRA na kibarua mmoja wamefikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Ilala kujibu mashtaka matatu ya kuomba na kupokea rushwa.

Washtakiwa hao ni Liberatus Rugumisa (30), Keneth Mawere (29) ambao ni maofisa wasaidizi wa kodi wa TRA na Nassoro Nassoro (42) ambaye ni kibarua.

Wakili wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana Rushwa (Takukuru), Lupyana Mwakatobe alidai mbele ya Hakimu Mkazi Adelf Sachore kuwa shtaka la kwanza la kuomba rushwa linawakabili Rugumisa na Mawere wanalodaiwa kulitenda Novemba 18 katika ofisi za TRA, Kariakoo. Wanadaiwa kuomba rushwa ya Sh50 milioni kutoka kwa mfanyabiashara Humphrey Lema ili wampunguzie kodi.

Katika shtaka la pili, Mwakatobe alidai Novemba 23 katika duka la kubadilishia fedha za kigeni la Cate Bureau de Change, Mtaa wa Nyamwezi na Donge, Kariakoo washtakiwa walijipatia Sh10 milioni kutoka kwa Lema ili wampunguzie kodi.

Alidai kuwa katika shtaka la tatu ambalo linawakabili wote watatu, inadaiwa kuwa Desemba Mosi katika ofisi za TRA, Kariakoo, kwa pamoja na kwa njia ya ushawishi, walipokea rushwa ya dola za Marekani USD 2,744 kutoka kwa mfanyabiashara huyo ili wampunguzie kodi.

Washtakiwa walikana mashtaka na Hakimu Sachore, aliahirisha kesi hiyo hadi Desemba 27 itakapotajwa na walirudishwa rumande baada ya kushindwa kutimiza masharti ya dhamana ya kuwa na wadhamini wawili kutoka taasisi inayotambuliwa na Serikali watakaosaini Sh2 milioni kila mmoja.

No comments: