WANAWAKE NA MAENDELEO FOUNDATION
D A R ES SALAAM | IJUMAA |DESEMBA
2, 2016
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Katika gazeti la Raia Mwema
toleo No 486 la Tarehe 30 Novemba, 2016 kumeandikwa habari yenye kichwa
kilichosomeka “Mali za Salma Kikwete kuuzwa kwa mnada?”. Katika habari hiyo kumetolewa madai ati kwamba
taasisi ya WAMA inayoongozwa na Mheshimiwa Mama Salma Kikwete inao mzigo mkubwa
bandarini ambao haujalipiwa ushuru na kodi. Na kwa sababu hiyo, Mamlaka ya
Mapato Tanzania imepanga kuuza mali hizo.
Kwa niaba ya Taasisi ya WAMA
napenda kutoa masikitiko yetu kwamba habari hizo ni za uongo na hazina ukweli
wowote. Kwa maoni yetu gazeti hilo lina dhamira mbaya dhidi ya Taasisi ya WAMA
na Mwenyekiti wake, Mheshimiwa Mama Salma Kikwete. Nia yao ni kupaka matope na
kuchafua majina na sifa ya taasisi yetu na kiongozi wake.
Ukweli kuhusu jambo hili ni
kwamba, WAMA ilitumiwa maboksi Kumi na Moja (11) ya vitabu vikiwa ni zawadi
(grant) kutoka Nakayama Foundation ya Japani ambayo ndiyo iliyofadhili ujenzi
wa Shule ya Sekondari ya WAMA-Nakayama iliyopo Nyamisati, Kibiti. Maboksi hayo yaliyotumwa
kupitia BL 243016002211 yaliwasili bandarini tarehe 27/06/2016. Yalitolewa tarehe
10/8/2016 baada ya WAMA kulipia kodi zote na ushuru wote unaotahili tarehe
26/07/2016.
Vitabu hivyo vimekwishapelekwa
shuleni na wanafunzi wanavitumia. Hakuna mzigo wowote wa Taasisi ya WAMA uliopo
bandarini unaosubiri kutolewa wala kuuzwa na TRA. Hivyo basi, gazeti hilo
kuandika kuwepo kwa mzigo mkubwa wa WAMA bandarini ni jambo la kughushi ambalo limefanywa
kwa dhamira mbaya na kwa sababu wanazozijua wao.
Tumelitaka gazeti la Raia Mwema
limuombe radhi Mwenyekiti wa WAMA Mheshimiwa Mama Salma Kikwete na kuiomba
radhi WAMA Foundation kwa kuandika taarifa za uongo. Gazeti hilo limechafua sifa
ya Mwenyekiti wa WAMA na WAMA Foundation kiasi ambacho wanao wajibu wa kuomba
radhi na kusafisha majina na heshima zetu mbele ya jamii.
Ikiwa hawatatekeleza haya ndani
ya kipindi cha siku Saba, yaani kabla ya tarehe 07 Desemba, 2016, tutalazimika
kuchukua hatua zipasazo za kisheria.
Daudi Nasib,
Katibu Mtendaji,
Dar es Salaam,
Tel: +255 22 2781287
info@wamafoundation.or.tz
How comes Mama Kikwete kuitwa Mheshimiwa?
ReplyDelete