ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, December 14, 2016

WATUMISHI WA KARAKANA ZA TEMESA WAPATIWA MAFUNZO ELEKEZI.

 Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme - TEMESA Dkt. Mussa Mgwatu (aliyesimama) akifungua mafunzo elekezi kwa watumishi wa karakana za TEMESA juu ya mfumo wa utozaji gharama katika karakana za TEMESA pamoja na mfumo wa utoaji taarifa za kila mwezi, yanayofanyika katika ukumbi wa Karakana ya MT. Depot Dar es Salaam. Kushoto ni Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Uendeshaji Bw. Hans Lyimo na kulia ni Kaimu Mkurugenzi wa Uzalishaji na Matengenezo Mhandisi Sylivester Simfukwe.
 Watumishi kutoka Karakana za Wakala wa Ufundi na Umeme – TEMESA wakimsikiliza Mtendaji Mkuu Dkt. Mussa Mgwatu (hayupo pichani) katika ufunguzi wa mafunzo elekezi juu ya mfumo wa utozaji gharama katika karakana za TEMESA pamoja na mfumo wa utoaji taarifa za kila mwezi, yanayofanyika katika ukumbi wa Karakana ya MT. Depot Dar es Salaam.
  Watumishi kutoka Karakana za Wakala wa Ufundi na Umeme – TEMESA wakimsikiliza Mhandisi Sylivester Simfukwe (aliyesimama) katika mafunzo elekezi juu ya mfumo wa utozaji gharama katika karakana za TEMESA pamoja na mfumo wa utoaji taarifa za kila mwezi, yanayofanyika katika ukumbi wa Karakana ya MT. Depot Dar es Salaam.
 Wawakilishi kutoka Karakana ya TEMESA Pwani wakifuatilia kwa makini mada mbali mbali katika mafunzo elekezi juu ya mfumo wa utozaji gharama katika karakana za TEMESA pamoja na mfumo wa utoaji taarifa za kila mwezi, yanayofanyika katika ukumbi wa Karakana ya MT. Depot Dar es Salaam. Picha zote na Theresia Mwami TEMESA

Na Theresia Mwami TEMESA
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme - TEMESA Dkt. Mussa Mgwatu leo amefungua mafunzo elekezi kwa watumishi wa karakana juu ya mfumo wa utozaji gharama za matengenezo ya magari katika karakana za TEMESA pamoja na mfumo wa utoaji taarifa za uzalishaji na matengenezo za kila mwezi.

Dkt. Mgwatu amesema kuwa mafunzo hayo yamelenga kuleta uwiano sawa katika gharama za matengenezo ya magari kwa karakana zote za TEMESA bila kujali mikoa zilipo karakana hizo.

Aliongeza kuwa utaratibu utakaoelekezwa katika mafunzo hayo utasaidia kupunguza gharama za matengenezo ya magari ya serikali, suala linalolalamikiwa na wateja wa TEMESA kwa muda mrefu sasa.

“Nataka sasa tuanze kutoza gharama za matengenezo ya magari kulingana na muda unaotumika kutengeneza gari husika (man hour), badala ya kutumia kigezo cha asilimia ya fedha iliyotumika kununulia vipuri kwa ajili ya matengenezo ya magari, kwani baadhi ya vipuri ni ghali sana lakini hutumia muda mchache sana kuvifunga,” alisema Dkt. Mgwatu.

Dkt. Mgwatu alisema kuwa, kumekuwa na changamoto ya uwasilishaji wa taarifa za utendaji kutoka katika mikoa/vituo vya TEMESA, mara nyingi taarifa hizi hazifiki kwa wakati. Huku akisisitiza kuwa ni matumaini yake baada ya mafunzo hayo taarifa hizo zitakuwa zikifika kwa wakati tena zikiwa sahihi.

Aidha Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Uzalishaji na Matengenezo, Mhandisi Sylivester Simfukwe alisema idara yake imejipanga kutoa huduma bora zinazokidhi viwango hasa katika matengenezo ya magari ya serikali, ili kuhakikisha kuwa uzalishaji unaongezeka na kero za wateja zinakwisha. Aliongeza kuwa mafunzo kama hayo yatatolewa kwa wawakilishi wa karakana zote za TEMESA nchi nzima.

Mafunzo hayo elekezi juu ya Mfumo wa utozaji gharama katika karakana za TEMESA pamoja na mfumo wa utoaji taarifa za kila mwezi, yanafanyika kwa siku 5 katika ukumbi wa MT. Depot, Dar es salaam na yamehusisha watendaji wa TEMESA kutoka mikoa ya Tanga, Morogoro, Pwani, Dar es Salaam, Lindi na Mtwara, pamoja na vituo vya MT. Depot na Kikosi cha Umeme.

No comments: