Wednesday, December 7, 2016

Wenye mabasi kuanza kutumia EFDs

MAMLAKA ya Udhibiti Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra), Mkoa wa Mbeya, imewataka wamiliki wa mabasi ya abiria kwenda mikoani na wilayani, kuhakikisha wanawasilisha taarifa za mabasi yao ili ziingizwe kwenye mitandao kwa matumizi ya tiketi za mfumo wa kielektroniki.

Taarifa hiyo ilitolewa jana na Ofisa Mfawidhi wa Sumatra, Mkoa wa Mbeya, Denis Daudi, alipokuwa akizungumza na MTANZANIA.

Katika utekelezaji wa mpango huo, Daudi alisema wameshaingia mkataba na kampuni moja binafsi itakayofanya kazi ya kusajili mabasi na kuingiza taarifa zake kwenye mitandao kwa ajili ya matumizi ya mfumo wa mashine za kielektroniki ziitwazo EFD.

“Mfumo huo hautofautiani na mfumo unaotumiwa na makampuni ya ndege na zoezi hilo linatarajia kuanza rasmi wakati wowote kuanzia sasa.

“Malipo yote yatafanyika kwa njia ya mtandao kwani mpango huo utapunguza usumbufu mkubwa waliokuwa wakiupata abiria wakati wa kukata tiketi.


“Katika suala hili, tumejipanga kudhibiti upandaji holela wa nauli zinazotozwa na mabasi yanayosafirisha abiria mikoani na wilayani hasa katika kipindi cha sikukuu.

“Awali, waliokuwa wakipandisha nauli walikuwa wakitozwa faini ya shilingi 250,000, lakini imeonekana adhabu hiyo ni ndogo kwani asilimia kubwa ya wakosaji, hutekeleza adhabu hiyo na kuendelea na safari.

“Kwa hiyo ili kukabiliana na tabia hiyo, tumejipanga kuwa na mbinu mpya zitakazowafanya wakosaji wajutie makosa yao badala ya utaratibu wa awali wa kulipa faini kuonekana hauwafanyi wajifunze,” alisema.

Pamoja na hayo, alisema katika kipindi cha mwaka wa fedha wa 2015/2016, Sumatra mkoani hapa walikusanya Sh milioni 166. 25 zilizotokana na faini za makosa 665 yaliyotokana na upandishaji wa nauli bila kufuata utaratibu.

No comments:

Post a Comment

bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake