Hatimaye Makampuni matano yanayomilikiwa na Mfanyabiashara Yusuf Mehbub Manji yameondolewa katika Jengo la Quality Plaza linalomilikiwa na Shirika la Hifadhi ya Jamii PSPF.
Jengo hilo lipo Kitalu Na. 189/2 na liko mkabala na Barabara ya Nyerere jijini Dar es Salaam.
Sababu inayotajwa ya Makampuni hayo kuondolewa katika jengo hilo ni deni la kodi ya pango linalofikia kiasi cha Shilingi bilioni 13.
Hatua ya kung'olewa makampuni hayo katika jengo hilo ambalo ni mali ya Mfuko wa Pensheni wa Watumishi wa Umma ni baada ya mpangaji kushindwa kuondoka kwa hiari baada ya kupewa saa 24.
Makampuni yaliyondolewa ni Quality Group Company Limited, Gaming Management Limited, Q-Consult Limited, Quality Logistics Company Limited, na International Transit Investment Limited.
Jeshi la Polisi lilisimamia wakati kampuni ya udalali ya Yono Auction Mart ikizihamisha kampuni hizo za Yusuf Manji.
Inadaiwa kuwa Mfuko wa PSPF kwa muda mrefu umekuwa unaidai Kampuni ya Quality Group fedha hizo za upangaji, lakini kila inapotakiwa kulipa imekuwa ikikwepa na kukimbilia mahakamani kuweka pingamizi la kulipa ili iendelee kukaa bure na kwamba uamuzi wa Mahakama Kuu uliotolewa Novemba 24, umemtaka aondoke ndani ya saa 24 na kulipa deni analodaiwa.
Pia mmiliki wa kampuni hizo, japo amekwisha ondolewa katika jengo hilo amepewa muda wa siku 14 kisheria awe amelipa deni hilo na kama atashindwa kulipa mali zake zitakamatwa na kuuzwa ili kupata fedha za kulipa deni analodaiwa na PSPF.
No comments:
Post a Comment