Katika ziara yake hiyo, Profesa Ndulu, alipatiwa taarifa fupi kuhusu utendaji wa kiwanda hicho ikiwemo mipango yake ya kuongeza uzalishaji.
Akizungumza na menejimenti ya kiwanda hicho, aliipongeza kampuni hiyo kwa kufanya mageuzi makubwa ya uzalishaji ikiwemo mpango wa KSL wa kuwaongezea ujuzi wafanyakazi wake.
Kiwanda hicho kimekuwa kikitoa mafunzo kwa wafanyakazi wake ya programu mbalimbali ikiwemo teknolojia za kisasa za uzalishaji wa sukari na maendeleo ya ufundi stadi.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa KSL, Ashwin Rana alisema kiwanda hicho kinatarajiwa kuzalisha tani 68,000 za sukari msimu huu, ingawa kumekuwa na tatizo la ukame tangu mwaka jana.
Alielezea mipango na mikakati ya kukuza kiwanda hicho ya miaka mitano, kuwa ina lengo la kuoneza uzalishaji ili kuendana na nia ya Rais John Magufuli ya kuifanya Tanzania iwe nchi ya kujitegemea ifikapo 2021.
Alisema kiwanda hicho kinatarajia kutumia rasilimali zilizopo ikiwemo ardhi, maji na rasilimali watu ili kuiwezesha sekta sukari kuimarika lakini pia kukifanya kiwanda hicho kiwe kinaongoza nchini kwa uzalishaji wa sukari.
Naye Mwenyekiti wa kiwanda hicho, Seif Ally Seif, alimuomba Gavana Ndulu huyo kufuata mfano wa nchi zinazoongoza kwa uzalishaji wa sukari, kwa kuwawekea masharti nafuu ya kifedha wawekezaji.
Kwa upande wake, Profesa Ndulu, alipongeza rekodi nzuri ya uzalishaji wa kiwanda hicho na kuihakikishia Menejimenti ya KSL kuwa atayafanyia kazi mambo yao ili kuwasaidia kukuza sekta hiyo. Alisema endapo serikali itawasaidia wafanyabiashara wa sukari, itasaidia kutengeneza ajira, kuingiza fedha za kigeni na kukuza viwanda.
HABARI LEO
No comments:
Post a Comment