Advertisements

Friday, January 20, 2017

JIONEE: ULIPOFIKIA UJENZI WA JENGO JIPYA AIRPORT DAR ( TERMINAL 3)


SERIKALI inatarajia kukamilisha ujenzi wa jengo la abiria namba tatu kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), Dar es Salaam kwa fedha zake za ndani ifikapo Desemba mwaka huu.

Fedha za awamu ya kwanza ya ujenzi wa jengo hilo zilikuwa ni za mkopo kutoka katika Benki ya HSBC, na katika awamu ya pili serikali inatarajia kutumia Euro 121,634,888 (sawa na Sh bilioni 290.2) kukamilisha ujenzi huo.

Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa wakati alipotembelea uwanjani hapo ili kufanya ukaguzi wa maendeleo ya ujenzi huo unaotarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwaka huu.

“Awamu ya kwanza ilikuwa ni mkopo lakini awamu ya pili Serikali tumesema hatutachukua mkopo, tutalipa kwa pesa zetu za Kitanzania,” alisema Profesa Mbarawa.

Alisema utaratibu wa kujenga uwanja huo kwa pesa za ndani si wa kwanza kwani kuna miradi mingi na hasa katika sekta ya barabara ambayo inatekelezwa kwa utaratibu huo.

Awali, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege (TAA), Salim Msangi alisema mradi huo unakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo fedha za kulipia Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) .

HABARI LEO

1 comment:

Anonymous said...

Safi sana chini ya uongozi wa Magufuli na wasaidizi wake watanzania tunaimani kubwa ya ukamilikaji wa miradi mingi ya maendeleo inayoedelea kujengwa, Mungu atawapa uwezo zaidi,Amen.