Advertisements

Thursday, January 12, 2017

Maiti 12 ajali ya jahazi Tanga watambuliwa

Sehemu ya hospitali ya Bombo
Bombo Hospital

MAITI 12 walioopolewa jana katika Bahari ya Hindi, wametambuliwa na kuchukuliwa na ndugu zao kwa maziko. Maiti hao ni wa ajali ya jahazi namba Z5512 Mv Burudani.

Walikuwa wamehifadhiwa katika Hospitali ya Mkoa wa Tanga ya Bombo.

Kati yao, wamo watu wazima wanaume wanne, wanawake watatu na watoto watano, wakiwemo wasichana wawili na wavulana watatu, ambao walikuwa wamefuatana na wazazi wao safarini. Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Bombo, alibainisha hayo jana wakati akitoa taarifa kwa vyombo vya habari.

“Waliotambuliwa na ndugu zao ni Badru Said (60) mkazi wa Pemba, Muddy Mrisho (20) na Halima Songoro (29) wakazi wa Muheza, Muhidin Said (23) mkazi wa Mikanjuni, Mwanashari na Mariam Sheriff wote wakazi wa Chongoleani jijini Tanga,” alisema.

“Watoto waliofariki ni Fatuma Abdi Kombo (6), Hadija Abdi (2), Ally Masudi Abdala (5), Yusuf Masudi Abdalla (3) wote wakazi wa Msakangoto na Murhati Yusuf (5) mkazi wa Mikanjuni jijini Tanga na hakuna maiti wengine zaidi walioongezeka,” alisema Dk Mbwilo.

Akizungumzia afya za majeruhi 33 walionusurika kwenye ajali hiyo na kufikishwa kwa nyakati tofauti hospitalini hapo jana, Dk Mbwilo alisema wengi wameruhusiwa kurejea nyumbani, isipokuwa watano.

“Kati ya majeruhi watano waliosalia wodini watatu ni wanawake waliolazwa katika wodi ya A2 ambao wanajumuisha watoto wadogo wawili. Majeruhi wengine wawili ni wanaume wamelazwa katika wodi ya A1 ambapo baada ya kuwaona leo (jana) asubuhi nimeridhika afya zao zimeimarika na punde tutawaruhusu kurudi nyumbani ili wakaungane na familia zao,” alisema.

Aliongeza,”Kati ya hao majeruhi wanawake, huyo mmoja ambae ni mtu mzima tumeamua kuendelea kubaki naye kwasababu anavyoonekana amechanganyikiwa na kwa uchunguzi wetu tumeona tatizo hilo alikuwa nalo tangu awali kabla ya kunusurika kwenye ajali hiyo”, alisema.

Kwa upande wake, Ofisa Mfawidhi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Usafirishaji wa Nchikavu na Majini (Sumatra) Mkoa wa Tanga, Walukani Luhamba akitoa taarifa kwa vyombo vya habari jana, alisema kutokuwepo kwa udhibiti wa kutosha katika bandari bubu, kumekuwa kukitoa fursa kwa wamiliki wa vyombo vya uvuvi na mizigo kati ya miji ya Tanga na Pemba, kukiuka masharti ya leseni zao.

“Kiukweli hakuna jahazi lolote lililosajiliwa kusafirisha abiria kati ya Tanga na Pemba. Jahazi la MV Burudani lililopata ajali juzi limesajiliwa kisiwani Zanzibar kwa shughuli za uchukuzi wa mizigo tu na si vinginevyo, lilipaswa kupakia au kushusha mizigo kuanzia saa 12 asubuhi hadi saa 12 jioni na sio kusafiri nyakati za usiku kama iliyofanyika juzi,” alisema.

Aliongeza,”Msimamo wetu Sumatra ni kwamba bandari rasmi tunazozitambua ni mbili tu ikiwemo ya hapa jijini Tanga na ile iliyoko wilayani Pangani hakuna nyingine…Jahazi hili lililopata ajali ni kati ya vyombo vinavyotoroka kwenye mwambao wa Bahari ya Hindi kupitia bandari zisizo rasmi (bubu) ambazo huvusha bidhaa zinazokwepa kodi na kusafirisha abiria kwa kificho nyakati za usiku”.

Alipoulizwa kuhusu uhalali wa bandari ya Kasera kutumiwa na baadhi ya wamiliki wa majahazi ili kusafirisha abiria, alisema kituo hicho kimesajiliwa kwa shughuli za kupakia na kushusha mazao ya uvuvi pekee.

“Bandari ndogo ya Kasera ni kituo cha kushughulikia uvuvi ambacho kina vyombo zaidi ya 200 vinavyotumiwa na wavuvi wanaoendesha kazi zao kwa kuhamahama kutokana na msimu wa mazao ya uvuvi. Sumatra tunawajibika kuwapa vyeti vya ubora wa vyombo kabla ya idara ya uvuvi kuwapa leseni,” alisema.

Akijibu kuhusu kutokuwepo kwa mfumo maalumu wa utambuzi na mawasiliano ndani ya majahazi, Mkaguzi wa Vyombo wa Sumatra Mkoa wa Tanga, Christopher Mlelwa alisema kwa sasa hakuna matumizi hayo.

Hata hivyo, alisema kwa kuwa shughuli za usafirishaji abiria kwa njia ya bahari katika maeneo ya mwambao wa Bahari ya Hindi mkoani Tanga, bado ni changamoto, Sumatra kwa kushirikiana na wadau itaendelea kuhamasisha wamiliki wa boti, zilizosajiliwa kwa safari za majini, kuanzisha safari kati ya miji ya Pemba na Tanga ili kuwezesha abiria kusafiri salama.

Ajali za mara kwa mara, zinazohusu majahazi na boti za kubeba abiria kinyume cha sheria, zinatokana na kutowepo kwa usafiri wa meli kati ya Tanga na visiwa vya Unguja na Pemba.

HABARI LEO

No comments: