Michuano hiyo itakayofanyika Gabon inatarajiwa kuanza keshokutwa hadi Februari 5 mwaka huu ambapo mataifa 16 yatashiriki.
Nape akizungumza katika hafla ya kumkabidhi bendera ya taifa Diamond Dar es Salaam jana, alisema kitendo cha msanii huyo kwenda kutumbuiza katika ufunguzi huo ni heshima kubwa kwa Tanzania.
Alimtaka Diamond kwenda kuliwakilisha vizuri taifa licha ya timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, kutopata nafasi ya kushiriki fainali hizo.
Nape pia aliishukuru Multi- Choice-Tanzania kwa kukubali kuwapatia tiketi sita wasanii wa Diamond ili kwenda kunogesha shoo hiyo ya mwanamuziki huyo mwenye mafanikio makubwa nchini.
Alisema nafasi ya Diamond angeweza kupewa msanii mwingine yeyote nyota kutoka katika nchi zinazojiita mahiri katika tasnia hiyo, na badala yake amepewa Mtanzania huyo.
Alisema hiyo ni fursa kubwa kwa Diamond kuitangaza Tanzania kimataifa katika muziki. Naye Diamond alimshukuru Nape kwa kupiga hodi MultiChoice na kuwaombea tiketi wasanii wake.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa MultiChoice- Tanzania, Salum Salum alisema Afcon ni uhondo mwingine kwa Watanzania kwani DStv ndio chaneli pekee itakayoonesha fainali hizo.
“DStv ndio itakuwa chaneli pekee yenye ruksa ya kuonesha fainali hizo za Afcon na TV nyingine yeyote ikionesha hapa nchini itakuwa inaiba matangazo,” alisema Salum.
Wiki iliyopita Diamond alipata fursa ya kutumbuiza wakati wa utoaji wa tuzo za wachezaji bora wa mwaka wa Afrika zilizoandaliwa na Shirikisho la Soka la Afrika (Caf) zilizofanyika Abuja, Nigeria.
Katika uzinduzi huo, Diamond ataimba kibao maalumu pamoja na wasanii Mohombi na Franco, kibao ambacho pia kitakuwa wimbo maalumu wa mashindano hayo.
HABARI LEO
No comments:
Post a Comment