WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amesema nchi haijakumbwa na baa la njaa na amewataka Watanzania
utosikiliza kampeni za upotoshwaji zinazofanywa na baadhi ya wafanyabiasha kuhusu
hali ya chakula kwani si za kweli bali ni za uzushi zenye lengo la kupandisha bei za vyakula.
Amesema
Serikali ndio yenye jukumu la kutoa taarifa za kuwepo kwa njaa ama kutokuwepo na
kwamba taarifa zinazosambazwa za kuwepo kwa baa la njaa nchini hazina ukweli
wowote na Serikali inawahakikishia wananchi kuwepo kwa usalama wa chakula.
Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo leo (Jumatatu, Januari 16, 2017) wakati akizungumza na waandishi wa habari mkoani hapa mara baada ya kuzindua safari za ndege za Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) kutoka Dar es Salaam kwenda Dodoma, ambapo amesisitiza kwamba hali ya upatikanaji chakula nchini ni tofauti na inavyoelezwa na baadhi ya vyombo vya habari.
Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo baada
ya kutolewa kwa taarifa katika vyombo mbalimbali vya habari kuhusu kuwepo kwa
baa la njaa nchini jambo ambalo si la kweli. Amewataka wananchi kuwa watulivu
na jambo hilo likitokea Serikali itatoa taarifa.
“Mwaka
jana nchi ilikuwa na akiba ya chakula cha zaidi ya tani milioni tatu hali iliyopelekea baadhi ya Wabunge
na wafanyabiashara kuomba kibali cha kuuza nafaka nje ya nchi, ambapo Serikali
ilitoa kibali hicho baada ya kujiridhisha kuwepo kwa akiba ya kutosha ya
chakula,” amesema.
Amesema
baada ya kutolewa kwa kibali hicho tani milioni 1.5 ziliuzwa nje ya nchi na
Kiasi
cha tani milioni 1.5 zilizobaki zilihifadhiwa kama akiba ambapo tayari wameruhusu
ziuzwe hapa nchini ili kupunguza kupanda kwa bei za vyakula nchini.
“Naomba wananchi msiwe na wasiwasi juu ya hali ya chakula nchini. Msisikilize kelele zinazopigwa na watu mbalimbali pamoja kwenye baadhi ya vyombo vya habari yakiwemo magazeti kwani taarifa hizo si za kweli. Chakula kipo cha kutosha licha ya mvua kusuasua katika baadhi ya maeneo nchini,” amesema.
Hata
hivyo Waziri Mkuu amesema kuwa kwa sasa mvua zimeanza kunyesha katika maeneo
mbalimbali nchini, hivyo amewaomba wananchi kuzitumia kwa kulima mazao ya muda
mfupi yanayostahimili ukame.
Waziri
Mkuu amesema kwamba endapo kutatokea uhaba wa chakula nchini, Serikali itatoa
utaratibu wa namna ya upatikanaji wa chakula kwa wananchi wake. Kuhusu kupanda
wa bei ya vyakula katika baadhi ya masoko amesema inatokana na kuwepo kwa uhaba
wa chakula katika nchi jirani.
Aidha, Waziri Mkuu amesema kwamba Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi, itatoa taarifa kuhusiana na hali halisi ya chakula nchini kwa sasa na pia itatoa taarifa kuhusu hali ya mvua ili Watanzania waweze kupata ukweli wa hali ilivyo.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
S. L. P. 980,
DODOMA.
JUMATATU, JANUARI 16, 2017.
Toeni chakula na muombe kingine cha akiba acheni kutuzingua na kauli za kila kuchapo! Kwanini imekuwa kuwakejeeli wananchi kwanza halafu maneno matamu yanapenyezwa sasa. Kwani hali ya hewa na kilimo kuwa mbaya imeanza leo? Inakuwepo mara kwa mara na majukumu ya Serikali na taasisi kuwa pamoja kwa mfano kuombea mvua na kuwapa wananchi matumaini. Lakini sio mwaafaah. Mniombee!!
ReplyDelete