ANGALIA LIVE NEWS

Friday, January 13, 2017

Profesa Muhongo awekwa mtu kati

Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter
By Mwandishi Wetu, Mwananchi mwananchi@mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Kauli ya Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo kuwa hakushirikishwa katika kupandisha bei ya umeme imepingwa vikali na wasomi na wanasiasa ambao wamesema ni lazima alikuwa na taarifa kuhusu jambo hilo.

Kauli za wasomi na wanasiasa hao zimekuja siku moja baada ya gazeti hili kuandika habari inayoonyesha kuwa Profesa Muhongo alihudhuria kikao kilichojadili suala hilo na baadaye kuandika barua kwa Waziri wa Fedha na Mipango kumtaarifu mpango mkakati wa mwaka 2017 wa masuala ya gesi na umeme, likiwemo suala la Tanesco kutakiwa kuwasilisha mapendekezo ya bei mpya ndani ya siku mbili.

Profesa Muhongo alizuia utekelezaji wa bei mpya ya umeme, siku chache baada ya Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (Ewura) kutangaza kupanda kwa bei ya umeme kwa asilimia 8.5, akisema shirika hilo haliwezi kumaliza changamoto zake kwa kupandisha bei ya umeme.

Alisema kiutaratibu, Tanesco hutakiwa kupeleka Ewura marekebisho ya bei ya umeme na kabla ya mamlaka hiyo kutangaza, ni lazima waziri mwenye dhamana akabidhiwe ripoti ya mwisho, lakini badala yake akashtukia bei mpya ikitangazwa.

Pia alisema viongozi wa Tanesco wamekuwa wakijilipa bonasi ya kati ya Sh40 milioni na Sh60 milioni na hivyo matatizo ya shirika hilo hayawezi kutatuliwa kwa kuwabebesha mzigo wananchi.

Kauli yake ilifuatiwa na uamuzi wa Rais John Magufuli kutengua uteuzi wa mkurugenzi mkuu wa Tanesco, Felschemi Mramba.

Lakini wasomi waliohojiwa na Mwananchi wamepinga kauli yake pamoja na uamuzi wa kuzuia bei mpya, wakisema unakiuka misingi ya utawala bora.

Ali Mufuruki

“Inawezekanaje waziri asiwe na taarifa?” alihoji mwenyekiti wa Umoja wa Maofisa Watendaji Wakuu wa Kampuni (CEOrt), Ali Mufuruki.

“Barua yake kwa Tanesco niliyoiona kwenye mitandao ya kijamii inaonyesha hakushirikishwa. Muhongo anasema hakushirikishwa, na nyinyi (gazeti la Mwananchi la jana), mnaonyesha alishiriki, sasa nasubiri reaction ya wizara. Lakini siamini kama hakushirikishwa.”

Mufuruki alisema Muhongo alisema mambo mengi ya Tanesco wakati akifuta bei mpya ya umeme, hivyo anaamini Mramba hakutimuliwa kwa sababu ya bei mpya bali utendaji.

“Kama Mramba aliadhibiwa kwa tarrif za umeme, litakuwa jambo la kushangaza sana. Kama kuna issue (jambo) nyingine kuhusu Mramba, basi anayejua ni Serikali,” alisema.

Mufuruki pia alisema makosa yaliyofanyika awali ni waziri kufuta uamuzi uliotolewa na Ewura wakati waziri hana mamlaka hayo kisheria na hivyo ni kinyume na misingi ya utawala bora.

“Ewura ndiyo consultant (mshauri), ndiyo yenye mamlaka ya kupitia mchakato huo, kwa kukusanya maoni ya wadau. Kwa hiyo issue (suala) la (kufutwa kazi kwa) Mramba ilitushangaza sana hata sisi,” alisema Mufuruki.

Mufuruki alisema Serikali ni mteja wa Tanesco kama walivyo wateja wengine, hivyo haiwezi kujipangia bei, badala yake kama walivyo wateja wengine, ilitakiwa kuchukua hatua za kuwasilisha malalamiko yake Tume Huru ya Ushindani (FCC) au mahakamani ili uamuzi utolewe.

Profesa Mohamed Bakari

Msomi mwingine, Profesa Mohamed Bakari wa Idara ya Sayansi ya Siasa ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), alisema kauli ya waziri hiyo ni moja ya tabia za wanasiasa kubadilikabadilika.

“Tatizo lililopo ni wanasiasa kubadilika kulingana na upepo katika jambo linalojadiliwa kwenye jamii,” alisema Profesa Bakari.

Alisema endapo suala la kupanda kwa gharama za umeme lisingekuwa na msukumo wa wananchi, anaamini mkurugenzi huyo wa Tanesco asingeondolewa madarakani.

“Wanasiasa wana tabia za kugeukageuka. Ni rahisi kubadilika kwa njia zozote zile, iwe kwa visingizio ilimradi kutafuta uhalali wa kisiasa, aonekane amefanya uamuzi kwa maslahi ya wananchi hata kama alishiriki katika makosa,” alisema.

Emmanuel ole Naiko

Mkurugenzi mtendaji mstaafu wa TIC, Emmanuel ole Naiko naye alisema isingewezekana kwa mkurugenzi wa Tanesco kufanya uamuzi huo peke yake.

“Ninajua waziri (Muhongo) ni mtendaji mzuri na jasiri, lakini hatua hizo zitatupeleka pabaya. Suala la Tanesco limesikitisha sana kwa sababu mkurugenzi hawezi kufanya uamuzi huo peke yake. Sasa nashukuru kama (Mwananchi) mmegundua waziri alishiriki. Tusubiri tuone,” alisema.

Wadau wengine

Aliyekuwa mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila, ambaye aliibua kashfa ya escrow iliyohusu uchotwaji wa fedha zilizohifadhiwa kwa pamoja na Tanesco na kampuni ya ufuaji umeme ya IPTL, alisema waziri huyo alimpotosha Rais John Magufuli.

Alisema tatizo ni wanasiasa wengi kutafuta umaarufu aliouita wa “bei ndogo” bila kujali wanakiuka sheria na misingi ya utawala bora.

“Haiwezekani waziri aseme hatambui kupandishwa kwa bei za umeme wakati alishiriki mkutano wa Benki ya Dunia unaoonyesha alikubali. Hata barua ya Ewura ilionyesha wizara ilishirikishwa kupitia kwa katibu mkuu ambaye ndiye mtendaji, kwa hivyo taarifa za kupandisha bei alikuwa nazo,” alisema.

Mbunge wa Kigoma Mjini (ACT Wazalendo), Zitto Kabwe alisema kutokana na kitendo cha Profesa Muhongo na uamuzi dhidi ya aliyekuwa mkurugenzi wa Tanesco, watendaji wa taasisi za Serikali wataendelea kuathiriwa zaidi na hofu.

“Jambo lolote linapoharibika wanaoathirika ni watendaji wa chini. Mazingira hayo yatapunguza ari ya watendaji hao kufanya kazi kwa ubunifu,” alisema Zitto.

Zitto, ambaye amewahi kuwa mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), alisema kutokana na kitendo cha waziri, Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini inatakiwa kuandaa ajenda kwa ajili ya kumjadili.

Mwenyekiti wa Kamati ya Nishati na Madini, Doto Biteko alisema Jumatatu kamati hiyo zitaanza vikao vyake lakini kwa sasa, kamati hiyo haitaweza kumjadili waziri huyo kwani tayari imeshaandaa ratiba yake.

“Lakini mjumbe wa kamati anayo haki kuwasilisha ndani ya vikao, kwa kuwa waziri au naibu wake lazima atakuwapo kwenye vikao na atakuwa na nafasi ya kujibu pale au asiporidhika anaweza kuwasilisha katika vikao vya bunge,”alisema Biteko.

Kuhusu hoja ya Profesa Muhongo kuwa waziri alitakiwa apewe ripoti ya mwisho ya marekebisho ya bei ya umeme kabla ya kutangazwa, mkurugenzi mkuu wa Ewura, Felix Ngamlagosi alisema hataweza kuzungumzia suala la umeme, kwa kuwa lilishajadiliwa na kutolewa msimamo na Serikali.

No comments: